Jumanne 2 Desemba 2025 - 06:00
Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu Yafanyika Nchini Pakistan

Hawza/ Mashindano ya kimataifa ya usomaji mzuri wa Qur’ani Tukufu yamefanyika mjini Islamabad, Pakistan, kwa ushiriki wa wawakilishi kutoka nchi 37 za Kiislamu duniani.

Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya Tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Wizara ya Mambo ya Kidini na Uendelezaji wa Maelewano ya Madhehebu ya Pakistan, kwa mara ya kwanza, iliandaa kwa fahari kubwa mashindano ya kimataifa ya usomaji mzuri wa Qur’ani Tukufu mjini Islamabad. Tukio hili la kiroho, lililojaa mazingira ya kisomo, unyenyekevu na kushikamana na Qur’ani, lilipata mvuto wa pekee kwa kushuhudiwa na wasomaji mashuhuri wa Qur’ani na wawakilishi kutoka nchi 37 za Kiislamu.

Katika hafla hiyo, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Arif Hussein Wahidi, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Maulamaa wa Kishia wa Pakistan, alishiriki katika sherehe za ufunguzi na pia katika hatua ya mwisho ya mashindano. Kando ya tukio hili, alikutana na kufanya mazungumzo na Sardar Muhammad Yusuf, Waziri wa Shirikisho wa Mambo ya Kidini; Sardar Ayaz Sadiq, Spika wa Bunge la Taifa la Pakistan; Reza Amiri-Moqaddam, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; pamoja na idadi ya watu mashuhuri wa kidini na kisiasa.

Nafasi ya Qur’ani katika Umoja wa Umma wa Kiislamu

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Arif Hussein Wahidi, katika hotuba yake, aliielezea Qur’ani Tukufu kuwa ni “sheria ya uja,” “hati ya uhai,” na “mpango mkamilifu zaidi wa maisha ya mwanadamu,” na akataja kufanyika kwa mashindano haya ya kimataifa kuwa ni hatua kubwa na ya kihistoria katika kueneza utamaduni wenye nuru wa Qur’ani.

Aliongeza kuwa: tukio hili, ambalo ni uzoefu wa kwanza wa Pakistan katika ngazi ya dunia katika uwanja wa usomaji wa Qur’ani, si tu fahari ya kitaifa kwa nchi hiyo, bali pia ni chachu ya kuenea kwa maarifa ya Qur’ani na kuimarika kwa utambulisho wa kidini wa jamii.

Msomi huyu mashuhuri wa Pakistan, akionesha matumaini yake juu ya baraka za kiroho za tukio hili, alisisitiza kuwa; rehema ya Mwenyezi Mungu, maendeleo endelevu, mshikamano wa kijamii na utulivu zaidi, ni miongoni mwa matunda ya kuzingatia na kuishikamana na Qur’ani Tukufu kwa Pakistan.

Ujumbe wa Umoja, Mshikamano na Udugu

Aidha, alitaja ushiriki wa wasomaji mashuhuri kutoka nchi mbalimbali kuwa ni ishara ya imani na heshima ya jamii ya kimataifa kwa Pakistan, na kusema: “Ushiriki wa nyota wa Qur’ani kutoka pande zote za dunia ni fahari kubwa kwa taifa la Pakistan, na tukio hili linapeleka ujumbe ulio wazi wa umoja, mshikamano na udugu wa Umma wa Kiislamu kwa dunia.”

Qur’ani: Msingi wa Pamoja na Kipimo cha Umoja

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Arif Wahidi, akisisitiza nafasi ya kipekee ya Qur’ani miongoni mwa Waislamu, alisema: “Qur’ani Tukufu ni mhimili wa muafaka wa Umma wa Kiislamu; ni kitabu ambacho ni chanzo cha uongofu, kinachomjenga mwanadamu, kilicho salama dhidi ya upotoshaji wowote, na kinachokubalika na madhehebu yote ya Kiislamu. Iwapo Umma wa Kiislamu utafanya kitabu hiki cha mbinguni kuwa ndio kipimo cha mienendo yake na nyaraka ya matendo yake, basi kufikiwa kwa umoja wa kweli kutakuwa jambo linalowezekana na linalofikika.”

Mazingira ya kiroho ya mashindano haya na msisitizo juu ya nafasi ya Qur’ani katika kuunganisha Umma wa Kiislamu, yameligeuza tukio hili kuwa hatua muhimu na ya kihistoria katika shughuli za Qur’ani nchini Pakistan.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha