Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Tehran, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Ahmad Khatami, Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya wiki hii mjini Tehran, katika hotuba zake za Swala ya Ijumaa, huku akizungumzia umuhimu wa kumtegemea Mwenyezi Mungu katika kukabiliana na maadui, amesema: Kumtegemea Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa hazina kubwa za Jihadi ya Haki. Nabii Musa (a.s), alipokabiliana na Firauni ambaye alikuwa ametawala kwa zaidi ya karne tatu, aliwausia watu wake kwamba ikiwa wanamwamini Mwenyezi Mungu, basi wamtegemee Yeye na wafahamu kuwa Mwenyezi Mungu atakuwa msaidizi wao.
Akizungumzia mifano mingine ya Mitume wa Mwenyezi Mungu katika kumtegemea Mola wao, ameongeza kuwa; Nabii Hud (a.s) naye, alipokabiliana na maadui zake, alitangaza kwa kusema: Mimi namfanya Mwenyezi Mungu kuwa shahidi, wala siogopi njama na ushirikiano wenu nyote, kwa sababu mimi namtegemea Mwenyezi Mungu, Mola wangu na Mola wenu. Vilevile, Mtume Mtukufu wa Uislamu (s.a.w.w), alipokabiliana na maadui zake, alisema: Mwenyezi Mungu anatutosheleza, na Kwake Yeye pekee tunategemea.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran, akieleza kuwa; kumtegemea Mwenyezi Mungu kumekuwa miongoni mwa nguzo kuu za Mapinduzi ya Kiislamu, amesisitiza: Imam Khomeini (r.a) aliweza kuyafikisha Mapinduzi ya Kiislamu kwenye ushindi kwa kutegemea hazina hii kubwa. Kadhalika, Imam wetu Shahidi, kwa kutegemea msaada huo wa Mwenyezi Mungu, aliyaongoza Mapinduzi ya Kiislamu katika safari yake ya miaka 47.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Khatami, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha utamaduni wa kumtegemea Mwenyezi Mungu na kuziamini ahadi Zake ndani ya jamii, amevielekea vyombo vya habari kwa kusema: Kama Khatibu wa Swala ya Ijumaa ambaye miongoni mwa majukumu yake ni kuwalingania watu katika kumcha Mwenyezi Mungu, ninaviomba vyombo vya habari vya televisheni, redio na magazeti, pamoja na wanaharakati wa mitandao ya kijamii, watimize wajibu wao katika kuimarisha hazina hii yenye thamani kubwa ndani ya jamii.
Katika kuendelea na hotuba yake, amezungumzia fundisho jingine linalopatikana katika mwenendo wa Mtume Mtukufu (s.a.w.w) kuhusu namna ya kukabiliana na adui, akasema: Mtume wa Uislamu, wakati wa Vita vya Uhud na baada ya vita hivyo, alisisitiza umuhimu wa uwepo wa vikosi vyenye imani na itikadi thabiti katika medani; vikosi ambavyo vinashiriki katika medani ya kuutetea Uislamu vikiwa na imani na ari ya kweli.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran, akikumbusha tukio la Waislamu kushiriki katika vita vya Hamra al-Asad baada ya Vita vya Uhud, amesema: Baada ya Vita vya Uhud, katika hali ambayo baadhi ya Waislamu walikuwa wamejeruhiwa na miili yao ikiwa na majeraha mengi, waliposikia amri ya Mtume (s.a.w.w) ya kwenda vitani, hata wale waliokuwa wakishughulikia matibabu ya majeruhi walijitokeza kwenda kushirikiana na Mtume.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Khatami ameendelea kusema: Katika tukio hilo, ndugu wawili ambao wote walikuwa wamejeruhiwa nao walijiunga na kundi la Waislamu, Abu Sufyan alipofahamu hali ya Waislamu na safari yao ya kwenda kukabiliana na jeshi la adui, alikabiliwa na ukweli kwamba jeshi lenye wapiganaji wenye imani na dhamira thabiti lilikuwa likielekea vitani; wapiganaji ambao hawangesitisha mapambano hadi adui ashindwe kikamilifu, jambo hilo lilimfanya Abu Sufyan ahisi hatari, hivyo akaamua kujiondoa na kuepuka kukabiliana nao tena.
Ametaja tukio hili la kihistoria kuwa ni mfano wa nguvu ya imani na ari ya wapiganaji, na akirejelea Aya ya 174 ya Suratul Aal-Imran, amesema kuwa; hiyo ndiyo nishani ya heshima wanayoipata wapiganaji wenye imani thabiti.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran, katika kuendelea na hotuba yake na akiwahutubia wananchi wa Iran, amesema: Ninawapa bishara njema, enyi wananchi wa Iran, kwamba wapiganaji wenu ni wa aina hiyo hiyo. Vikosi vya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, vikiwemo Jeshi la Wananchi, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah), Basij na Jeshi la Polisi, vyote vina silaha ya imani na itikadi hiyo.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Khatami amesisitiza: Inshaallah, iwapo adui atafanya kosa hata dogo kabisa, vikosi hivi vyenye imani na uwezo mkubwa vitampiga adui huyo pigo kali lisilosahaulika.
Katika kuhitimisha sehemu hiyo ya hotuba yake, amemuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu aijaalie ushindi Jihadi ya Uislamu dhidi ya Jihadi ya Ukafiri, azibatilisha njama za maadui dhidi ya mfumo wa Kiislamu na awaangamize.
Wiki ya chuki ya Iran na dunia dhidi ya Marekani
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, akizungumzia matukio ya wiki iliyopita, amesema: Wiki iliyopita ilikuwa ni wiki ya chuki ya Iran na dunia dhidi ya Marekani. Kauli mbiu ambayo wananchi wa Iran wamekuwa wakiitoa kwa miaka 47 sasa, katika wiki hii ilisikika pia ndani ya Marekani yenyewe, na mabadiliko ya kisiasa ya nchi hiyo yalisababisha kushindwa wafuasi wa Republican.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran, akifafanua mabadiliko hayo, amezungumzia kufanyika maandamano ya tarehe 13 Aban katika miji 900 ya nchi hiyo, akasema: Katika miji yote hiyo, kauli mbiu kuu ya wananchi ilikuwa ni “Mauti kwa Marekani.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Khatami, akizungumzia kutekwa kituo cha ujasusi cha Marekani tarehe 13 Aban mwaka 1358 Hijria Shamsia (1979), ameongeza kuwa; siku hiyo wananchi wa Iran waliiondoa Marekani nchini mwao, na leo hii, tarehe 13 Aban mwaka 1405 Hijria Shamsia (2026), wananchi wa Iran wana dhamira ya kuyafanya mipango ya Marekani katika eneo hili ishindwe kutimia.
Katika kuendelea na hotuba yake, akisisitiza kuwa kauli mbiu ya “Mauti kwa Marekani” ina mizizi yake katika misingi ya Qur'ani, amesema: Kwanza, Marekani ni nchi dhalimu, na Qur'ani Tukufu inasema:
«أَلا لَعْنَةُ اللَّهِ عَلَی الظَّالِمِینَ»
“Fahamuni kuwa laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya madhalimu.”
Pili, viongozi wa Marekani, kwa mujibu wa maelezo ya Qur'ani, wanajumuishwa katika kundi la waharibifu. Na tatu, wanasiasa wa Marekani ni watu wanaojihusisha na kusema uongo.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran, akirejelea Aya za Qur'ani zinazozungumzia dhuluma, ufisadi na kusema uongo, amesisitiza kuwa; kwa hiyo kauli mbiu ya “Mauti kwa Marekani” si kauli mbiu isiyo na msingi, bali ni kauli mbiu inayotokana na misingi ya kidini na Qur'ani. Amesema kuwa maadamu vitendo vya kichochezi na uovu wa Marekani vitaendelea, kauli mbiu hiyo haitaondoka katika ndimi za wananchi wa Iran.
Kushindwa kwa Netanyahu na Republican katika mabadiliko ya kisiasa
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Khatami, katika kuendelea na hotuba yake, amezungumzia chaguzi mbili zilizofanyika katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na nchini Marekani, akasema: Katika uchaguzi wa utawala wa Kizayuni, Netanyahu hakuweza kupata kiwango cha kura kilichohitajika ili kuunda tena serikali, na kwa hakika ameshindwa. Ameongeza kuwa inawezekana mikondo mbalimbali ya kisiasa ndani ya utawala huo ikafanya juhudi za kufikia muafaka na kuunda serikali, lakini ukweli ni kwamba Netanyahu ameshindwa katika uchaguzi huu.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran, katika sehemu nyingine ya hotuba yake, akizungumzia athari za matukio ya Iran katika siasa za ndani za Marekani, amesema: Kwa mara nyingine tena, Iran imeonesha kuwa inaweza hata kuathiri hatima ya kisiasa ya Marekani. Akikumbusha tukio la uchaguzi wa Marekani wa mwaka 1980 na kushindwa Jimmy Carter, amenukuu simulizi ya matamshi yake, akisema kuwa wakati huo Carter alionesha mshangao wake kutokana na ukweli kwamba hatima ya kisiasa ya Marekani ilikuwa imeathiriwa na matukio yaliyotokea Tehran.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Khatami, vilevile akizungumzia uchaguzi wa hivi karibuni nchini Marekani, amedai kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizotajwa, asilimia 74 ya wapiga kura walioshiriki katika uchaguzi walionesha upinzani wao dhidi ya Trump kutokana na shambulio dhidi ya Iran na vita vilivyoanzishwa dhidi ya nchi yao.
Akizungumzia misimamo ya Trump kuhusu matokeo ya vita dhidi ya Iran, ameongeza kuwa; hata Trump mwenyewe amekiri kuwa vita dhidi ya Iran ndivyo vilivyoifikisha Marekani katika hali iliyopo sasa, na mwenendo huu unaweza kusababisha madhara magumu zaidi kwa Washington.
Wilayat al-Faqih: Mhimili wa kuendeleza ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu
Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran, katika kuhitimisha hotuba zake, akisisitiza umuhimu wa kuhifadhi na kuendeleza mafanikio ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema: Tunapaswa kuendeleza ushindi huu, kwa sababu mafanikio haya yamepatikana kutokana na baraka za Wilayat al-Faqih.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Khatami, akikumbusha nasaha za Imam Khomeini (r.a) aliposema: “Iungeni mkono Wilayat al-Faqih ili nchi yenu isipate madhara,” amesisitiza kuwa; hivi sasa pia tuna Kiongozi shujaa na mwenye uelewa wa kina, ambaye anaendeleza njia ya Imam Khomeini (r.a) na Imam Shahidi. Kwa hiyo, tunapaswa kutambua thamani ya neema hii.
Amesema kuwa njia pekee ya kuweka kizuizi chenye ufanisi dhidi ya maadui ni kuimarisha nguvu ya taifa na kuhifadhi moyo wa kutokubali kushindwa. Amefafanua kuwa mkakati wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unapaswa kuwa ni kuelekea kwenye kuwa na nguvu zaidi na uimara mkubwa zaidi. Mwelekeo wowote wa kusalimu amri mbele ya adui mwenye kiburi na ubeberu utampa ujasiri zaidi wa kuongeza madai yake na kuendelea na vitendo vyake vya uhasama.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran, akionya dhidi ya kuwa na matumaini ya kupita kiasi kuhusu kubadilika mwenendo wa mfumo wa utawala wa kibeberu, ameongeza kuwa; wale ambao bado wana matumaini ya kubadilika kwa asili na mwenendo wa mfumo huo wamekosea sana, kwa sababu uzoefu umeonesha kuwa njia ya kukabiliana na adui ni kuhifadhi nguvu na kusimama imara.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Khatami, katika kuhitimisha hotuba yake, akirejelea kauli ya mwandishi wa Misri, Hassanein Heikal, kuhusu nafasi ya Wilayat al-Faqih, amesema: Heikal ana kauli fulani kuhusu Wilayat al-Faqih, lakini mimi kwa upande wangu nasema hivi: Amirul-Muuminina Imam Ali (a.s) ndiye aliyeitengeneza bomu hili, na Imam Khomeini (r.a) ndiye aliyelilipua chini ya miguu ya Marekani.
Katika kuhitimisha, amemuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu azidhoofishe juhudi za maadui wa Uislamu na wale wanaofanya njama dhidi ya mfumo wa Kiislamu, na aendelee kuilinda na kuisitiri jamii ya wananchi wa Iran kwa uwepo wa mfumo wa Kiislamu na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi.
Maoni yako