Jumatatu 2 Novemba 2026 - 18:58
Hukumu ya kuuawa Sheikh Hussein Al-Matouq inadhihirisha kuwa vita dhidi ya wafuasi wa Ahlul-Bayt (as) ni vita vya Kizayuni vinavyojivika vazi la Kiarabu

Hawza/ Sheikh Adel Al-Shaala, mwanazuoni wa Kishia kutoka Bahrain, amelaani hukumu ya kifo iliyotolewa dhidi ya Sheikh Hussein Al-Matouq, akiitaja hatua hiyo kuwa ni hukumu ya «kitwa'ghuti», na kusisitiza kwamba vita vinavyoendeshwa dhidi ya wafuasi wa Ahlul-Bayt (as) katika eneo hili ni vita vya kisiasa na Kizayuni vinavyojionesha katika sura ya Kiarabu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Adel Al-Shaala, mwanazuoni wa Kishia kutoka Bahrain, katika hotuba yake alisisitiza kwamba: Endapo dini itakabiliwa na tishio kutoka kwa mtawala Mwislamu, jukumu la waumini ni kupambana na hatari yake; kwa sababu mtawala wa aina hiyo ni miongoni mwa mataghuti madhalimu, hata kama yeye ni Mwislamu, maadamu anatawala kwa kutumia dhuluma, uonevu na uvamizi dhidi ya Waislamu, basi anahesabiwa kuwa miongoni mwa «waasi» (Bughaat), ambao jihadi dhidi ya dhuluma na uasi wao ni wajibu katika harakati za kuipigania dini.

Ili kuthibitisha kauli hiyo, alirejelea msimamo wa Imam Hussein (as) dhidi ya Yazid, ambapo alisema:

«مَنْ رَأَی سُلْطَاناً جَائِراً، مُسْتَحِلًّا لِحُرُمِ اللَّهِ، نَاکِثاً لِعَهْدِ اللَّهِ، مُخَالِفاً لِسُنَّةِ رَسُولِ اللَّهِ، یَعْمَلُ فِی عِبَادِ اللَّهِ بِالْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ، ثُمَّ لَمْ یُغَیِّرْ بِقَوْلٍ وَلَا فِعْلٍ، کَانَ حَقِیقاً عَلَی اللَّهِ أَنْ یُدْخِلَهُ مَدْخَلَهُ».

«Mtu yeyote atakayemuona mtawala dhalimu anayehalalisha mambo ambayo Mwenyezi Mungu ameyaharamisha, anayevunja ahadi ya Mwenyezi Mungu, anayepinga mwenendo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, na anayetenda dhambi na kuvuka mipaka miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu, kisha asifanye mabadiliko yoyote kwa kauli wala kwa vitendo vyake, basi ni haki ya Mwenyezi Mungu kumuingiza katika makazi yale yale ambayo (Yazid) ataingia.»

Alibainisha kuwa kuutetea Uislamu wa kweli hakuna umuhimu mdogo kuliko kutetea uhai, mali, heshima au familia ya mtu.

Kuhusiana na maamuzi ya tawala zinazotawala katika eneo la Ghuba ya Uajemi, ambayo yanalenga kuibana dini, Sheikh Al-Shaala alisisitiza jambo hili: Kumnusuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kunatimia kupitia kuunga mkono swala ya Ijumaa na swala za jamaa; ambazo Mwenyezi Mungu amezitayarisha kwa ajili ya kuabudiwa Kwake.

Alieleza kuwa, katika siku hizi, ibada za aina hii nchini Bahrain zinashambuliwa kwa njia ya kuwakamata kilazima makumi ya maulamaa kwa tuhuma za udanganyifu na makosa ya dhambi, pamoja na kuzuia kwa nguvu kuswaliwa swala ya Ijumaa, ikiwemo swala ya Ijumaa ambayo ni miongoni mwa swala kubwa zaidi za Ijumaa nchini Bahrain. Haya yanafanyika kwa kutumia nguvu za kiusalama na kijeshi, sambamba na kuwakamata maimamu wote wa swala za Ijumaa, idadi ya swala za Ijumaa ambazo zimepigwa marufuku na utawala wa Bahrain imefikia 109.

Aliongeza kuwa, kumnusuru Mwenyezi Mungu kunafanyika kwa kuunga mkono yale ambayo Mwenyezi Mungu ameyaandaa kwa ajili ya kuwaongoza viumbe Wake, yakiwemo kuiunga mkono Qur’ani, Sunna ya Mtume na kizazi chake kitoharifu (rehema na amani ziwe juu yao wote). Miongoni mwa njia za kufikia lengo hili ni hotuba na mazungumzo ya kidini, na kuunga mkono uhuru wa hotuba hizo kwa hakika ni kuinusuru dini yenyewe.

Kupambana na watawala madhalimu ni jukumu la waumini hata kama ni Waislamu

Alisisitiza kwamba, pale dini inapokabiliwa na hatari, waumini wana jukumu la kufanya muqawama wa amani kwa kutumia hekima na mawaidha mazuri, na kutomruhusu dhalimu kuiathiri dini kwa madhara yoyote. Muqawama huu wakati mwingine hufanyika kwa njia ya «moja kwa moja» na kwa kuchukua msimamo dhidi ya maovu, na wakati mwingine hufanyika kwa njia ya «isiyo ya moja kwa moja».

Mwanazuoni huyo wa Bahrain aliendelea kusema kwamba, muqawama wa amani usio wa moja kwa moja unajumuisha hatua mbalimbali, kama vile kupinga maamuzi ya hivi karibuni ya mamlaka yanayolenga kuitawala dini.

Miongoni mwa maamuzi hayo ni kukata uhusiano na watu wanaopata vibali rasmi vya kusimamia swala za jamaa, kutoa hotuba, kupanda juu ya mimbari, kufanya madaha ya kidini au kupokea na kusambaza haki za kisheria.

Aliongeza kuwa; waumini wanapaswa kujitenga na watu hao katika yale yanayohusiana na maovu hayo. Hii ni pamoja na kujiepusha na kuswali nyuma yao, kuhudhuria kwenye mimbari zao au katika mawakibu zao, au kuwakabidhi haki za kikanuni; ili kwamba twaghuti asiweze kuyatawala na kuyaingilia mambo ya dini.

Katika kuendelea kufafanua suala hilo, Sheikh Al-Shaala alisema kuwa, pia kuna muqawama wa amani wa moja kwa moja, ambao unatekelezwa kwa kutokubali kupokea vibali kutoka kwa viongozi wanaohusika na misikiti, mimbari, Husainiya, mawakibu na haki za kikanuni. Maana yake ni kwamba kila mtu anapaswa kujiepusha na kuwa «kama mnyama anayekamuliwa maziwa yake au kipando kinachopandwa na mtu mwingine». Kwa kufanya hivyo, jamii haitalazimika kubeba jukumu la muqawama wa amani usio wa moja kwa moja peke yake, kiwango na namna ya kuitetea dini huamuliwa na faqihi mwadilifu mwenye sifa zinazotakiwa za uongozi wa kisiasa na kisharia.

Aidha, alikosoa kukamatwa maulamaa wa wafuasi wa Ahlul-Bayt (as) nchini Bahrain, Imarati na Kuwait, pamoja na kuwaweka katika mazingira ya shinikizo ndani ya mahakama za kubuni na kutaka kuzitawala dini zao.

Akilaani hukumu ya kifo dhidi ya Ayatullah Sheikh Hussein Al-Matouq, alisema: Suala hili halihusiani na hali fulani maalumu ya kiusalama, bali ni mpango uliopangwa unaolenga dini ya Mtume Mtukufu (saww) na Ahlul-Bayt (as).

Sheikh Al-Shaala aliongeza: Sisemi kwamba hivi ni vita vya kimadhehebu, kwa sababu wafuasi wa Ahlul-Bayt (as) ni watu wanaopenda amani na wanaowaunga mkono ndugu zao Waislamu katika sehemu mbalimbali za dunia. Waislamu wenye uelewa wanajua kwamba Mashia wako pamoja nao katika nyakati za shida, jihadi na kudhulumiwa, vita vinavyoendeshwa dhidi ya Mashia havitokani na sababu nyingine isipokuwa msimamo wao wa kuiunga mkono Palestina.

Alifafanua kwamba; vita vinavyoendelea katika eneo la Ghuba ya Uajemi dhidi ya Ahlul-Bayt (as) si vita kati ya makundi mawili ya kimadhehebu, bali ni vita vya kisiasa dhidi ya Mashia, ambapo ubaguzi wa kimadhehebu unatumiwa kama silaha ya Kizayuni kwa ajili ya kuzusha mgawanyiko na kufikia ubabe na kujipatia mamlaka ya juu.

Mwisho wa hotuba yake, Sheikh Al-Shaala alisisitiza tena na kulaani ukamataji unaofanyika katika eneo hili, hususan kukamatwa wanawake waumini na maulamaa wa kweli. Aidha, alilaani vikali hukumu zote za vifungo vya dhuluma katika eneo la Ghuba ya Uajemi, ambazo zimetolewa kupitia mahakama zisizo na uwazi wala uadilifu, hususan hukumu za vifo ambazo zimezichukulia damu takatifu kuwa ni jambo lisilo na thamani.

Akizungumzia hukumu ya hivi karibuni ya kifo dhidi ya mwanazuoni na mtu mwenye nafasi muhimu katika jamii, Sheikh Al-Matouq, pamoja na ndugu zake waumini, alisisitiza kwamba; hukumu hizi za kitwaghuti zinadhihirisha kuwa vita ambavyo wafuasi wa Ahlul-Bayt (as) wanakabiliana navyo katika eneo hili ni vita vya Kizayuni vinavyojivika vazi la Kiarabu-Kiebrania; vita vinavyowafanya waamini kwamba dini yao na haki zao ziko katika hatari na zinatishiwa.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha