Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Jumuiya ya Wapalestina nchini Chile, ikijibu kauli za Evelyn Matthei, mgombea urais wa muungano “Chile Vamos”, imetoa tamko kali na kuyaita maneno yake kuwa ya kupotosha, ya kukanusha na yenye kwenda kinyume na sera ya muda mrefu ya kidiplomasia ya nchi hiyo — sera ambayo daima imeegemea kuheshimu haki za binadamu na sheria za kimataifa.
Katika tamko hilo rasmi, Jumuiya ya Wapalestina nchini Chile imesisitiza kwamba maneno ya Matthei si tu yanawafanya zaidi ya nusu milioni wa-Chile wenye asili ya Kipalestina kuwa wahanga tena, bali pia ni matusi kwa kila mtu anayeshikamana na haki na heshima ya kibinadamu. Imesema: “Kukanusha mauaji ya kimbari, wakati hata Umoja wa Mataifa umetambua jambo hilo, ni juhudi ya kupaka rangi upya jinai za kutisha.”
Jumuiya hiyo imesisitiza pia kwamba Rais wa zamani Sebastián Piñera mnamo mwaka 2011 alilitambua rasmi taifa la Palestina, na kwa zaidi ya miaka 78, sera ya mambo ya nje ya Chile imekuwa ikisimama imara juu ya kutetea sheria za kimataifa, na imevuka mipaka ya mirengo ya kisiasa.
Tamko hilo pia limekosoa vikali kauli za Matthei kuhusu uwezekano wa kuanzisha tena ununuzi wa silaha kutoka Israel, na kuutaja kama upotovu wa wazi kutoka kwenye misingi ya maadili na kisheria ambayo ndiyo imekuwa dira ya siasa za kigeni za Chile. Katika tamko hilo imeandikwa: “Juhudi za kufanya uhusiano wa kijeshi na nchi inayotuhumiwa kwa mauaji ya kimbari kuwa wa kawaida, zitaifanya Chile kuwa katika nafasi ya kujitenga na ya aibu mbele ya jujuiya ya kimataifa.”
Aidha, imesisitizwa kwamba nchi kama Uingereza, Norway, Uholanzi, Ufaransa, Kanada, Australia na Umoja wa Ulaya zimechukua hatua kubwa zaidi kuliko Chile na zimeweka vikwazo dhidi ya Israel; huku hata Italia na Uhispania zikiwa zimeunga mkono misaada ya kibinadamu kuelekea Ghaza.
Tamko hilo, likihitimisha, limesisitiza: Chile haipaswi kurudi nyuma katika dhamira yake ya kutetea uhalali na sheria za kimataifa: “Hatutanyamaza mbele ya maneno yanayopaka rangi upya ukatili, yanayopunguza ukubwa wa mauaji ya kimbari na yanayojaribu kurudisha nyuma miongo kadhaa ya dhamira ya Chile kwa sheria za kimataifa.”
Maoni yako