Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Kongamano hilo lilifanyika chini ya usimamizi wa kituo cha Jaamiatul Mustafa, kwa kushirikiana na Kamati ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), huku likiwakutanisha viongozi wa dini, wanazuoni, pamoja na wadau wa amani kutoka jamii mbalimbali. Tukio hilo lilitawaliwa na hali ya heshima, majadiliano ya kielimu, na mshikamano wa kijamii.
Katika kongamano hilo, mada mbalimbali zilijadiliwa kuhusu dhana ya Mwokozi wa siku ya mwisho, ambapo wawakilishi wa dini na madhehebu tofauti walielezea mitazamo yao juu ya suala hilo. Washiriki walisisitiza kuwa; licha ya tofauti za kiitikadi na kimadhehebu, imani ya kuja kwa mwokozi ni fikra inayopatikana katika tamaduni na dini nyingi duniani, jambo linaloweza kuwa msingi wa maelewano na matumaini ya pamoja kwa wanadamu.
Kwa upande wa madhehebu ya Shia Ithnaasharia, Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC), Maulana Hemedi Jalala, alipata nafasi ya kuwasilisha kwa kina dhana ya Mahdawiya mbele ya hadhira. Katika maelezo yake, alifafanua nafasi ya imani ya mwokozi katika kujenga matumaini, kusimamia haki, na kuimarisha uwajibikaji wa kijamii kwa waumini.
Kongamano lilihitimishwa kwa dua ya pamoja, huku washiriki wakimuomba Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwa mwokozi wa ulimwengu ambae Kwa mujibu wa imani ya madhehebu ya Ahlulbayt (as), mwokozi huyo ni Imam Mahdi (ajtf), anayetarajiwa kuja kuujaza ulimwengu uadilifu na amani baada ya kujaa dhuluma.
Tukio hilo limeonekana kuwa hatua muhimu katika kuimarisha mazungumzo ya kidini na kuonesha mchango wa taasisi za kielimu na kijamii katika kujenga utamaduni wa amani na uelewano ndani ya jamii.






Maoni yako