Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, likinukuu Islamic Analysis, wakati mchakato wa utakaso wa kikabila dhidi ya Wapalestina unaofanywa na utawala wa Kizayuni pamoja na waungaji mkono wake wa Magharibi ukiendelea, ripoti zimefichua nafasi ya baadhi ya miundo ya makanisa ya Magharibi katika kuzuia kusambazwa kwa simulizi zinazoikosoa Israel.
Agapia Stefanopoulos, mtawa wa Kanisa la Orthodox wa Marekani mwenye asili ya Kigiriki ambaye aliishi katika Monasteri ya Mtakatifu Maria Magdalena mjini Quds kati ya mwaka 1996 hadi 2006, na ambaye kwa miaka mingi ameifahamu kwa karibu hali ya Palestina, amesema kwamba; kutokana na kueleza alichokishuhudia kuhusu hali halisi ya Palestina, amekumbwa na vikwazo na marufuku ya kutoa hotuba kutoka kwa viongozi wa kanisa.
Muundo wa uongozi unaoogopa kusemwa ukweli
Mtawa Agapia katika mahojiano yake ya hivi karibuni na kituo cha YouTube “Reason2Resist with Dimitri Lascaris” alisisitiza kwamba; Israel hailengi tu utambulisho wa Kiislamu wa Palestina, bali pia inalenga urithi wa kihistoria na wa kina wa Wakristo wa Palestina.
Alisema kwamba; Ofisi ya Uaskofu Mkuu wa Kanisa la Orthodox la Kigiriki nchini Marekani imejaribu kuzuia ukweli huu kuwafikia waumini na wanachama wa kanisa, na kwa sababu hiyo, imeweka vikwazo dhidi ya hotuba zake.
Kwa mujibu wake, ukimya wa viongozi wa Kanisa la Orthodox kuhusu matukio ya Palestina unatokana kwa kiwango kikubwa na mahusiano yao ya karibu ya kisiasa na serikali ya Ugiriki, pamoja na hofu ya kupungua kwa nafasi na ushawishi wao.
Stefanopoulos anaamini kwamba baadhi ya viongozi wa kidini, kwa kuhofia kwamba kuikosoa Israel kunaweza kuhatarisha nafasi yao ya kisiasa na kijamii, wanatanguliza maslahi ya kisiasa na ya kimaada kuliko majukumu yao ya kimaadili na kidini.
Kuporomoka kwa simulizi la “muungano wa Kiyahudi na Kikristo”
Agapia Stefanopoulos pia alitoa kauli ambazo kwa mujibu wake zinatia shaka simulizi linaloenezwa katika vyombo vya habari vya Magharibi kuhusu “maadili ya pamoja ya Kiyahudi na Kikristo”.
Alidai kwamba; majeshi ya Israel katika vituo vya ukaguzi huwazuia Wakristo wa Palestina, na katika baadhi ya matukio wanawavua misalaba kutoka shingoni mwao na kuitupa.
Pia alizungumzia kuporwa kwa ardhi zinazomilikiwa na makanisa na shinikizo zinazoendelea dhidi ya Wakristo wa Palestina, na alidai kwamba; mchakato huu unawalazimisha kuhama kwa lazima na kuiacha ardhi yao.
Kwa mujibu wa mtawa huyo wa Kanisa la Orthodox, Uzayuni si tishio kwa Waislamu wa eneo hilo pekee, bali pia unaweka changamoto kwa uwepo wa dini zote za kihistoria na zenye mizizi ya Mashariki ya Kati.
Ukosoaji dhidi ya Uzayuni wa Kikristo
Stefanopoulos katika sehemu nyingine ya mazungumzo yake alikosoa itikadi ya “Uzayuni wa Kikristo”.
Anaamini kwamba mkondo huu, kwa kuifananisha dhana ya “Israel” katika Agano la Kale na dola ya kisasa ya Israel iliyoanzishwa mwaka 1948, unatoa tafsiri potofu na iliyopotoka ya mafundisho ya kidini.
Kwa mujibu wake, itikadi hii imejengwa juu ya aina fulani ya “udanganyifu wa kiroho” na haiendani na ujumbe na mafundisho ya Nabii Isa Masih (as).
Mtawa huyo wa Kanisa la Orthodox alisisitiza kwamba; kuunga mkono “ukandamizaji na vurugu dhidi ya Wapalestina” kunapingana kabisa na mafundisho ya msingi ya Ukristo kuhusu rehema, huruma na uadilifu.
Muqawama wa Palestina kwa mtazamo wa Agapia
Mwishoni, Agapia Stefanopoulos alielezea Muqawama wa Wapalestina kuwa ni mwitikio halali dhidi ya ukaliaji wa ardhi, na alisema kwamba; watu wa Ugiriki na wafuasi wa Kanisa la Orthodox, kwa kuzingatia uzoefu wao wa kihistoria katika kupigania uhuru na kutetea ardhi yao, wanapaswa kuwa na uwezo wa kuielewa vyema zaidi hali ya Wapalestina na kushirikiana nao kwa hisia na huruma.
Maoni yako