Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, wakati juhudi na hatua za mikondo mbalimbali ya kisiasa nchini Iraq za kukamilisha uundaji wa serikali mpya chini ya uongozi wa Ali Al-Zaidi zinaendelea, vyanzo maalumu na vyenye taarifa vimeripoti kuwepo kwa hujuma na vikwazo vilivyowekwa na Marekani. Lengo la hatua hizi ni kuzuia njia ya baadhi ya mikondo na shakhsia fulani kushika nafasi katika serikali mpya, huku wakati huohuo ikijaribu kulazimisha watu wanaowataka kushika nyadhifa nyeti za kiusalama.
Ali Al-Zaidi, Waziri Mkuu aliyeteuliwa, aliwasilisha baraza lake la mawaziri lililopendekezwa kwa Bunge la Iraq, ambalo tarehe 15 Mei lilifanikiwa kupata kura ya imani.
Inafaa kutajwa kwamba; watu wanaotakiwa kushika wizara tano, ikiwemo Wizara ya Ulinzi, hawakutambulishwa, Pia wagombea wa wizara nyingine nne, ikiwemo Wizara ya Mambo ya Ndani, hawakuweza kupata kura za wabunge wengi.
Kwa hivyo, hatima ya wizara 14 imekwishaamuliwa na wizara nyingine 9 bado zimebaki, huku matumaini yakiwa kwamba baada ya mapumziko ya Sikukuu Tukufu ya Eid al-Adha, suala lao litapatiwa ufumbuzi katika wiki ijayo.
Mikondo mbalimbali ya kisiasa, ikiwa ni pamoja na Mfumo wa Uratibu wa Kishia, Baraza la Kisiasa la Kisunni na pande kuu za Wakurdi, zikiwemo Chama cha Democratic cha Kurdistan kinachoongozwa na Masoud Barzani pamoja na Umoja wa Kizalendo wa Kurdistan unaoongozwa na Bafel Talabani, zinafanya mazungumzo marefu na ya mfululizo ili kutatua tofauti zilizopo na kufunga haraka iwezekanavyo jalada la kuundwa serikali.
Wakati huohuo, Washington, katika mwendelezo wa juhudi zake zisizokoma za kuzuia ushiriki wa mikondo inayohusishwa na Mhimili wa Muqawama katika serikali mpya, inaendelea kufanya harakati katika pande mbalimbali.
Mikondo hii imefanikiwa kupata zaidi ya viti 80 kati ya viti 329 vya Bunge la Iraq; jambo ambalo hata maafisa wakuu wa Marekani wamekiri hadharani.
Jumla ya viashiria na taarifa zinaonyesha kuwa; safari ya hivi karibuni ya Jenerali David Petraeus, aliyekuwa mkuu wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kwenda Iraq, pamoja na safari ambayo haikutangazwa ya Tom Barrack, mjumbe maalumu, ilikuwa katika mwelekeo wa kuongeza mashinikizo ili kulazimisha watu walio karibu na mitazamo ya Marekani kushika nyadhifa za kiusalama katika serikali mpya.
Jambo hili ni mbali na juhudi zinazoendelea bila kukoma za kuivunja Hashd al-Shaabi na kuijumuisha kwa namna fulani katika taasisi za kiusalama na kijeshi za serikali.
Vyanzo vyenye taarifa kuhusu mazingira ya mazungumzo ndani ya Mfumo wa Uratibu vimesema kwamba; vikundi vinavyounda mfumo huo vina msimamo wa pamoja wa kukataa aina yoyote ya kuingiliwa au maagizo kutoka nje katika kuchagua na kuamua shakhsia yoyote, iwe katika serikali mpya au katika nyadhifa nyingine za juu.
Wakati huo huo, miito na madai ya umuhimu wa kukomesha kabisa uwepo wa kijeshi wa Marekani katika ardhi ya Iraq, pamoja na kuzikomboa mali na rasilimali za Iraq kutoka chini ya udhibiti wa Marekani, vimeongezeka kwa kasi.
Maoni yako