Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hafidh Naeem-ur-Rehman, kiongozi wa Jamaat-e-Islami Pakistan, katika barua aliyo muandikia Rais wa Iran na viongozi wengine wa nchi za Kiislamu, ametoa wito wa mshikamano na kuwa na sauti moja kutoka kwa serikali za Kiislamu katika kuwatetea watu wanyonge wa Palestina. Ametilia mkazo umuhimu wa kuchukua misimamo madhubuti na ya pamoja ili kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni na kutoa msaada wa kweli kwa watu wa Gaza.
Katika barua hiyo, Hafidh Naeem-ur-Rehman amependekeza kwamba tarehe 20 Aprili itangazwe kuwa “Siku ya Mshikamano na Gaza.” Ameyataka mataifa ya Kiislamu kuonesha uungaji mkono wao kwa taifa la Palestina kupitia hafla na shughuli zilizoratibiwa kwa pamoja na kuusikilizisha ulimwengu sauti ya umma wa Kiislamu.
Kiongozi huyo wa Jamaat-e-Islami, akirejelea hali ya kutisha ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, ameandika kwamba: janga la kibinadamu huko Gaza limevuka mipaka yote ya mgogoro, na linamuumiza kila mwanadamu alie huru. Akitaja kushambuliwa makusudi kwa raia, hospitali, shule na makazi ya wakimbizi, ameelezea hali hiyo ya sasa kuwa ni mfano wa wazi wa jinai dhidi ya ubinadamu.
Hafidh Naeem-ur-Rehman, akilinganisha mgogoro wa sasa wa Ghaza na maafa ya kihistoria kama vile Holocaust, mauaji ya halaiki ya Bosnia, na mgogoro wa Kosovo, amekumbusha kuwa: tajiriba za zamani zimeonesha kuwa katika kukabiliana na migogoro ya aina hii, jamii ya kimataifa inapaswa kubeba wajibu wa kimaadili na kibinadamu. Leo hii, Ghaza nayo inakabiliwa na janga linalofanana, jambo linalohitajia mwitikio wa dharura kutoka kwa jamii ya kimataifa.
Katika hitimisho lake, amesisitiza juu ya uungaji mkono wa watu wa Pakistan kwa taifa la Palestina, amewaomba viongozi wa nchi za Kiislamu wachukue hatua za haraka, za pamoja na zenye ufanisi ili kukomesha mauaji na jinai za kila siku zinazofanywa na utawala wa Kizayuni, na kutekeleza ipasavyo wajibu wao wa kihistoria ndani ya wakati huu nyeti.
Maoni yako