Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Mataka akiwa ameambatana na Katibu wa Sekretarieti ya Baraza la Ulamaa pamoja na Mratibu wa Ofisi ya Mufti Makao Makuu, katika safari maalum ya kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani, uwazi na uwajibikaji wa hali ya juu.
Mara baada ya kuwasili, kiongozi huyo alilakiwa kwa heshima kubwa na Sheikh wa Mkoa wa Singida, Sheikh Issa Nassor, Katibu wa BAKWATA Mkoa, Alhaj Omar Muna, pamoja na maafisa mbalimbali wa Baraza hilo. Baada ya mapokezi, Sheikh Mataka alitembelea Ofisi ya BAKWATA Mkoa wa Singida na kusaini kitabu cha wageni, akielezea furaha yake kuona maandalizi ya uchaguzi yakienda vizuri.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Singida, Alhaj Omar Muna, Katibu Mkuu wa BAKWATA Taifa, Alhaj Nuhu Jabir Mruma Ashighatiiniy Almwangawiy, anatarajiwa kuwasili ili nae kuungana na viongozi hao katika usimamizi wa mchakato huo wa kidemokrasia wa Kiislamu.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Hajjat Halima Dendego, atakuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo ya uchaguzi, itakayofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida. Uchaguzi huu unatarajiwa kuwa wa kipekee, ukiwa sehemu ya juhudi za BAKWATA Taifa kuimarisha misingi ya uongozi, uwazi na ushirikishwaji katika ngazi zote za taasisi.
Waislamu wa Singida wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hili muhimu lenye lengo la kuimarisha umoja, uadilifu na ustawi wa jamii ya Kiislamu katika mkoa huo.
Kauli mbiu ya uchaguzi: “Uongozi wa Haki, Umoja na Maendeleo ya Waislamu.”
Maoni yako