Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Akram Al-Kaabi, Katibu Mkuu wa Harakati ya Nujabaa, katika ujumbe wake alimpongeza Mtukufu Ayatollah Sayyid Mujtaba Khamenei kwa kuchaguliwa kwake kuwa Kiongozi wa tatu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Katika ujumbe huo imeelezwa kwamba:
Mtukufu Ayatollah Sayyid Mujtaba Khamenei:
Mwenyezi Mungu Mtukufu akujalie malipo makubwa kwa msiba wa shahidi wa Uislamu, kiongozi mwenye hekima na Sayyid mtukufu (Mwenyezi Mungu aitakase roho yake), pamoja na mashahidi wote wa mhimili wa muqawama, hasa watoto wasio na hatia wa shule ya msingi; na pia kwa mama yenu mtukufu, mke wenu mtukufu, dada yenu mpendwa pamoja na mume wake, na watoto wao wawili wadogo.
Heri yenu kwa kushiriki katika msimamo wa Imam Hussein (amani iwe juu yake), ambapo mmewatoa wapendwa wenu katika msafara wa Karbala kwa ajili ya njia ya haki.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu akujalieni upone haraka na kikamilifu kutokana na majeraha yaliyotokana na shambulio hili la kinyama na lisilo la kiungwana. Pia tunamuomba akujalie mafanikio yanayoendelea na akulinde kwa ulinzi wake wa kiungu.
Kwa miaka mingi iliyopita, tulipokuwa tukisikiliza hotuba na kauli zenu zilizojaa elimu, utamaduni na maarifa; zilizojaa uelewa wa kina kuhusu Iran na nchi nyingine; pamoja na uchambuzi wa kina wa matukio, upeo wa mbali wa fikra na mtazamo wa baadaye, utambuzi wa busara wa nguvu na udhaifu wa Umma wa Kiislamu na ufahamu wa njia za kukabiliana na changamoto; sambamba na daraja yenu ya juu ya ijtihad tuliyoifahamu, na sifa za kipekee za darsa zenu za kiwango cha juu (Dars al-Kharij), siku zote tuliamini kwamba Mwenyezi Mungu amekuandalia hadhi na nafasi kubwa sana.
Lakini pale Mwenyezi Mungu alipowaokoa kutoka chini ya vifusi vya mabomu ya utawala wa kikatili wa Kizayuni na Marekani na mkawa mmetoka salama, tulipata yakini kwamba yale tuliyokuwa tumeyaona awali yalikuwa ni kweli.
Ewe mrithi bora wa watangulizi bora, mmeinuka ili kuweka dawa juu ya majeraha yenu wenyewe, na pia kuponya majeraha ya nyoyo zetu, na kuuongoza Umma wa Kiislamu kutoka ushindi mmoja hadi ushindi mwingine; hadi siku mtakapoikabidhi bendera hiyo kwa Imam wa Zama (roho zetu ziwe fidia kwake).
Hivyo basi, kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu, mjue kwamba; mhimili mzima wa muqawama pamoja na wapiganaji na makamanda wake, kama walivyokuwa chini ya amri ya baba yenu shahidi, vivyo hivyo watatii amri zenu pia.
Muwe katika hifadhi ya Mwenyezi Mungu.
Akram Al-Kaabi
Maoni yako