Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Alireza Arafi, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, alifanya ziara ya kutembelea moja kwa moja kwa muda wa dakika 200 katika vituo vya kale na vyenye athari kubwa zaidi za kielimu katika ulimwengu wa Kishia, ambavyo ni Hawza za Faidhiyyah na Darush-Shifaa zilizopo Qum.
Katika ziara hiyo, alikutana ana kwa ana na walimu, viongozi wa usimamizi na wanafunzi vijana wa Hawza, na kujadili hali ya sasa ya masuala ya elimu, utafiti pamoja na changamoto na mahitaji yao mbalimbali.
Kutembelea vyumba vya wanafunzi wa Hawza, kukagua hazina ya Kituo cha Nyaraka na Makumbusho ya Hawza na Wanazuoni wa Dini, kufuatilia maudhui ya maonesho yanayohusu ukosoaji wa makundi potofu na uradidi wa kiroho wa uongo katika Kituo cha FAM cha Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Hawza ya Qum anayeshughulikia masuala ya Da'wa na Utamaduni, kusimamisha Swala ya jamaa, pamoja na kusimulia kumbukumbu za kusisimua za siku za mapambano na harakati za kishujaa katika kipindi cha kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu, vilikuwa miongoni mwa vipengele muhimu vya ziara hiyo iliyochukua zaidi ya saa tatu.
Mwanzo wa ziara: Kuingia bila taarifa katika kitovu cha harakati za Kiislamu
Katikati ya mchana, uwanja wa kihistoria na njia zilizojengwa kwa mawe katika Hawza ya Faidhiyyah vilipokea hatua za Mkurugenzi wa Hawza. Ujio wa Ayatullah Arafi bila taratibu za kifahari wala taarifa ya awali, tangu dakika za mwanzo, ulibadilisha hali ya kawaida ya kituo hiki cha muda mrefu cha elimu ya Fiqhi na maarifa ya kidini.
Faidhiyyah si alama ya elimu na Fiqhi pekee, bali pia ni utambulisho wa kihistoria wa harakati za Kiislamu na kitovu cha matukio muhimu yaliyobadilisha historia ya zama za hivi karibuni. Ni mahali ambapo kila chumba cha wanafunzi na kila baraza yake vina simulizi ya mashujaa na matukio makubwa ya kihistoria.
Baada ya kuwasili, Ayatullah Arafi alielekea moja kwa moja katika uwanja na madarasa makuu ya Hawza, ambako alijionea kwa karibu shughuli za sasa za kielimu, utaratibu wa masomo ya ngazi za juu na mahudhurio ya wanafunzi katika shughuli za kielimu.
Ujio huu wa moja kwa moja katika mazingira ya wanafunzi ulikuwa ishara ya uhusiano endelevu kati ya uongozi wa Hawza na msingi wake mkuu unaojumuisha walimu na wanafunzi. Hii ni desturi ya muda mrefu ambayo kuendelezwa kwake kunahakikisha uchangamfu wa kielimu na maendeleo ya Hawza.
Majadiliano na walimu pamoja na viongozi wa Hawza
Katika kuendelea na ratiba hiyo ya dakika 200, Mkurugenzi wa Hawza alifanya kikao kifupi lakini chenye maudhui mengi na viongozi wa kiutendaji, manaibu wanaoshughulikia masuala ya elimu na malezi ya kiroho, pamoja na baadhi ya walimu waliokuwepo katika Hawza za Faidhiyyah na Darush-Shifaa.
Katika kikao hicho, walifanya tathmini ya taratibu za ufundishaji na hali ya programu mbalimbali za sasa. Katika majadiliano hayo, mambo yafuatayo yalikuwa miongoni mwa mada kuu zilizojadiliwa:
1. Nidhamu ya kimapokeo na ufanisi wa mfumo wa Hawza:
Kufufua utamaduni wa majadiliano ya kina ya kielimu, kuandika na kurekodi maelezo ya masomo, pamoja na kuimarisha mawasiliano ya ana kwa ana kati ya mwanafunzi na mwalimu, hizi ni sifa za kipekee ambazo zimekuwa zikiitambulisha Hawza katika historia yake yote.
2. Kutumia mifumo mipya ya usimamizi:
Kuboresha kiwango cha huduma na vifaa vya kielimu, kuzipatia Hawza maktaba za kidijitali na kurahisisha upatikanaji wa vyanzo vya msingi vya utafiti kwa wanafunzi.
3. Kusisitiza nafasi ya walimu kama vielelezo vya kuigwa:
Kuimarisha vipengele vya malezi na maadili sambamba na ufundishaji wa elimu za kiakili na za mapokezi, kwa namna ambayo utakaso wa nafsi uendane sambamba na maendeleo ya kielimu.
Ayatullah Arafi, akipongeza juhudi za usiku na mchana zinazofanywa kwa kujituma na moyo wa kujitolea na wafanyakazi wa usimamizi wa Faidhiyyah na Darush-Shifaa, alizitaja Hawza hizo mbili kuwa ni mstari wa mbele katika harakati za kimawazo na kiroho za mji wa Qum. Pia alisisitiza umuhimu wa kufuatilia kwa ukaribu na mara kwa mara mwenendo wa maendeleo ya kielimu ya wanafunzi wa Hawza.
Kufuatilia makundi potofu katika maonesho ya Kituo cha FAM: Umuhimu wa kujibu kikamilifu shubha na maswali ya kisasa
Sehemu nyingine ya ziara hiyo ilihusisha kutembelea maonesho maalumu yenye mada ya “Makundi Potofu na Mikondo Mipya ya iliyokengeuka” yaliyoandaliwa na Kituo cha FAM cha Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Hawza ya Qum anayeshughulikia masuala ya Da'wa na Utamaduni. Katika sehemu hii, yaliwasilishwa matokeo ya tafiti za hivi karibuni, nyaraka, vitabu na michoro ya ufafanuzi kuhusu chimbuko, mbinu na nyenzo zinazotumiwa na makundi yaliyokengeuka na yasio sahihi pamoja na mikondo inayobuni imani na mafundisho mapya ya uzushi.
Miongoni mwa makundi na mikondo hiyo ni Ahmad al-Hasan, harakati za kuabudu na kutukuza ustaarabu wa kale, Uwahabi na Ubaha'i, ambazo zinajaribu kupenyeza fikra zao miongoni mwa kizazi cha vijana na jamii za Kiislamu.
Katika ziara hiyo, Muhammad Jawad Nasiri, Mkurugenzi wa Kituo cha Uendeshaji cha FAM, alieleza muundo na uwezo wa kituo hicho, huku akiwasilisha ripoti kuhusu shughuli na hatua mbalimbali za kitaalamu zinazofanywa na kituo katika kukabiliana na makundi potofu. Akifafanua majukumu ya kituo hicho, alieleza shughuli zilizotekelezwa katika eneo la ukosoaji na uchambuzi wa kitaalamu wa kimapinduzi wa madhehebu na makundi potofu, utoaji wa huduma za ushauri kwa watu walioathiriwa na makundi hayo, pamoja na hatua za kiutamaduni na kinga zinazolenga kutoa uelewa kwa umma na kuzuia kupenya na kuenea madhehebu na upotofu wa kimawazo na kiroho.
Katika kuendelea na ziara hiyo, yaliandaliwa maonesho ya kazi mbalimbali na nyaraka zinazohusiana na madhehebu na makundi potofu, mabango yanayotambulisha madhehebu hayo, pamoja na mifano ya bidhaa na vitu mbalimbali vya kiroho vinavyohusishwa na mikondo mipya inayojitokeza.
Vilevile, wataalamu wa vitengo mbalimbali vya kituo hicho, huku wakieleza maeneo yao maalumu ya shughuli, waliwasilisha ripoti kuhusu hatua zilizochukuliwa, mafanikio yaliyopatikana na mipango ya kila kitengo.
Kufungua kurasa za historia katika Makumbusho na Kituo cha Nyaraka za Hawza na Wanazuoni wa Dini
Hatua iliyofuata katika ziara hiyo ilikuwa kutembelea Makumbusho na Kituo cha Nyaraka za Hawza na Wanazuoni wa Dini. Kituo hiki ni hazina adimu ya kihistoria inayohifadhi nyaraka za maandishi ya mkono, barua za Maraji' wakubwa wa Taqalidi, matangazo na maandishi ya mkono ya kipindi cha harakati za Mapinduzi, pamoja na historia ya mwenendo wa kijamii wa wanazuoni wa Kishia.
Wakati wa kutembelea nyaraka zilizofanyiwa ukarabati wa hivi karibuni na sehemu mbalimbali za kumbukumbu za kihistoria, Ayatullah Arafi alisema kuwa; kuhifadhi urithi huu wa ustaarabu ni wajibu wa kidini na wa kulinda utambulisho wetu.
Mkurugenzi wa Hawza za Kiislamu alibainisha kwamba: Utambulisho wa Kishia na historia ya utendaji wa wanazuoni wa dini katika kulitumikia dini na kuwaunga mkono wanyonge vinaonekana wazi kupitia nyaraka hizi. Kwa hiyo, ni lazima kwa kutumia teknolojia za kidijitali, nyaraka hizo ziwekwe katika mazingira yatakayowawezesha watafiti, wanahistoria na wasomi wa Hawza na vyuo vikuu kuzitumia, ili simulizi zilizopotoshwa zisiweze kuharibu kumbukumbu za kihistoria za vizazi vijavyo.

Mandhari Nzuri: Kusimamishwa Swala katika Mihrabu ya kumbukumbu za kihistoria
Sauti nzuri ya adhana ya adhuhuri iliposikika katika eneo takatifu la Haram ya Bibi Fatimah Ma'sumah (s.a.), ziara ya dakika 200 ya Mkurugenzi wa Hawza ilihitimishwa katika Mihrabu ya kale ya Hawza ya Faidhiyyah. Uwanja na ukumbi wa Swala wa Faidhiyyah ulijaa waumini, walimu wakongwe, wahudumu, watafiti na wanafunzi vijana wa Hawza.
Swala ya Adhuhuri na Alasiri ilisimamishwa kwa uimamu wa Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Muhammad Shubeiri Zanjani, katika mazingira yaliyojaa utulivu na hali ya kiroho. Hii ilikuwa taswira ya wazi ya umoja, nidhamu na uimara wa Hawza ambayo mizizi yake imejikita katika misingi halisi ya historia ya zaidi ya miaka elfu moja, huku dira yake ikiwa imeelekezwa katika kufikia kilele cha mafanikio ya kesho na kutatua mahitaji ya Umma wa Kiislamu.
Ripoti: Akbar Pustchian
Maoni yako