Kwa mujibu wa taarifa ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Eric Cantona, nyota wa zamani wa soka la Ufaransa na mshambuliaji wa zamani wa klabu ya Manchester United, alipokea jezi yenye mchoro uliobuniwa upya kutokana na tukio maarufu la teke lake la mtindo wa Kung Fu, wakati wa ziara yake katika jiji la Derry, nchini Ireland Kaskazini. Katika mchoro huo, safari hii anayelengwa na teke hilo ni Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Chris Frey, mbunifu wa michoro na mmiliki wa duka la “Frey Clever” lililopo katika jiji la Derry, alimkabidhi Cantona jezi hiyo kama zawadi wakati nyota huyo alipokuwa jijini humo kwa ajili ya kuendesha kipindi kilichoitwa “Eric, Mfalme Cantona”.
Kupitia mitandao ya kijamii, Frey alieleza furaha yake ya kukutana na mwanasoka huyo wa Ufaransa na kubainisha kuwa aliandaa mchoro huo kwa lengo la kuonesha mshikamano wake na Palestina. Kwa mujibu wa tovuti hiyo, Cantona pia alifurahishwa na kupokea zawadi hiyo.
Mchoro huo ulikuwa umeoneshwa awali katika kioo cha maonesho ya duka la Frey, na uliposambazwa kwenye mitandao ya kijamii ulizua maoni mbalimbali, kuanzia ya kuuunga mkono na kufanya mzaha, hadi yale ya kuukosoa.
Cantona, ambaye ni miongoni mwa watu mashuhuri wanaounga mkono haki za Wapalestina, amekuwa akilaani mara kadhaa sera za utawala wa Kizayuni wa Israel, na pia ameitaka Israel kuzuiwa kushiriki katika mashindano ya kimataifa.
Aidha, amelikosoa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) kutokana na kile alichokieleza kuwa ni matumizi ya viwango viwili tofauti katika namna yanavyoichukulia Israel na Urusi.
Maoni yako