Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya Tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia Pakistan, katika ujumbe wake kutokana na mnasaba wa tarehe 2 Disemba, Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Utumwa, alisisitiza kuwa; ingawa binadamu ameumbwa akiwa huru, lakini katika historia yote daima amekuwa akifungwa katika maumbo mapya na mbinu mpya za kiutumwa, na hivi leo utumwa huo umechukua sura ngumu zaidi na nzito zaidi.
Katika ujumbe huo amesema kuwa: Leo ubinadamu unakabiliwa na aina ngumu zaidi ya utumwa kuliko wakati wowote uliopita. Iwapo hapo zamani watu walitekwa na kufanywa watumwa mmoja mmoja, leo katika zama mpya mataifa na serikali zimenasa katika utumwa wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni wa madola ya kibeberu; na aina hii ya utumwa ni hatari zaidi na pana zaidi kuliko ilivyokuwa hapo zamani.
Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia Pakistan, akirejelea utawala wa mifumo ya kisasa ya kiuchumi amesema: Mfumo wa ubepari wa kimataifa (capitalism) pamoja na kauli mbiu zake za hadaa na zinazovutia kwa nje, umewafunga wanadamu wa leo katika minyororo ambayo kujinasua kwayo imekuwa vigumu sana. Mfumo huu haujamtawala tu mtu binafsi, bali umeidhibiti pia jamii, utamaduni, uchumi na siasa za mataifa, na kuyanyang’anya uhuru wao.
Katika kuendeleza ujumbe wake, kwa kutaja vipengele mbalimbali vya utumwa huu, amesema: Binadamu wa leo amenasa katika minyororo mingi, ikiwa ni pamoja na:
1. Utumwa wa kiuchumi: Unaolazimishwa na taasisi za fedha za kimataifa, ambapo mataifa mengi yamenaswa katika mtego wa madeni, masharti dhalimu ya kifedha na vikwazo vya kiuchumi.
2. Utumwa wa kiutamaduni na kistaarabu: Huu ndio utumwa hatari zaidi, kwa kuwa kupitia kupenya katika fikra na fahamu za binadamu, hulenga utambulisho wake binafsi na wa kijamii, na kwa kulazimisha thamani zisizo za kimaumbile, hunyang’anya haki ya kufikiri na kuishi kiasili.
3. Utumwa wa kisiasa: Unaotekelezwa kupitia njama, mapinduzi ya kijeshi, uvamizi, kuingilia serikali na maamuzi nyeti ya hatima ya mataifa.
Mwanazuoni huyu mashuhuri wa Pakistan ameongeza kuwa; mifano ya utumwa huu ni mingi isiyohesabika, lakini miongoni mwa mifano iliyo wazi na ya kuhuzunisha zaidi ni Palestina, hususan Ukanda wa Ghaza; mahali ambapo ukoloni na ubeberu kwa njia katili zaidi umekanyaga haki za binadamu na hawazingatii mipaka wala maadili yoyote.
Ameonya kuwa: Maadamu dunia haitajifunga kwa dhati katika usawa wa haki za binadamu, na mikataba ya kimataifa ambayo kwa masikitiko makubwa bado imebaki katika kiwango cha kauli mbiu pekee haitatekelezwa kivitendo, basi kuokoka kwa mwanadamu kutoka katika makucha ya utumwa wa kisasa hakutawezekana.
Inafaa kutajwa kuwa tarehe 2 Disemba 2025, nchini Pakistan na duniani kote huadhimishwa kama Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Utumwa.
Lengo la siku hii ni kuongeza uelewa kuhusu uhalifu mkubwa kama vile biashara ya binadamu, unyonyaji wa kingono, kazi za kulazimishwa, utumwa wa kisasa na ndoa za kulazimishwa; uhalifu ambao unatishia kwa kiwango kikubwa uhuru na heshima ya binadamu.
Maoni yako