Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Greta Thunberg, mwanaharakati wa haki za binadamu, siku ya Jumanne aliishtumu Israel kwa kosa la utekaji nyara, akidai kuwa Israel ilimteka yeye na wenzake katika maji ya kimataifa.
Aidha, alieleza kuwa alikataa kutia saini waraka waliomlazimisha kuutia saini, ambao ulilenga kuonyesha kwamba aliingia katika nchi hiyo kinyume cha sheria.
Mwanaharakati huyu kutoka Sweden alisema: “Mimi na timu yangu tulitoa taarifa katika lango la uingiaji wa uwanja wa ndege wa Charles de Gaulle baada ya kuondoka Israel, kwamba hatukuvunja sheria yoyote, na tunatoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa wanaharakati wa haki za binadamu ambao bado wanashikiliwa mateka nchini Israel.”
Akaongeza kwa kusema: “Ninatoa ushahidi kwamba tulitekwa nyara katika maji ya kimataifa na tulipelekwa Israel kwa nguvu kinyume na matakwa yetu.”
Kuhusiana na matamshi ya serikali ya Trump yaliyomwita kuwa ni mtu mwenye hasira, alicheka na kusema: “Nadhani dunia kwa sasa inahitaji wanawake wenye hasira zaidi ili kuipata haki!”
Mapema siku ya Jumatatu, majeshi ya Israel yaliwateka watu waliokuwa kwenye meli ya misaada ya kibinadamu iliyokuwa ikielekea Ukanda wa Ghaza kwa lengo la kuvunja vizuizi vya baharini na kusambaza maziwa ya unga kwa watoto. Greta Thunberg alikuwa miongoni mwa watu 12 waliokuwa kwenye meli hiyo, wakiwemo pia waandishi wa habari.
Chanzo: A NEWS
Maoni yako