Kwa mujibu wa kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Mian Muhammad Shehbaz Sharif, Waziri Mkuu wa Pakistan, katika tamko lake akirejelea shambulio lililofanywa na Israel dhidi ya Qatar alisema: “Kwa niaba ya serikali na wananchi wa Pakistan, na pia mimi binafsi, nalilaani vikali tendo lisilo halali lililofanywa na Israel la kubomabomoa maeneo ya makazi ya watu mjini Doha na kuhatarisha maisha ya raia wasio na hatia.”
Akaongeza kusema: “Katika hali hii ngumu, tunatoa rambirambi na mshikamano wetu na Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, familia ya kifalme na wananchi wa Qatar.”
Waziri Mkuu wa Pakistan pia alisisitiza: “Kitendo hiki cha Israel hakina hoja yoyote na ni uvunjaji wa wazi wa uhuru na mamlaka kamili ya ardhi ya Qatar, shambulio kama hili linaweza kuhatarisha uthabiti na usalama wa kikanda na kuyaweka mashakani maslahi ya nchi zote jirani.”
Tamko hili linadhihirisha msimamo thabiti wa Pakistan wa kuiunga mkono Qatar na kulaani uvamizi wa Israel, huku likisisitiza ulazima wa umakini na mshikamano wa nchi za Kiislamu katika kulinda amani na usalama wa eneo.
Maoni yako