Jumatatu 8 Desemba 2025 - 11:09
Mapinduzi kabla ya kudhihiri Imam Mahdi (a.s.)

Hawza/ Baadhi ya watu, wakitegemea baadhi ya riwaya, wamefikia hatua ya kudhania kwamba aina yoyote ya harakati dhidi ya watawala madhalimu kabla ya kudhihiri kwa Imam wa Zama (a.s.) ni haramu; kwa sababu hiyo, wanapinga kila wito wa kuitaka haki na wanauita kuwa ni wa kitwaghuut.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, mkusanyiko wa tafiti za Mahdawiyya ukiwa na anuani isemayi “Kuielekea jamii bora”, umetolewa kwa lengo la kusambaza mafundisho na maarifa yanayohusiana na Imam wa Zama, Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake kutukufu, na kuwasilishwa kwenu ninyi wasomi waheshimiwa.

Mojawapo ya mada ambazo daima zimekuwa zikijadiliwa na kubishaniwa katika tafiti za Mahdawiyya, ni hukumu ya mapinduzi na serikali za wakati wa ghaiba na kabla ya mapinduzi ya ulimwengu ya Imam Mahdi, Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake kutukufu. Baadhi ya watu, wakitegemea baadhi ya riwaya, wanadhania kwamba aina yoyote ya harakati dhidi ya watawala madhalimu kabla ya kudhihiri kwa Imam wa Zama (a.s.) ni haramu; na kwa hivyo, wanapinga kila wito wa haki na wanauita kuwa ni wa kitwaghuut

Hapa tutafanya uchambuzi mfupi wa riwaya zinazohusiana na mapinduzi ya kabla ya kudhihiri.

Utwaghuti wa wabeba bendera wa mapinduzi kabla ya kudhihiri

Baadhi ya riwaya hizi, kwa ujumla, zinahukumu kila aina ya uasi na kuinuliwa kwa bendera yoyote kabla ya mapinduzi ya Hujjat (Imam Mahdi), Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake kutukufu, na humtambulisha mbeba bendera wake kuwa ni ṭāghūt au mushiriki, tunataja riwaya mbili tu katika utafiti huu:

Imam Ja‘far Sadiq (a.s.) amesema:

«كُلُّ رَايةٍ تُرْفَعُ قَبْلَ قِيامِ القائِمِ فَصاحِبُها طاغُوتٌ يُعْبَدُ مِنْ دُونِ اللّهِ عَزَّوَجَلَّ.»

Kila bendera itakayoinuliwa kabla ya kusimama kwa Qā’im, basi mwenye kuibeba ni twaghuut anayabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
(Al-Kāfī, Juz. 8, uk. 295)

Imam Muhammad al-Baqir (a.s.) amesema:

«كُلُّ رَايةٍ تُرْفَعُ قَبْلَ رَايَةِ القائِمِ صاحِبُها طاغُوتٌ.»

Kila bendera itakayoinuliwa kabla ya bendera ya Qā’im, mwenye kuibeba ni twaghuut.
(An-Nu‘mānī, Al-Ghayba, uk. 114)

Mbali na kasoro za kiusimulizi (isnād) zinazopatikana katika riwaya hizi, mmoja wa watafiti katika kuchambua maana ya riwaya hii anaandika:
Wito upo katika aina mbili:

1. Wito wa haki; yaani kuwaita watu kusimamisha haki na kurejesha hatamu za uongozi mikononi mwa Ahlul-Bayt (a.s.), wito kama huu umethibitishwa na kuungwa mkono na Maimamu Maasumu (a.s.).
2. Wito wa batili; yaani kuwaita watu ili kujitangaza na kujikuza mwenyewe. Na makusudio ya kauli “kila bendera” ni sehemu hii ya pili; yaani wito unaokuwa sambamba na unaopingana na wito wa Ahlul-Bayt (a.s.), si ule ulio katika mwelekeo na mkondo wao. Kwa hiyo, mapinduzi ambayo yamefanyika kwa msingi wa kulinda heshima ya Ahlul-Bayt (a.s.) na kuwaita watu kuelekea kwao, kwa ujumla yako nje ya wigo wa mifano inayolengwa na riwaya hii.

Huenda ikasemwa: riwaya hii inaonyesha ubatilifu wa mapinduzi yeyote kabla ya kusimama kwa Qā’im, Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake kutukufu; yaani kigezo cha ubatilifu si kwamba wito uwe wenye manufaa binafsi na uwe sambamba, si katika mkondo wa, harakati za Maimamu Maasumina (a.s.); bali kigezo ni kutangulia mapinduzi hayo kabla ya mapinduzi ya Imam Mahdi, Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake kutukufu; iwe ni wito wa haki au wito wa batili!

Kwanza: kuna uwezekano mkubwa, riwaya hizi zinahusiana na baadhi ya mapinduzi ya wakati huo pekee, na kwa istilahi ni “qadhiya ya nje” (qadhiya kharijiya), si ya jumla (haqiqiya), na hazihusiani na mapinduzi yote; na kigezo cha haki na batili kinabaki kuwa ni wito wa kuielekea njia iliyo sawa.

Pili: kuna riwaya nyingi kutoka kwa Maimamu Maasumu (a.s.) ambazo zimeunga mkono kikamilifu baadhi ya mapinduzi yatakayotokea baadaye na kabla ya kudhihiri kwa Imam wa Zama, na zimewahimiza watu kujiunga nayo; kama vile bendera ya Yamani.
(Najmuddin Tabasi, Mpaka kudhihiri, Juz. 1, uk. 78)

Imam Khomeini (r.a.), akiwajibu wale wanaojitafutia visingizio kwa kutegemea riwaya zilizotajwa, anasema:

“Riwaya hizi hazihusiani kabisa na kuundwa kwa serikali ya Mwenyezi Mungu iliyo ya haki—ambayo kila mwenye akili huiona kuwa ni lazima. Bali katika riwaya ya kwanza kuna uwezekano wa aina mbili: aina ya kwanza ni kwamba; inahusiana na habari za kudhihiri kwa Walii wa Zama (a.s.) na alama za kudhihiri, na inataka kusema kuwa bendera zinazoinuliwa kwa madai ya uimamu kabla ya kusimama kwa Qā’im ni batili; na aina ya pili ni kuwa; ni aina ya utabiri kuhusu serikali hizi zitakazoanzishwa duniani hadi wakati wa kudhihiri, ambazo hakuna hata moja itakayotekeleza wajibu wake ipasavyo; na hivyo ndivyo ilivyokuwa hadi sasa...”
(Kashf al-Asrār, uk. 225)

Pia anasema mahali pengine:


“Riwaya hizo zinawahusu wale watakaoinua bendera wakidai Mahdawiyya sambamba na bendera ya Mahdi; kwamba hiyo ni batili.”
(Sahifa-ye Imam, Juz. 21, uk. 14)

Kushindwa kwa mapinduzi kabla ya kudhihiri

Kuna riwaya zinazoeleza kutofanikiwa na kushindwa kwa mapinduzi kabla ya mapinduzi ya Imam Mahdi (a.s.). Kundi hili la riwaya linaashiria kutokuwa halali kwa jitihada za kuanzisha serikali ya Kiislamu, kwa sababu mapinduzi yasiyozaa matunda, kwa mtazamo wa akili na wenye akili, hayapendezi.

Baadhi ya riwaya zinazotajwa katika muktadha huu ni kama ifuatavyo: Imam Zaynul-‘Abidin (a.s.) amesema:

«وَاللَّهِ لَا يَخْرُجُ وَاحِدٌ مِنَّا قَبْلَ خُرُوجِ القَائِمِ عليه‌السلام إِلَّا كَانَ مَثَلُهُ مَثَلَ فَرْخٍ طَارَ مِنْ وَكْرِهِ قَبْلَ أَنْ يَسْتَوِيَ جَنَاحَاهُ فَأَخَذَهُ الصِّبْيَانُ فَعَبَثُوا بِهِ.»

Naapa kwa Mwenyezi Mungu! Hakuna yeyote kati yetu atakayetoka (kuinuka) kabla ya kutoka kwa Qā’im, isipokuwa mfano wake ni kama kifaranga kilichoruka kutoka kwenye kiota chake kabla mabawa zake hazijakamilika; ndipo watoto wakakikamata na wakaanza kucheza nacho.
(Al-Kāfī, Juz. 8, uk. 264)

Kutokana na riwaya hii, wamehitimisha kwamba: kusimama kwa lengo la kuunda serikali ya Kiislamu si tu kuwa hakutazaa matunda, bali pia kutaleta dhiki na mateso kwa Ahlul-Bayt. Kwa hivyo, inafaa kuacha wazo la kuanzisha serikali ya Kiislamu kabla ya mapinduzi ya Imam Mahdi, Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake kutukufu!

Mbali na matatizo ya isnād, kutegemea riwaya hii na zinazofanana nayo kuna batili kwa sababu kadhaa:

Hoja ya kwanza: Riwaya hii hailengi kukataa uhalali wa kusimama, bali inakanusha ushindi. Kama tutasema kwamba riwaya hii inakanusha uhalali, basi mapinduzi ya Imam Husayn (a.s.) dhidi ya Yazid, na pia mapinduzi ya Zayd bin ‘Ali, na Husayn bin ‘Ali (Shahidi wa Fakh), na mengineyo, yangehukumiwa kuwa si sahihi! Hali ya kuwa bila shaka mapinduzi haya yaliungwa mkono na Maimamu (a.s.). Imam Ja‘far Sadiq (a.s.) alisema kuhusu mapinduzi ya Zayd Shahidi:

«وَ لَا تَقُولُوا خَرَجَ زَيْدٌ فَإِنَّ زَيْداً كَانَ عَالِماً وَكَانَ صَدُوقاً وَلَمْ يَدْعُكُمْ إِلَى نَفْسِهِ إِنَّمَا دَعَاكُمْ إِلَى الرِّضَا مِنْ آلِ مُحَمَّدٍ عليهم السلام وَ لَوْ ظَهَرَ لَوَفَى بِمَا دَعَاكُمْ إِلَيْهِ إِنَّمَا خَرَجَ إِلَى سُلْطَانٍ مُجْتَمِعٍ لِيَنْقُضَه.»

Msimseme Zayd kwa kumlaumu; kwani Zayd alikuwa mtu mwenye elimu na mkweli, wala hakuwaita watu kuelekea kwake yeye mwenyewe; bali aliwaita kuelekea kwenye radhi ya Ahlul-Muhammad (a.s.). Na lau angeshinda, angebakia kuwa mwaminifu kwa yale aliyowaahidi. Alisimama dhidi ya utawala uliokuwa imara na uliojaa nguvu, ili kuubomoa.
(Al-Kāfī, Juz. 8, uk. 264)

Hoja ya pili: Kutofanikiwa kwa mapinduzi si dalili ya kuondoa wajibu wa kusimama. Kwa mfano, katika vita vya Siffin ilienea habari kuwa Mu‘awiya amekufa. Watu wakafurahi, lakini Imam Ali (a.s.) akasema mbele ya furaha hiyo: Naapa kwa Mwenyezi Mungu ambaye roho yangu imo mikononi Mwake, Mu‘awiya hatakufa mpaka watu waungane naye. Akaulizwa: basi kwa nini unapigana naye? Imam akasema:

«اَلْتَمِسُ العُذْرَ بَيْنِي وَ بَيْنَ اللَّهِ.»

Ninatafuta udhuru baina yangu na Mwenyezi Mungu.
(Ibn Shahr Ashub, Al-Manāqib, Juz. 2, uk. 259)

Riwaya hii na zinazofanana nayo zinaonesha kuwa Mwislamu anapaswa kutekeleza wajibu wake, wala hapaswi kusubiri lazima apate matokeo anayoyataka.

Hoja ya tatu: Katika baadhi ya riwaya, zimetolewa bishara kuhusu mapinduzi kabla ya kusimama kwa Qā’im ambayo yatakuwa ni maandalizi ya serikali ya Imam Mahdi (a.s.). Bila shaka maandalizi hayo yanatokana na mafanikio ya mapinduzi hayo. Aidha, kuandaa mazingira chanya yenyewe ni tunda kubwa zaidi. Miongoni mwa mapinduzi mashuhuri zaidi ni kutoka kwa Yamani, ambaye katika riwaya nyingi, bendera yake imetajwa kuwa ndiyo bendera iliyoongoka zaidi.

Hoja ya nne: Ikiwa riwaya hizi zingelenga kukataza kusimama na kupambana na dhulma na ufisadi, basi zingepingana na aya za jihadi, kuamrisha mema na kukataza maovu, na pia mwenendo wa viongozi Maasumina (a.s.).

Kimya na kujitenga

Baadhi ya riwaya zinawahimiza watu wakae kimya na watulie, na zinawakataza kushiriki katika mapinduzi na mapambano yoyote kabla ya kutimia alama za kudhihiri. Kwa mfano, Imam Ja‘far Sadiq (a.s.) anamwambia Sudayr:

«يَا سَديرُ الْزَمْ بَيْتَكَ وَكُنْ حِلْساً مِنْ أَحْلَاسِهِ وَاسْكُنْ مَا سَكَنَ اللَّيْلُ وَالنَّهَارُ، فَإِذَا بَلَغَكَ أَنَّ السُّفْيَانِيَّ قَدْ خَرَجَ فَارْحَلْ إِلَيْنَا وَلَوْ عَلَى رِجْلِكَ.»

Ewe Sudayr! Kaa nyumbani na ushikamane na maisha yako, tulia maadamu usiku na mchana vimetulia; lakini itakapokufikia habari kuwa Sufyani ametoka, basi njoo kwetu hata kama utakuja kwa miguu.
(Al-Kāfī, Juz. 8, uk. 264)

Kwa mujibu wa baadhi ya watu, maana ya riwaya hii haiwazuii Sudayr pekee, bali inawajumuisha watu wote; yaani wote wanapaswa kunyamaza na kujiepusha na mapinduzi hadi kutoka kwa Sufyani na alama nyingine.

Katika kujibu mtazamo huu inapaswa kusemwa: kueneza hukumu kwa watu wote na katika nyakati zote kunategemea kuthibitisha kuwa mtu fulani au mazingira maalumu hayakuwa ndiyo yalilengwa na Imam.

Kwa hiyo, hata tukikubali usahihi wa isnād za baadhi ya hadithi, hakuna hata moja kati yake inayoweza kupinga uhalali wa mapinduzi na serikali katika zama za ghaiba; bali riwaya za aina hii zinahukumu kuwa batili mapinduzi ambayo hayana masharti muhimu, au yanayofanywa kwa malengo maovu na kwa matamanio binafsi.

Hivyo, ikiwa mapinduzi yatafanyika kwa masharti yaliyobainishwa katika Sheria, chini ya usimamizi wa mtawala mwadilifu (faqihi), na malengo yake yakajengwa juu ya misingi ya Sheria, basi yatakuwa ni maandalizi ya mapinduzi ya Imam Mahdi, Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake kutukufu; na si tu kwamba hayatakatazwa, bali katika baadhi ya nyakati, jitihada za kuyasimamisha zitakuwa ni wajibu.

Utafiti huu unaendelea...

Imenukuliwa kutoka katika kitabu “Darsnāma-ye Mahdaviyya”, kilichoandikwa na Khodamorad Soleimiyan, huku ikifanyiwa babadiliko kiasi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha