Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Ghazi Hanina, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Mkusanyiko wa Wanazuoni wa Kiislamu wa Lebanon, katika mazungumzo na mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza mjini Mashhad, huku akizungumzia vipengele vya kiitikadi na vya ustaarabu vya tukio la Ghadir, alisema: “Hakika ya Ghadir imejidhihirisha katika dhana ya Wilayah, na shakhsia ya Amirul-Mu’minin Ali (as) inachukuliwa kuwa mfano mkamilifu zaidi wa utekelezaji wa Wilayah ya Mwenyezi Mungu ndani ya jamii ya Kiislamu.”
Sira ya Alawi; mfano wa kudumu wa utekelezaji wa uadilifu
Akibainisha kuwa maisha ya Amirul-Mu’minin Ali (as) yalijaa kujitolea, kujitoa muhanga na kufanya juhudi katika njia ya haki, aliongeza:b“Mtukufu huyo, iwe kabla ya tukio la Ghadir au baada yake, daima alijitahidi kwa ajili ya kusimamisha uadilifu, kutetea maadili ya Kimungu na kulinda heshima ya wanadamu, na alitumia uwezo wake wote katika njia ya kusimamisha haki.”
Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Mkusanyiko wa Wanazuoni wa Kiislamu wa Lebanon aliendelea kusema: “Uchunguzi wa Sira ya Amirul-Mu’minin (as) unaonyesha kwamba kuzingatia uadilifu, kuwajibika na kuwatetea waliodhulumiwa ni miongoni mwa sifa muhimu zaidi za utawala na shakhsia yake, na sifa hizi ndizo zilizoyafanya madhehebu ya Alawi kuwa mfano wa kudumu kwa vizazi vyote.”
Ghadir; mtaji wa pamoja wa Waislamu kwa ajili ya umoja na muqawama
Sheikh Hanina huku akisisitiza kwamba ujumbe wa Ghadir haujawekewa mipaka ya dhehebu moja au kundi maalumu, alifafanua: “Dhana kama uadilifu, kutafuta haki, Wilayah na kupambana dhidi ya dhulma ni ujumbe wa jumla unaowahusu Waislamu wote, na unaweza kuwa mhimili wa mshikamano na umoja wa Umma wa Kiislamu.”
Alieleza: “Leo katika medani ya mabadiliko ya ulimwengu wa Kiislamu, Mashia na Masunni katika nyanja nyingi wanasimama pamoja kutetea malengo ya haki na uadilifu na wanapambana dhidi ya sera za kibabe na dhulma, bila shaka, kipimo kikuu katika medani hii si mafungamano ya kimadhehebu, bali ni kushikamana na maadili ya Kiislamu, uadilifu na kutetea haki.”
Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Mkusanyiko wa Wanazuoni wa Kiislamu wa Lebanon, huku akigusia ulazima wa kuimarisha umoja wa Kiislamu, alisema: “Waislamu wanapaswa kwa kuhamasishwa na mafundisho ya Ghadir na Sira yenye nuru ya Amirul-Mu’minin Ali (as), kuyaweka pembeni mazingira ya hitilafu na sababu za mifarakano, na kwa kuwa macho dhidi ya njama za maadui wa Uislamu, waendelee kufuata njia ya umoja, muqawama na heshima ya Umma wa Kiislamu.”
Alisisitiza kwa kusema: “Katika mazingira ya sasa, ulimwengu wa Kiislamu unahitaji zaidi kuliko wakati mwingine wowote kupitia upya dhana za msingi za Ghadir; dhana ambazo zinaweza kuwa msingi wa nguvu, maendeleo na ushindi wa Umma wa Kiislamu mbele ya changamoto zilizopo.”
Maoni yako