Jumatano 20 Agosti 2025 - 20:01
Sheikh Alhad Mussa: Viongozi wanatakiwa wawe kama Chumvi kwenye hii Dunia

Hawza/ Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh Alhad Mussa, leo hii katika mdahalo wa amani amewafananisha viongozi na chumvi kwa kusema: Viongozi wanatakiwa wawe kama chumvi katika huu ulimwengu, bali wao ndio chumvi ya hii dunia

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Alhadi Mussa Salum, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), katika mazungumzo yake amesisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa na wananchi, akisema kwamba wao ndio “chumvi ya dunia,” kwani chumvi ikishaharibika itaongezwa kitu gani ili ikolee?,” alihoji Sheikh Alhad Mussa Salum

Sheikh Alhad ametoa kauli hiyo katika mdahalo wa amani, haki, na demokrasia kuelekea uchaguzi mkuu, uliofanyika leo Agosti 20,2025, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam. 

Katika muendelezo wa mazungumzo yake Sheikh Alhad Mussa Salum alisema: Ikiwa viongozi hawatakuwa na mwenendo mwema, hakuna mtu wa kuwaongoza, na kwamba kila mmoja anapaswa kuonyesha njia sahihi katika nafasi yake ili wananchi wapate mfano mzuri wa kuuiga.

Ameongeza kuwa; ni jukumu la viongozi wote, wa dini na wa Serikali, kuhamasisha amani na kuepuka kuwa chanzo cha vurugu na migogoro, huku akisisitiza kuwa hakuna amani inayoweza kupatikana bila ya kuwepo haki, na vile vile haki haiwezi kupatikana pasi na amani, lakini amani inapaswa kupewa kipaumbele kwa kuwa bila amani, hakuna maendeleo yanayoweza kufikiwa.

Mwisho wa hotuba yake, Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania, Sheikh Alhad Mussa Salum, amesisitiza umuhimu wa viongozi kutimiza ahadi walizozitoa kwa vitendo, vile vile alieleza kuwa mdahalo huo ni nafasi ya kuonesha uzalendo, kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kufuata sheria katika uchaguzi, na kuutetea ukweli na uwazi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha