Alhamisi 15 Mei 2025 - 09:40
Ayatollahil-Udhma Jawadi Amuli: “Elimu, Akili na Malezi” ni nguzo tatu za ukombozi kwa Hawza na Vyuo Vikuu

Hawza/ Ayatollahil-Udhma Jawadi Amuli ametaja nguzo tatu za ukombozi, yaani “Elimu, Akili na Malezi”, kuwa ndio njia ya ustawi wa mtu binafsi na jamii katika hawza na vyuo vikuu katika ulimwengu wa Kiislamu.

Kwa mujibu wa kitengo cha kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, siku ya Jumanne tarehe 23 Ordibehesht (kwa kalenda ya Irani), Ayatollahil-Udhma Jawadi Amuli, mmoja wa marjaa wakubwa wa Kishia, alitoa hotuba katika mji mtakatifu wa Najafu Ashraf, katika kituo cha elimu cha Imamu Khui, mbele ya umati mkubwa wa mamia ya masheikh, wanafunzi na wanazuoni wa hawza.

Akiitukuza hadhi ya hawza ya kale na yenye mizizi ya Najafu, aliiita mfano dhahiri wa kauli ya Mwenyezi Mungu: “أُسِّسَ عَلَى التَّقْوَى” (iliyoasisiwa juu ya uchamungu), na akasema kuwa kuanzia Sheikh Tusi hadi Ayatollah Khui, watu wa Mwenyezi Mungu wamelelewa katika hawza hii, ambayo ni muonekano ya aya isemayo: "فِیهِ رِجَالٌ یُحِبُّونَ أَنْ یَتَطَهَّرُوا" (ndani yake wamo watu wanaopenda kujitakasa). Baraka hizi zote ni zao la wilaya ya walii kamili, Amirul-Mu’minin Ali (a.s.).

Ayatollah Jawadi, aligawanya mhimili wa hotuba yake katika sehemu mbili: “wadhifa chanya” na “wadhifa hasi” kwa wanafunzi wa dini. Katika sehemu ya kwanza, alisisitiza kuwa kujifunza elimu ni wadhifa wa kila mtu, na kwa kunukuu hadithi isemayo “kutafuta elimu ni faradhi”, alisema kuwa Mwenyezi Mungu ameweka mbingu, ardhi na vyote vilivyomo ndani yake chini ya himaya ya mwanadamu; hivyo hakuna mtu anayepaswa kusema “siwezi”. Ulimwengu huu ni maktaba ya Mwenyezi Mungu, na mwanadamu amepewa jukumu la kujifunza na kuutawala.

Ameeleza kuwa hawza zina wajibu wa kuwa na uelewa wa kina na sahihi wa Qur’an na Sunna za Ahlul-Bayt (a.s.), na kwamba vyuo vikuu vina wajibu wa kufahamu maumbile, mbingu, ardhi na vipengele vya kimada vya ulimwengu ili jamii ya Kiislamu iweze kujitegemea na kutotegemea Mashariki wala Magharibi.

Katika sehemu ya pili, Ayatollah Jawadi Amuli alisisitiza kuwa elimu pekee haitoshi, bali jamii inapaswa, mbali na kuwa na elimu, iwe na akili pia. Akasema kuwa jukumu letu si tu kuondoa ujinga wa kielimu na ujinga wa kivitendo, bali pia tunapaswa kupambana na ujinga wa kimuundo na mfumo wa kijinga. Aliongeza kuwa Imam si mwalimu wa dini tu, bali ni mwenye jukumu la kuitakasa jamii kutokana na ujinga wa kitamaduni.

Akirejea hadithi isemayo “Atakayekufa bila kumtambua Imam wa zama zake, atakuwa amekufa kifo cha kijinga”, alibainisha kuwa iwapo jamii haitoweza kuutambua na kuukubali uongozi wa Kimaimamu na mfumo wa wilaya, basi itabakia katika ujinga. Pia kwa kuashiria matukio ya vita vya Siffin na fitna ya tahkimi (hukumu), alisema kuwa baada ya fitna hizo, Amirul-Mu’minin Ali (a.s.) mara nyingi alisisitiza kuwa jamii imerejea katika ujinga, si kwa sababu ya ujinga wa mtu binafsi, bali kwa sababu ya kuangukia katika mfumo wa kijinga.

Katika sehemu muhimu ya hotuba yake, Ayatollah Jawadi Amuli alisisitiza haja ya kulea wanazuoni wataalamu wa ijtihadi wa kweli, na kusema kuwa kufuata bila kuelewa (taqlid) hakutatatua matatizo ya jamii. Aliweka wazi kuwa mtu mwenye uwezo anapaswa kuwa mujtahid, achimbue masuala kutoka katika vyanzo, arejeshe matawi kwenye misingi, na aweze kujibu mahitaji ya zama.

Alitaja nguzo tatu za ukombozi “Elimu, Akili na Malezi” kuwa ndiyo njia ya ustawi wa mtu na jamii katika hawza na vyuo vikuu katika ulimwengu wa Kiislamu, na hatimaye alimuombea dua kila Muislamu katika umma huu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha