Ijumaa 2 Januari 2026 - 01:00
Vijana waibadilishe mitandao ya kijamii liwe jukwaa la elimu na mazungumzo yenye kujenga

Hawza/ Dkt. Muhammad Tahir-ul-Qadri, katika hotuba yake huku akisisitiza nafasi kubwa na yenye athari ya mitandao ya kijamii, amewataka vijana kwa kuzingatia maadili na kuwajibika, kuibadili nafasi hii iwe uwanja wa elimu, amani na mazungumzo yenye kujenga, na kujiepusha na uchochezi wa chuki na uenezaji wa uvumi.

Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha  tarjama cha  Shirika la Habari la Hawza, Dkt. Muhammad Tahir-ul-Qadri, Rais wa Harakati ya Minha'j-ul-Qur’an, katika hotuba yake alifafanua umuhimu unaozidi kuongezeka wa mitandao ya kijamii na mahitaji yake ya kimaadili, akisema: Mitandao ya kijamii ni chombo chenye nguvu sana cha kueneza fikra, ambacho kinaweza kutumiwa katika njia ya kheri au katika njia ya shari; kwa hiyo, matumizi yake yanapaswa kujengwa juu ya misingi ya maadili ya juu, uaminifu na hisia ya uwajibikaji.

Aliendelea kusema kuwa, katika zama za sasa mitandao ya kijamii imekuwa miongoni mwa zana zenye ushawishi mkubwa zaidi katika kuunda fikra za umma, elimu, wito wa kidini na marekebisho ya jamii. Aliongeza kusema: Endapo nafasi hii itatumiwa kwa njia chanya na yenye kujenga, inaweza kuchukua jukumu muhimu katika kusambaza elimu, uelewa na amani; lakini matumizi yasiyo na uwajibikaji na yasiyo ya kimaadili yatachochea jamii kupotea, chuki, mifarakano na kukosekana utulivu.

Dkt. Tahir-ul-Qadri alisisitiza pia juu ya umuhimu wa umakini na uwajibikaji katika kusambaza maudhui, akasema: Watumiaji wa mitandao ya kijamii wanapaswa kabla ya kusambaza upya habari au taarifa yoyote, kuhakikisha ukweli wake; kwa sababu uvumi, taarifa zisizo sahihi na propaganda hasi si tu zinawaumiza watu binafsi, bali pia huathiri jamii nzima. Na Uislamu unatuhimiza kusema ukweli, kuwa waaminifu na kulinda heshima na hadhi ya wengine, na mafundisho haya yanatumika kikamilifu pia katika anga ya mtandaoni.

Akiwahutubia vijana, alisema: Wakati umefika wa kubadilisha mitandao ya kijamii kutoka kuwa chombo cha kupotezea muda, kubomoa haiba za watu na mijadala isiyo na manufaa, na kuifanya iwe jukwaa la elimu, utafiti, kujijenga kimaadili na mazungumzo chanya. Kuimarisha na kueneza maadili ya kidijitali ni miongoni mwa mahitaji muhimu zaidi ya nyakati hizi.

Msomi huyu wa Kisunni alihitimisha kwa kusisitiza: Kueneza adabu, subira na kuheshimiana katika mitandao ya kijamii ni msingi wa kuijenga jamii iliyoendelea na yenye amani. Kueleza tofauti za maoni kwa njia inayofaa na kujiepusha na lugha ya chuki na matusi ni wajibu wa kimaadili unaomkabili kila mtumiaji wa mitandao ya kijamii.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha