Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, kikao cha nne katika mfululizo wa makongamano ya kielimu ya “Maadili ya Muqawama” yenye anuani ya “Misingi ya Wahyi na wajibu wa Qur’ani katika maadili ya Muqawama” kilifanyika kwa juhudi za Taasisi ya Kielimu na Kitamaduni ya Had mjini Qom Iran.
Muqawama; zaidi ya uwanja wa vita
Katika kikao hicho, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Hamid Malikii huku akifafanua vipengele vya Qur’ani na kimaadili vya Muqawama, alieleza kuwa; subira na ustahimilivu ni miongoni mwa nguzo za msingi kabisa za imani, na akasema: “Muqawama hauishii tu katika kuwepo kwenye uwanja wa vita, bali kila aina ya kusimama imara mbele ya adui, matamanio ya nafsi, vishawishi vya kishetani na kuhifadhi maadili ya Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa vielelezo vya Muqawama na ustahimilivu.”
Akiashiria kwamba subira ni hakika ya imani na mzizi wa uimara wa mwanadamu muumini, alisema: “Yeyote ambaye ataweza kusimama imara mbele ya maasi, matatizo na utiifu kwa Mwenyezi Mungu, atakuwa amepata sifa ya kimaadili ambayo Qur’ani inaielezea kuwa ni imani madhubuti na yenye kudumu.”
Qur’ani; kitabu cha uongofu, tiba na rehema
Naibu Mkurugenzi wa Hawza ya Qom kwa kurejea aya ya 57 ya Suratu Yunus, aliitambulisha Qur’ani Tukufu kuwa ni kitabu cha “mawaidha, tiba, uongofu na rehema”, na akaongeza: “Qur’ani kwanza humwamsha mwanadamu, kisha hutibu maradhi yake ya kiroho na kimaadili, na hatimaye humwekea mbele njia ya uongofu na kufikia rehema za Mwenyezi Mungu.”
Alisisitiza kuwa: “Kwa mtazamo wa Qur’ani, Muqawama bila ya maadili hauna maana. Katika shule ya Mwenyezi Mungu, lengo halihalalishi njia, na hata katika medani ya vita pia ni lazima kuhifadhi misingi ya kibinadamu na kimaadili.”
Imani ya Akhera; msingi mkuu wa Muqawama
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Hamid Malikii huku akieleza kwamba; imani ya Akhera ni miongoni mwa nguzo muhimu zaidi za Muqawama alisema: “Iwapo mwanadamu hatakuwa na msingi wa kimaadili na imani ya Akhera, hawezi kusimama katika njia ya haki wala kuwa na ustahimilivu mbele ya mashinikizo na matatizo.”
Muqawama una mizizi katika fitra ya mwanadamu
Aliendelea kwa kuashiria aya ya 30 ya Suratu Rum, na akaielezea aya hiyo kuwa ni miongoni mwa misingi muhimu zaidi ya kifitra ya Muqawama, akasema: “Mwenyezi Mungu katika aya hii anasema:
Mwanadamu anapaswa kuielekea dini ya Mwenyezi Mungu kwa uwepo wake wote, umakini na moyo wake wote.”
Naibu Mkurugenzi wa Hawza ya Qom aliongeza: “Uislamu si mkusanyiko tu wa hukumu za ibada, bali unajumuisha yote yanayopaswa kufanywa na yasiyopaswa kufanywa pamoja na sheria za mtu binafsi na kijamii, na umeletwa kwa ajili ya kutimiza maisha mema ya kibinadamu; yaani maisha yaliyo juu zaidi ya maisha ya kawaida ya mwanadamu.”
Akifafanua maana ya fitra ndani ya Qur’ani alisema: “Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu kwa namna ambayo anaweza kuitambua haki na pia kuvutiwa na mema. Mwanadamu kwa fitra yake ni wa kimaadili, wa kiroho, wa kimungu na mtafutaji wa haki, na ndani yake kumewekwa mapenzi ya heshima, utu, ukamilifu na umilele.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Ma'likii akirejea mtazamo wa Allameh Tabatabai alisema: “Allamah Tabatabai anaamini kuwa, kila haja iliyowekwa ndani ya mwanadamu ina uhalisia wake katika ulimwengu wa nje; ndio maana mwanadamu kwa fitra yake anatafuta ukaribu wa Mwenyezi Mungu, radhi Zake na ukamilifu wa mwisho kabisa.”
Vizuizi vya saada na ulazima wa ustahimilivu
Aliendelea kuzungumzia vizuizi vya njia ya saada na Muqawama, na akaongeza: “Mielekeo ya kimada kama matamanio, kuipenda dunia, kutafuta starehe, kurubuniwa na vishawishi vya nafsi ni miongoni mwa vizuizi muhimu zaidi vya harakati ya mwanadamu kuelekea ukamilifu.”
Mwalimu huyo wa Hawza ya elimu ya dini alikumbusha: “Mwanadamu ili avuke vizuizi hivi anahitaji imani madhubuti na mwelekeo wenye nguvu; mwelekeo ambao Mwenyezi Mungu ameuweka ndani ya fitra yake. Ikiwa mwanadamu atasalimu amri mbele ya dhambi na kuirudia rudia, ladha yake ya kiroho hubadilika na hupoteza uwezo wa kutofautisha haki na batili.”
Alisisitiza kuwa: “Kufikia saada na ukamilifu hakuwezekani bila ya Muqawama na ustahimilivu, na mwanadamu lazima aweze kusema ‘hapana’ mbele ya matamanio ya nafsi na mashinikizo ya nje.”
Ufafanuzi wa Qur’ani kuhusu kambi ya haki na batili
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Hamid Malikii pia huku akirejea Suratul Muhammad (saww), alielezea kwamba; Qur’ani imefafanua wazi kabisa kambi ya haki na ya batili, na akasema: “Qur’ani inaichukulia kambi ya batili kuwa ni wale wanaowazuia watu na njia ya Mwenyezi Mungu, na upande wa pili, kambi ya imani ni wale wanaounganisha imani na matendo mema.”
Aliongeza: “Sunna ya Mwenyezi Mungu imejengwa juu ya kuwasaidia waumini, na popote ambapo kuna imani, ustahimilivu na tawakkul, basi nusura ya Mwenyezi Mungu pia itapatikana.”
Naibu Mkurugenzi wa Hawza mwishoni akisisitiza umuhimu wa kuhifadhi roho ya Muqawama katika jamii ya Kiislamu alisema: “Kuishi pamoja na Qur’ani, kuimarisha imani na kuhifadhi roho ya ustahimilivu ni miongoni mwa sababu muhimu zaidi za heshima na nguvu ya Umma wa Kiislamu.”
Maoni yako