Kwa mujibu wa taarifa ya kikundi cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawzah, Dkt. Muhammad Tahir al-Qadri, ambaye pia ni mwanzilishi wa harakati ya Minhaj-ul-Qur'an ya Pakistan, alieleza kuwa tukio la kuuwawa Imam Ali (a.s) lilikuwa ni janga kubwa katika historia ya uislamu, na alisisitiza kuwa shahada hii ilituma ujumbe kwa umma wa Kiislamu kwamba badala ya kufuata matamanio ya dunia ya muda, unapaswa kuzingatia mafanikio katika maisha ya Akhera kama lengo kuu la maisha yao.
Aliongeza kusema: "Maisha ya Imam Ali (a.s) yamejaa misingi na mafundisho ambayo hata leo hii yanatoa mwanga wa mwongozo wa thamani katika maisha yetu ya kijamii na kimaadili."
Mchambuzi huyu maarufu wa Ahlu-Sunna, katika hafla ya I'tikaf ya Manhaj-ul-Quran ya Pakistan iliyoongozwa na mada ya "Upendo wa Mwenyezimungu na ladha ya Tauhidi", alisisitiza: "Imam Ali (a.s) alikuwa ni mfano wa haki, ujasiri, na uaminifu. Yeye kwa subira, uvumilivu na kujitolea, aliuonesha umma wa kiislamu njia ya haki." Aliongeza kwa kusema: "Mafundisho ya Imam Ali (a.s) katika nyanja za subira, uvumilivu, haki, usawa, na huduma kwa ubinadamu, bado ni mwongozo muhimu kwa umma wa Kiislamu."
Alipozungumzia hali ngumu inayoukabili umma wa Kiislamu, alisema: "Kuongezeka kwa kutokufuata amri za Mwenyezi Mungu kumesababisha kupungua kwa rehema na baraka.
Mwezi mtukufu wa Ramadhani, hasa katika kumi la mwisho, ni fursa ya kujijua, kujikosoa na kurejea katika njia ya kimungu. Umma unapaswa kuyaacha maisha ya kughafilika na kutokana na toba na ibada, watu wanaweza kupata radhi za Mwenyezimungu."
Dkt. Tahir al-Qadri allkisisitiza umuhimu wa vijana katika mustakabali wa umma wa Kiislamu, alisema: "Mafanikio katika dunia na Akhera yako katika upendo wa dini na mapenzi kwa tabia nzuri ya Mtume Muhammad (s.a.w).
Vijana wanapaswa kuchukua mfano kutokana na mafundisho ya Imam Ali (a.s) na kuboresha maadili na tabia zao." Aliongeza: "Wale wanaovumilia magumu katika njia ya haki, watafikia mwisho mwema."
Dkt. Tahir al-Qadri alisisitiza: "Mafundisho ya Imam Ali (a.s) ni njia ya ukombozi kwa umma wa Kiislamu. Ikiwa umma wa Kiislamu utadumisha misingi ya haki, subira, na kujitolea vitu ambavyo Imam Ali (a.s) alitufundisha tushikamane navyo, utaweza kuzishinda changamoto na matatizo yote."
Aliongeza: "Kifo cha Imam Ali (a.s) kina ujumbe kwa umma kwamba njia ya mafanikio ni kurejea kwa Mwenyezimungu na kufuata njia ya haki na uadilifu.
Maoni yako