Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, kufuatia kauli za matusi na zinazowafurahisha maadui, zilizotolewa dhidi ya Ahlul-Bayt wa Isma na Tohara (a.s.), na hasa dhidi ya uwepo mtukufu na wenye nuru wa Bibi Fatima Zahra (s.a.), Jumuiya ya Wanazuoni wa Chuo cha Elimu ya Dini cha Qom imetoa tamko na kutoa onyo kali dhidi ya aina hii ya kauli.
Matini ya tamko la Jumuiya ya Wanazuoni ni kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Kitabu Chake Kitukufu:
“Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya Mtume, na kukusafisheni baarabara.”
(Al-Ahzab: 33)
Kauli batili na zisizo za kielimu za mtu mmoja asiye na uelewa na mwenye uwezo mdogo kuhusu historia ya Ahlul-Bayt (a.s.), ambazo hivi karibuni zimezua mijadala na misukosuko katika vyombo vya habari, ni mfano wa wazi wa kuvuruga fikra za jamii kwa kauli za msemaji huyo.
Ingawa kukabiliana kielimu na kubainisha makosa na upotofu wa mtu huyo na mitazamo kama hiyo ni jukumu la msingi la wanazuoni na mafaqihi, hata hivyo ulazima wa kuwawajibisha watu wa aina hii kupitia taasisi zinazohusika ni jambo lisiloepukika.
Utaalamu wa kutosha katika kuitambua dini na mbinu zake, pia kuelewa kikamilifu maudhui ya dini na mafundisho yake, pamoja na kutumia metodolojia na njia sahihi za utafiti wa dini, ni hitaji la msingi kwa yeyote anayetaka kuingia kitaalamu katika kubainisha ukweli. Kwa msingi huo, kuingilia mijadala ya kihistoria na watu wasiokuwa na ujuzi na utaalamu ni dhulma na usaliti mkubwa dhidi ya taaluma na fikra, na ni kuchafua sura ya haki na ukweli.
Suala la kudhulumiwa kwa uwepo mtukufu na wenye nuru wa Bibi Zahra (s.a.) limeelezwa wazi katika vyanzo vya Kiislamu, na haiwezekani kupuuzwa kwa urahisi kwa kukanusha simulizi moja tu ya kihistoria huku kukiwa na idadi kubwa ya riwaya na nyaraka za kihistoria.
Jumuiya ya Wanazuoni wa Chuo cha Elimu ya Dini cha Qom, katika muktadha wa kulinda mafundisho ya kweli ya Kishia na uwepo wenye nuru wa Watu Watukufu (a.s.), hususan kipande cha Mtume (s.a.w.), Bibi Siddiqah Tahira (s.a.), inalaani vikali kauli za kuvunja misingi na mipaka zilizotolewa na mtu huyu mwenye nia ovu, na inatangaza yafuatayo:
“Mtu huyu anapaswa kuomba radhi kwa kauli zake za matusi, na bila ya visingizio wala maneno ya kupamba, akiri waziwazi kosa na upotovu wa kauli zake, ili watu wengine wasiweze kuingia katika uwanja huu na kufanya itikadi za vijana wa nchi hii kuwa chombo cha njama za mikondo kama vile Uwahabi.”
Kwa kuwa jukumu la kulinda na kuhifadhi dini liko mikononi mwa wanazuoni wa Uislamu – ‘kwa sababu Waumini wanazuoni ni ngome za Uislamu’ – ni lazima kupambana kwa uthabiti dhidi ya uenezwaji wa shubuha na fikra potovu, na katika mabaraza ya kielimu, kuandaliwa mazingira ya kukuza nyanja mbalimbali za elimu, maarifa na kufichua mambo yaliyokuwa hayajulikani.
Jumuiya ya Wanazuoni wa Chuo cha Elimu ya Dini cha Qom Iran.
Maoni yako