Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Tarehe 25 Oktoba 2025, katika uwanja wa ndege wa Linate, maafisa wa Italia walitoa kumuelekea Muhammad Hannoun, mwenyekiti wa Jumuiya ya Wapalestina nchini Italia, amri ya kufukuzwa na kumzuia kuingia katika jiji la Milan kwa muda wa mwaka mmoja. Amri hiyo, iliyotolewa na mkuu wa polisi wa Milan, imeambatana na mashtaka ya kisheria kwa tuhuma za “uchochezi wa vurugu”, tuhuma zinazohusishwa na hotuba aliyoitoa katika mkutano wa wafuasi wa Palestina mnamo tarehe 18 Oktoba.
Hannoun alikuwa amesafiri kuelekea Milan ili kushiriki katika programu ya umma ya kuunga mkono harakati za Wapalestina, lakini mara tu aliposhuka uwanjani alikamatwa, kisha akaondoshwa na kupelekwa mji wa Genoa ambako ndiko anakokaa.
Tukio hili limezua mitazamo yenye mgongano. Baadhi ya maafisa wa serikali, akiwemo Waziri Salvini, wameipongeza hatua hiyo na kuiita “ya lazima”. Kinyume chake, wanaharakati na wachambuzi wa kisiasa kadhaa wameitaja hatua hiyo kuwa mfano wa ukandamizaji unaoongezeka kutokana na maandamano pamoja na sauti za wanaoiunga mkono Palestina na kuiona kuwa ni kosa la jinai — mwenendo unaoibuka katika mazingira ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaoendelea huki Ghaza.
Muhammad Hannoun ameitaja hatua hiyo kuwa “shambulio la kisiasa” na amewashutumu maafisa wa Italia kwa kushirikiana na utawala wa Kizayuni na uhalifu unaoendelea dhidi ya taifa la Palestina. Aidha, amelaani nafasi ya Italia katika kuusaidia kijeshi utawala wa Israel, akisema: “Silaha za Italia zinashiriki katika mauaji ya halaiki ya watu wa Ghaza.”
Tukio hili halizuii tu swali la uhuru wa kujieleza, bali linahusu pia haki — na hata wajibu — wa kufichua uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari. Kwa mujibu wa wachambuzi, amri ya kumfukuza Hannoun haikulenga maoni yake tu, bali ni jaribio la kuinyamazisha sauti inayofichua mauaji ya kimfumo yanayofanywa na utawala wa Tel Aviv dhidi ya watu wa Ghaza. Katika mazingira kama haya, kufukuzwa kwa mmoja wa wanaharakati wa kihistoria wanao iunga mkono Palestina nchini Italia kunachukuliwa kuwa ishara ya kutisha: yule anayefichua jinai anaitwa mhalifu, na anayezifanya, anapewa hadhi ya “mtetezi wa ustaarabu wa Magharibi.”
Muhammad Hannoun kwa miaka mingi amekuwa miongoni mwa sura mashuhuri zaidi katika harakati za kuiunga mkono Palestina nchini Italia. Amehusika katika kuandaa maandamano, kampeni za uhamasishaji, na programu za kitamaduni zinazounga mkono mapambano ya Wapalestina, na anajulikana kwa misimamo yake ya wazi katika kufichua sera za kibaguzi za utawala wa Israel.
Tukio la Milan limetokea katika mazingira ya ongezeko la ukandamizaji wa mikusanyiko ya wafuasi wa Palestina barani Ulaya, ambako kuonesha mshikamano na taifa la Palestina kunazimwa kwa urahisi kwa tuhuma za “uchochezi wa chuki”, huku mauaji ya kimbari yanayoendelea yakipuuziwa na taasisi rasmi na kuhalalishwa kimyakimya.
Maoni yako