Jumatano 8 Oktoba 2025 - 10:57
Sababu zilizo chochea kufanyika Operesheni ya Mafuriko ya Aqsa “Tufan al-Aqsa” kwa kauli ya daktari wa Kipalestina

Hawza/ “Munaim” — daktari wa Kipalestina — ameandika: Sisi kabla ya tarehe 7 Oktoba tulihisi hatari; bali tuliiona kwa macho yetu wenyewe. Hatari ya kutoweka kabisa haki zetu; hatari ya kusahauliwa kwetu; hatari ya kupoteza maeneo yetu matakatifu; na muhimu zaidi, hatari ya kupoteza Msikiti wa al-Aqsa, Qibla cha kwanza cha Waislamu. Tuliiona hatari hiyo na tukaamua kupigana kwa nyama na mifupa yetu.

Kwa mujibu wa Idara ya Habari za Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, katika kumbukumbu ya mwaka wa pili wa Operesheni Tukufu ya “Tufan al-Aqsa”, licha ya mafanikio mengi ya operesheni hii — ambapo muhimu zaidi ni kufufua tena dhamira ya Palestina na kuibadilisha kuwa suala kuu la Ulimwengu wa Kiislamu, na hata dunia nzima — bado katika akili za baadhi inaweza kuwepo shaka na kujiuliza kwa nini operesheni ya tarehe 7 Oktoba ilitokea.

Watu wanyonge wa Palestina kwa takribani karne moja wamekuwa wakikabiliana na janga ovu la uvamizi, kama mradi wa Uingereza, Marekani na Magharibi. Taifa la Palestina halihitaji chochote isipokuwa ardhi na nchi yao wenyewe. Lakini dai hili rahisi na la kimsingi limefanya vizazi vyao kukumbana mara kwa mara na aina zote za dhulma, mateso, mauaji, kifungo na uhamisho.

Uhalifu wote wa Wazayuni kwa miongo kadhaa katika miaka ya hivi karibuni, kwa njama za mhimili wa uovu, ulipangwa kusahaulika kupitia mpango wa “kuweka sawa uhusiano” kati ya nchi za Kiarabu na utawala wa kivamizi wa Quds. Habari kuhusu suala la Palestina hata katika vyombo vya habari na majukwaa ya kisiasa ya Ulimwengu wa Kiislamu zilikuwa zikianza kufifia kabla ya Tufan al-Aqsa.
Lakini operesheni ya kipalestina halisi, Tufan al-Aqsa, mnamo tarehe 7 Oktoba 2023, ghafla ilisababisha mshtuko mkubwa duniani.

Operesheni hii ilikuwa ni kama kilio cha pamoja cha Wapalestina wote — kuanzia wafungwa walioko katika magereza ya kutisha ya utawala huo, hadi wakimbizi waliolazimishwa kuondolewa kwenye nyumba na mashamba yao katika Ukingo wa Magharibi na maeneo mengine ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, ambapo walilazimishwa kubomoa nyumba zao kwa mikono yao wenyewe na kuzikabidhi kwa Wazayuni.

Ingawa baada ya miaka miwili tangia Operesheni ya Tufan al-Aqsa, takwimu za kutisha za ukatili wa Wazayuni huko Ghaza zinaendelea kuripotiwa, lakini kwa mujibu wa wataalamu wa Kipalestina, ukatili wa Ghaza katika kipindi cha miaka miwili ni mfano wa uhalifu wa Wazayuni katika miongo kadhaa iliyopita, uliowekwa wazi mbele ya macho ya dunia kwenye pazia la Ghaza.

“Munaim”, mwanafunzi wa udaktari wa Kipalestina, katika ukurasa wake binafsi wa mitandao ya kijamii aliandika:
Shahidi Yahya al-Sinwar katika miaka ya 2018 na 2023 alitoa hotuba muhimu sana, akieleza sababu ya kutokea kwa Operesheni ya tarehe 7 Oktoba, na kama Wapalestina walikuwa na njia nyingine yoyote ya kujinusuru na kurejesha haki zao kando na operesheni hiyo.

