Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Wizara ya Mambo ya Nje ya Chile kwa ushirikiano na jamii ya Wapalestina wanaoishi nchini humo, siku ya Jumatatu mjini Santiago, iliandaa sherehe maalum kwa ajili ya kuzishukuru nchi ambazo katika miaka ya karibuni zimeitambua serikali huru ya Palestina. Hatua hii imetajwa na wanadiplomasia na wanaharakati wa haki za binadamu kuwa ni alama ya uamsho wa kimataifa mbele ya dhulma ya kihistoria.
Katika hafla hiyo, serikali za Hispania, Kanada, Ireland, Ufaransa, Uingereza, Mexiko, Ureno na Australia zilitajwa kuwa ni miongoni mwa nchi ambazo kati ya miaka 2023 hadi 2025, kwa ujasiri wa kisiasa na kwa kuelewa wajibu wa kibinadamu, zilichukua hatua katika mwelekeo wa kuleta amani endelevu katika Mashariki ya Kati.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Chile, Alberto van Klaveren, katika hotuba yake alisisitiza kwamba: “Kuhudhuria sherehe hii ni kutoa heshima kwa serikali ambazo kwa mtazamo ulio wazi na kwa hisia ya uwajibikaji wa kihistoria zimetambua uwepo wa Palestina. Amani na haki hupata maana tu pale zinapojengwa juu ya msingi wa kuheshimu haki za mataifa na sheria za kimataifa.”
Aidha, akirejea historia ya Chile katika kuunga mkono haki ya watu wa Palestina, aliongeza kuwa: “Tangia suala la Palestina lilipojadiliwa katika Umoja wa Mataifa mwaka 1947, Chile imekuwa ikisisitiza daima juu ya haki ya watu wa Palestina kujitawala na kuunda taifa huru na endelevu; taifa litakaloishi kwa amani na usalama kandokando ya Israel, ndani ya mipaka inayotambulika kimataifa.”
Vera Baboun, balozi wa Palestina nchini Chile, naye alishukuru msimamo thabiti na wa kweli wa Chile katika kutetea dhima ya Palestina, na akatoa wito wa kuongezwa shinikizo la kimataifa dhidi ya utawala unaokalia ardhi kwa mabavu. Vilevile, Khalid al-Salum, balozi wa Saudi Arabia, Cyril Roux, balozi wa Ufaransa, na Jana Skaleh, mkurugenzi wa jamii ya Wapalestina wa Chile, walisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kimataifa na wakakumbushia kuwa utambuzi wa Palestina haupaswi kuwa mwisho wa safari, bali ni mwanzo wa ahadi mpya ya kusitisha uhalifu na kujenga upya matumaini ndani ya Mashariki ya Kati.
Sherehe ilihitimishwa kwa dakika moja ya ukimya kwa ajili ya kuwakumbuka waathirika wa vita vya Ghaza, na hali ya mshikamano iliyotanda ilionekana kama ishara ya azma ya dunia kusikiliza kilio cha haki.
Katika taarifa ya mwisho ya sherehe hiyo, ilielezwa kwamba: “Kila nchi inayolitambua taifa la Palestina, haifanyi tu mkataba na taifa moja, bali inaonesha ukweli na dhamiri ya kibinadamu.”
Maoni yako