Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, kongamano hili lililofanyika katika mazingira ya kiroho na yaliyojaa hamasa, liliwakutanisha kwa wingi wanazuoni, wanafikra na wananchi wa matabaka mbalimbali kutoka madhehebu tofauti. Lengo kuu la hafla hii lilikuwa kufafanua ujumbe wa milele wa harakati ya Imam Hussein (a.s.) na kusisitiza uaminifu kwa misingi ya kutafuta haki ya Imam Hussein (a.s.). Tukio hili lilipokelewa kwa shangwe na mwitikio mkubwa kutoka kwa washiriki.
Dkt. Saeed Talibinia, Mkurugenzi Mkuu wa Nyumba ya Utamaduni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Karachi, alishiriki kikamilifu katika hafla hii na kupongeza kuandaliwa kwa kongamano hilo. Katika mkutano huu, wanaume na wanawake, wanafunzi wa vyuo, wanafunzi wa vyuo vya dini (talaba) na watoto walihudhuria kwa idadi kubwa. Washiriki kwa kusaini hati maalumu, walihuisha ahadi yao ya uaminifu kwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Aidha, kwa ajili ya watoto, ziliandaliwa programu mbalimbali kama uchoraji, michezo ya mafumbo (puzzle) na shughuli za kielimu na burudani, ambazo zilipokelewa kwa hamasa kubwa.
Dkt. Meraj-ul-Huda Siddiqi, msomi wa Kisunni, katika hotuba yake alisema: Leo pia, msafara wa Husseini umesimama mbele ya batili; jana Imam Hussein (a.s.) alikuwa akiongoza, na leo mwana wa Ali (a.s.), Imam Khamenei, ndiye mbeba bendera wa mapambano dhidi ya tawaghuti duniani.
Akaongeza kwa kusema: Wakati sauti ya Trump inapopiga kelele, dunia hunyamaza; lakini pale sauti ya Imam Khamenei inapoinuliwa, huwaamsha watu huru wa dunia na kuvuruga mipango ya batili. Kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yatafikia ushindi wa haki katika pembe zote za dunia.
Ukimya wa nchi za Magharibi mbele ya mauaji ya kimbari Ghaza
Dkt. Meraj-ul-Huda Siddiqi aliendelea kwa kukosoa vikali ukimya wa nchi za Magharibi mbele ya mauaji ya kimbari huko Ghaza, akisema: Nchi hizo hizo, mbele ya ghasia, uchomaji wa misikiti na maeneo ya umma, pamoja na kuuawa kwa raia na majeshi ya usalama nchini Iran, huwaunga mkono wachochezi wa machafuko.
Pia alikumbushia kuwa kwa ishara moja tu ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, mamilioni ya vijana nchini Iran na Pakistan wako tayari kujitoa muhanga.
Harakati ya upinzani ya Imam Hussein (a.s.) bado iko hai na inaendelea
Hujjatul-Islam Sayyid Nazir Abbas Taqavi, mjumbe mwandamizi wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia la Pakistan, katika hotuba yake alisema: Harakati ya upinzani ya Imam Hussein (a.s.) bado iko hai na inaendelea, na njia hii itaendelea hadi kudhihiri kwa Imam Mahdi (a.j.). Leo hii, upinzani huu wa Husseini–Mahdawia unaendelea chini ya uongozi wa Ayatullah Mkuu Sayyid Ali Khamenei. Na lau kama mashahidi wangeweza kusimamisha upinzani, basi harakati ya Karbala ingekomea hapo; lakini upinzani wa Karbala bado uko hai na unaendelea kumshinda adui.
Akaendelea kwa kuvitaka vyombo vya habari vya Pakistan kujiepusha na kuathiriwa na propaganda za adui, akisema: Vyombo vya habari vinapaswa, badala ya kuandamana na propaganda dhidi ya Kiongozi wa Mapinduzi, viwe wasambazaji wa fikra na shule ya mawazo ya Imam Khamenei.
Msomi huyu wa Kipakistani, akiashiria ujasiri wa Kiongozi wa Mapinduzi, alisema: Wakati Wazayuni walipokuwa wamejificha katika maficho, Ayatullah Mkuu Sayyid Ali Khamenei alikuwa uwanjani na aliswali Swala ya Ijumaa kwa ushiriki wa mamilioni ya watu.
Leo tunapaswa kukusanyika chini ya bendera ya uongozi wa Imam Khamenei
Bi Fatima Sabzawari, mwalimu wa Kipakistani, katika hotuba yake alisema: Kwa ajili ya kutimiza haki na uadilifu, ni lazima tufanye juhudi katika njia ya kudhihiri kwa Imam wa Zama (a.j.). Baada ya kuitambua haki, ni lazima pia tupige hatua katika njia ya haki. Na ikiwa sisi ni waaminifu kwenye ahadi yetu kwa Imam Hussein (a.s.), basi leo tunapaswa kukusanyika chini ya bendera ya uongozi wa Imam Khamenei. Aliongeza kuwa, Iran na Pakistan zote ziko katika shabaha ya adui, na ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kuzitetea nchi hizi mbili.
Msafara unaoelekea kwa Mwenyezi Mungu chini ya uongozi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi
Hujjatul-Islam Aqil Musa, mwanazuoni wa Kipakistani, alisema: Kwa mtazamo wa Qur’ani, msafara unaoingia uwanjani kwa ajili ya Mwenyezi Mungu pekee, leo unaongozwa na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi. Kutofuatana na msafara huu hakutuletei chochote isipokuwa khasara. Na kufufuliwa dini katika zama za sasa ni matokeo ya harakati ya upinzani ya Imam Hussein (a.s.).
Upendo wetu kwa Ayatullah Sayyid Ali Khamenei unapita mipaka ya nchi
Profesa Munawar Abbas naye alisema: Kumpenda Imam Hussein (a.s.) kunahitaji kusimama dhidi ya dhulma. Njia hii ilianza Karbala na itaendelea hadi kudhihiri kwa Imam wa Zama (a.j.). Nasi wananchi wa Pakistan tunaihuisha ahadi yetu kwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi na tunawatangazia maadui kwamba upendo wetu kwa Naibu wa Imam wa Zama (a.j.), Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, unapita mipaka ya kijiografia.
Maoni yako