Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, taasisi moja mashuhuri ya Uingereza katika takwimu zake za hivi karibuni imeripoti kuwa Waislamu wa Uingereza ndio wachangiaji na wafadhili wakarimu zaidi nchini humo. Ingawa sehemu kubwa ya misaada ya kheri ya Waislamu hutolewa kwa lengo la misaada ya kibinadamu ya kimataifa, ripoti hii pia inabainisha kuwepo kwa uwezo mkubwa ambao bado haujatumiwa ndani ya Uingereza, unaoweza kuihuisha na kuiendesha miradi mingi iliyokwama nchini humo.
Ukarimu huu wa Waislamu una mizizi yake katika mafundisho ya Kiislamu, hususan Zaka na Sadaka. Zaka huchangia hadi asilimia 40 ya jumla ya fedha zinazokusanywa na taasisi za misaada za Kiislamu zilizofanyiwa utafiti, huku asilimia 60 iliyobaki ikitokana na aina nyingine za utoaji wa mali.
Misaada mingi imejikita katika misaada ya kimataifa, jambo linaloonyesha hisia ya mshikamano wa kimataifa miongoni mwa Waislamu. Hata hivyo, ripoti hii inaonesha pia mabadiliko ya kizazi na kitamaduni kuelekea kuimarika kwa utamaduni wa kusaidiana ndani ya jamii za Waislamu wa Uingereza.
Waislamu vijana wa Uingereza, hususan wa vizazi vya tatu na vya nne, wanaendelea kuunga mkono kwa nguvu zaidi juhudi za kutatua matatizo kama ukosefu wa makazi, uhaba wa chakula na umasikini wa watoto. Ripoti inabainisha kuwa vijana wasomi na wenye uwezo wanaitikia kwa haraka migogoro iliyo wazi ndani ya jamii zao, na jambo hili linachukuliwa kuwa ni hatua chanya na ya kupongezwa.
Chanzo: 5 PILLARS
Maoni yako