Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, hafla ya uzinduzi wa kazi mbili za kielimu za Hujjatul-Islam wal-Muslimin Muhammad Hadi Muftah, kwa anuani za "Fiqhul-Hukūmah na Fiqhul-Mujtama‘ al-Urūbī", imefanyika katika ukumbi wa Kituo cha Vyombo vya Habari na kuraza za Mtandaoni cha Hawza.
Katika hafla hiyo, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Muhammad Hasan Zamani, huku akiwashukuru waandaaji wa kikao hicho, alisema: “Desturi njema ya kuzindua vitabu vya kielimu vyenye ubunifu mpya inapaswa kuenezwa hawza. Ni vizuri desturi hii ya kuonyesha kazi zenye nadharia mpya ipate mizizi imara hawza; kwa bahati mbaya, bado jambo hili halijapanuka vya kutosha. Ninashauri uongozi wa hawza kuongeza vikao vya kielimu na vya nadharia katika nyanja zote za elimu ya Kiislamu – kuanzia fiqhi na usūl, hadi falsafa, kalām, ‘irfān na elimu za kijamii.”
Misingi ya vikao vya kielimu na uhuru wa fikra
Aliongeza kusema: “Haya ni miongoni mwa maagizo muhimu ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi Iran, ambaye takribani miongo mitatu iliyopita, kwenye mkutano wake wa kihistoria na wanazuoni na wanafunzi katika Madrasa ya Faydhiyyah, alisisitiza umuhimu wa vikao vya kielimu, majadiliano ya nadharia, na majukwaa ya fikra huria hawza. Hata hivyo, hatujafanikiwa vya kutosha katika eneo hili hadi leo.
Utamaduni wa kukubali ukosoaji uwe wa kudumu
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Zamani, akirejelea pendekezo la Hujjatul-Islam wal-Muslimin Muftah kuhusu kukosolewa kwa kazi zake mbili, alisema:
“Kitendo chake cha kuhimiza ukosoaji wa kazi zake ni chenye thamani kubwa. Katika nchi yetu, waandishi wengi hukimbia kukosolewa na hupendelea sifa; tofauti na nchi nyingine, ambako waandishi hupokea ukosoaji kwa mikono miwili na hata huwazawadia wakosoaji wenye hoja madhubuti ili marekebisho ya kielimu yafanywe katika machapisho yajayo. Hivyo basi, tunapaswa kukuza utamaduni huu katika vyuo vyetu, ili kuimarisha mazungumzo ya kielimu na kukuza fikra.”
Mshauri huyo aliongeza kuwa: “Katika baadhi ya nchi za Kiislamu kama Misri, mwandishi baada ya kuchapisha kazi yake huomba mwenyewe kikao cha ukosoaji na hata hufadhili gharama za wakosoaji ili kazi yake iboreshwe kielimu. Utamaduni huu ni dalili ya ukuaji wa kielimu, na inafaa pia uanze kuota mizizi kwenye hawza zetu.”
Uislamu — dini ya kimataifa
Katika sehemu ya pili ya hotuba yake, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Zamani alisisitiza juu ya ulimwengu wa Uislamu akasema: “Uislamu ndio dini pekee ya kimataifa, na inakuwa ya kimataifa kwa pande tatu: kwanza, sheria na hukumu zake za fiqhi ni za kimataifa; pili, mustakabali wake ni wa kimataifa; na tatu, wafuasi wake wanapaswa kuifanya iwe ya kimataifa. Mwenyezi Mungu ameyaweka maamrisho ya Uislamu kwa namna inayojibu mahitaji ya jamii zote za kibinadamu katika zama zote hadi Siku ya Kiyama.”
Akiashiria Aya za Qur’ani kuhusu ahadi ya kusambaa kwa Uislamu duniani, alisema: “Qur’ani katika Aya kama ‘وَعَدَ اللَّهُ الَّذینَ آمَنُوا…’ na ‘لِیُظْهِرَهُ عَلَی الدِّینِ كُلِّهِ’. Imebainisha wazi kwamba Uislamu utakuwa dini iliyo juu ya dini zote. Kwa hiyo, sisi maulamaa tunapaswa kuwa na nafasi muhimu katika kutekeleza ahadi hii ya Mwenyezi Mungu.”
Kisa cha safari ya Ujerumani
Akaongeza kwa kisa: “Nilipokuwa safarini Ujerumani, nilialikwa kutoa hotuba katika Kituo cha Kiislamu cha Hamburg kwa ajili ya Wairani, lakini sikuwa najua Kijerumani wala Kiingereza, hivyo sikuweza kuhutubu kwa wasiokuwa Wairani. Wakati huo huo, watu kama Dkt. Muftah kwa kutumia ujuzi wao wa lugha za kigeni waliweza kuutambulisha Uislamu Magharibi. Leo tunapaswa kuwa na makumi ya watu kama hao ndani ya vyuo vyetu.”
Fiqhi yenye ubunifu na kushughulika na masuala mapya
Mshauri huyo aliongeza akimsifu Hujjatul-Islam Muftah: “Kujikita katika masuala mapya ya fiqhi, hasa yanayohusu jamii za Ulaya, ni jambo la lazima. Wengine hudhani fiqhi ya Kishia imemaliza masuala yote na kwamba tunapaswa kurudia yaliyoandikwa na waliotutangulia, lakini ukweli ni kuwa fiqhi lazima ijishughulishe na changamoto mpya za kijamii na kimataifa.”
Akapendekeza: “Ni vizuri Hujjatul-Islam Muftah aendelee na njia hii na akusanye masuala mapya yanayowahusu Mashia wanaoishi katika nchi zisizo za Kiislamu chini ya jina ‘Fiqhul-Mujtama‘ al-Urūbī’, na kuyawasilisha kwa Marja‘ na walimu wa darsa kharij ili yajadiliwe na kukamilishwa katika vikao vya kielimu.”
Uvumilivu wa kielimu na fikra za kiushahidi
Akasema: “Inawezekana baadhi ya mitazamo ya kifiqhi, kama kuhusu umri wa kubaleghe au mgongano kati ya sheria za nchi mwenyeji na hukumu za fiqhi, isiwe inakubalika kwa mafaqihi wote, lakini tunapaswa kuwa na uvumilivu wa kielimu na kuyajadili kwa hoja. Katika historia ya fiqhi, mara nyingi fatwa zilizokuwa zikihesabiwa kuwa ni shadhi, baadaye zimekuwa kauli mashuhuri. Kwa hivyo, upekee wa rai hauimaanishi ubatili wake.”
Kufafanua hekima ya hukumu na kujibu shubha za Magharibi
Hujjatul-Islam Zamani aliongeza: “Ni muhimu kufafanua hekima za hukumu za Kiislamu. Katika nchi kama Misri, wanapojibu maswali ya kisheria (istifta’), maulamaa wao hutoa pia sababu kuu ya fatwa, ili wasikilizaji na wakosoaji wafahamu msingi wa kielimj wa hukumu hiyo. Njia hii huongeza uelewa wa kijamii na kukuza elimu ya fiqhi.”
Akaendelea kusema: “Kuhusu kitabu Fiqhul-Hukūmah, japokuwa kuna kazi nyingi muhimu kuhusu utawala wa Kiislamu na wilāyat al-faqīh, bado wanafunzi na hata wasomi wengi hawajavifahamu. Moja ya changamoto ni udhaifu wa kupeleka vitabu hivi mikononi mwa wasomaji wa vyuo na vyuo vikuu. Natumaini kituo cha vyombo vya habari vya hawza vitaimarisha juhudi katika kuvitambulisha.” Hujjatul-Islam wal-Muslimin Zamani alihitimisha hotuba yake akisema:
“Uzinduzi wa vitabu vya kielimu ni fursa ya kukutanisha mitazamo, kuchochea ubunifu wa kielimu, na kuinua hadhi ya fiqhi ya Kiislamu.”
Mwisho wa taarifa.
Maoni yako