Shahidi Yahya al-Sinwar mwaka 2023, kabla ya Operesheni ya 7 Oktoba, katika moja ya hotuba zake alisema:

“Katika kipindi kifupi cha miezi michache — ambacho kwa makadirio yangu hakitazidi mwaka mmoja — tutailazimisha nguvu ya uvamizi ichague moja kati ya chaguzi mbili:
Ima tutailazimisha iheshimu sheria za kimataifa, izingatie maamuzi ya kimataifa, iondoke Ukingo wa Magharibi na Bayt al-Maqdis, ivunje makoloni, iwaachie wafungwa na kuwarudisha wakimbizi;
Au tutailazimisha hiyo na jamii ya kimataifa kutekeleza masharti haya na kuanzisha nchi ya Kipalestina kwa mujibu wa mipaka ya mwaka 1967 yenye Quds kama mji mkuu.
Ama vilevile, tutauweka utawala huu wa kivamizi katika hali ya mgongano na kukabiliana na irada zote za kimataifa, kuutenga sana, na kumaliza mchakato wa kuingizwa kwake katika eneo na dunia, na vilevile kumaliza hali ya kufilisika iliyojitokeza katika ngome zote za muqawama.”

Munaim, mwanafunzi wa Kipalestina, akiashiria kuwa siku hii ni muhimu zaidi katika historia ya Palestina, aliendelea kusema:
Sisi Wapalestina katika miaka 77 ya uvamizi tumeona kila aina ya dhulma na uvamizi, na mbele yake tumesimama na kupinga kwa kutumia njia elfu moja tofauti. Katika miaka ya hivi karibuni tulilikataa pia “Mradi wa Kuwekasawa Mahusiano” — mradi uliyojengwa juu ya kuachana na imani za kidini na kudharau maeneo matakatifu ya Kiislamu na yasiyo ya Kiislamu katika ardhi ya kihistoria ya Palestina. Tulichagua maisha yenye heshima ndani ya Ukanda wa Ghaza ulioko chini ya mzingiro na vita badala ya maisha ya starehe yenye fedheha.

Viongozi wetu katika miaka ya karibuni wamekuwa wakiwahutubia watu duniani na kuwaomba wachukue hatua ili sisi Wapalestina tupate haki zetu. Lakini hakuna aliyetuona kama “wanadamu”. Mataifa ya Kiarabu, Kiislamu na Magharibi yalitusahau, na yakaikubali “Israeli” kama nchi huru na sehemu ya eneo hili.

Sisi kabla ya tarehe 7 Oktoba tulihisi hatari; bali tuliiona kwa macho yetu wenyewe. Hatari ya kutoweka kabisa kwa haki zetu; hatari ya kusahauliwa kwetu; hatari ya kupoteza maeneo yetu matakatifu; na muhimu zaidi, hatari ya kupoteza Msikiti wa al-Aqsa, Qibla cha kwanza cha Waislamu. Tuliiona hatari hiyo na tukaamua kupigana kwa nyama na mifupa yetu.

Tulipiga pigo kali katika kiwiliwili cha jeshi lenye vifaa vya hali ya juu zaidi duniani, tukavunja hadithi ya “utawala usioweza kushindwa” na tukaufichua uso dhaifu na mchafu wa Wazayuni mbele ya macho ya dunia.

Wazayuni kwa miaka mingi walijaribu kutubadilisha sisi watu wa Ghaza tuwe kama mataifa mengine yanayoishi chini ya kivuli cha ubeberu. Lakini leo hii, kila mtu anajitahidi kuwa kama watu wa Ghaza — huru na wenye heshima. Wazungu na Wamarekani, wote wanaita jina “Ghaza” na kuapa kwa maisha yetu, ilhali miaka miwili tu iliyopita, hatukuwa na uwepo wowote katika fikra za dunia.
Lakini leo, tumekuwa utajo na wimbo wa kila mpigania uhuru duniani.

Siku ya 7 Oktoba tulitimiza wajibu wetu; tulitekeleza wajibu wetu wa kisheria na kibinadamu.
Lakini ninyi enyi Waarabu na Waislamu, mmefanya nini?
Je, bado hamjahisi hatari ya Israeli?
Siwaulizi mlitufanyia nini sisi; bali nawauliza:
Mlifanya nini kwa ajili yenu wenyewe?
Mlifanya nini kwa ajili ya utukufu wenu na uhuru wenu?
Mlifanya nini kwa ajili ya kulinda utu na ubinadamu?

Mimi, kama Mpalestina, nasema:
Nilitimiza wajibu wangu tarehe 7 Oktoba. Na kama nilivyolipa gharama ya kuwa Mpalestina kwa kipindi cha miaka 77 ya uvamizi, sasa pia nalipa gharama ya kuwa mwenye heshima, mwenye ufahamu na mwenye kusimama imara.
7 Oktoba itabaki kuwa siku muhimu zaidi katika historia ya Palestina hadi pale ardhi ya nchi yangu itakapokombolewa kikamilifu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha