Jumatatu 2 Novemba 2026 - 21:00
Kiongozi mmoja wa Kihindu atoa maelezo ya kuvutia kuhusiana na hadhi ya Bibi Fatimah Zahra (as)

Hawza/ Yogi Chandra Nath Maharaj, mmoja wa viongozi wa kidini wa Wahindu nchini Nepal, akizungumzia nafasi na hadhi ya juu ya Bibi Fatimah Zahra (as), alisema: “Waislamu hawana haja ya kutafuta kielelezo kingine, kwani shakhsia ya Bibi Fatimah Zahra (as) ni mfano kamili unaojumuisha sifa zote tukufu na fadhila zote za kimaadili.”

Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, kongamano lililopewa anuani ya “Ujumbe wa Amani wa Bibi Fatimah Zahra (as)” lilifanyika nchini Nepal, likihudhuriwa na kundi la wafuasi wa madhehebu ya Shia, Ahlus-Sunna pamoja na dini ya Kihindu. Kongamano hilo, lililojikita katika mwenendo na fadhila za Bibi Fatimah Zahra (as), lilisisitiza umuhimu wa amani, kuishi pamoja kwa amani na mazungumzo baina ya dini mbalimbali.

Hafla hiyo ilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo cha Tiba za Kichina cha Jadi, katika mji wa Nepalganj, na ilianza kwa kusomwa aya za Qur’ani Tukufu zilizosomwa na Swaghir Ahmad Khan, msomaji wa Qur’ani dhehebu la Ahlus-Sunna. Baada ya hapo, Abu Sahma Danish, mmoja wa wanafunzi wa Ahlus-Sunna, alisoma mashairi ya kumsifu Mtume Muhammad (saww).

Katika sehemu nyingine ya hafla hiyo, kundi la washairi kutoka Ahlus-Sunna, wakiwemo Ashfaq, Mi’raj Himalaya, Sayyid Ashfaq Rasul Hashimi, Sarwar Nepali na Haji Qadir Ansari, waliwasilisha mashairi ya kumsifu Bibi Fatimah Zahra (as), wakidhihirisha mapenzi na heshima yao kwa mwanamke huyo mtukufu.

Vilevile, baadhi ya wanawake wa Kishia na Ahlus-Sunna, akiwemo Thana Shad na Masrur Fatimah, walitoa heshima zao kwa hadhi tukufu ya Bibi Zahra (as) kwa kusoma mashairi yaliyohusu utukufu wake.

Katika kuendelea hafla hiyo, Shahida Shah Wahidi alitoa hotuba kwa lugha ya Kinepali, ambapo alizungumzia nyanja mbalimbali za mwenendo na shakhsia ya Bibi Fatimah Zahra (as), huku akifafanua nafasi na mchango wa mtukufu huyo katika maisha ya mtu binafsi na ya kijamii.

Sushila Nepali, mwakilishi wa Wahindu katika Bunge la Nepal na mgeni maalumu wa kongamano hilo, naye katika hotuba yake alisema kuwa; kushiriki katika programu hiyo kulimpa fursa kwa mara ya kwanza ya kufahamu mtazamo wa Uislamu kuhusu nafasi na hadhi ya mwanamke.

Akizungumzia suala la hijabu, aliongeza kuwa: “Hijabu si kizuizi cha maendeleo ya wanawake, bali ni njia ya kulinda heshima, staha na usafi wa maadili yao.”

Mwakilishi huyo wa Bunge la Nepal, huku akieleza mshangao wake kuhusu nafasi na hadhi ya Bibi Fatimah Zahra (as) katika Uislamu alisisitiza kuwa; hapo awali hakuwa na ufahamu kuhusu uwepo wa shakhsia kubwa na mashuhuri kama hii miongoni mwa wanawake wa Kiislamu.

Katika sehemu nyingine ya hafla hiyo, Kalim Arefi, mmoja wa wanazuoni wa Ahlus-Sunna, alizungumzia fadhila za kimaadili na ukarimu wa Bibi Fatimah Zahra (as).

Yakub Ansari, mmoja wa wanasiasa mashuhuri wa Ahlus-Sunna na aliyewahi kuwa mwakilishi katika Bunge la Jimbo, naye huku akizungumzia umuhimu wa kuandaa mikutano ya aina hiyo alisema kuwa; hadi sasa wanazuoni wa Ahlus-Sunna hawajawahi kuandaa kongamano lenye mada hii na linalohusiana na shakhsia hii tukufu.

Sayyid Ali Baqir Abidi, mwanafikra wa Kishia na mmoja wa wageni wa hafla hiyo, ambaye alishiriki katika kongamano hilo akitokea katika mji wa Alipur, Bengaluru, nchini India, naye alizungumzia fadhila na sifa mbalimbali za kipekee za Bibi Fatimah Zahra (as).

Yogi Chandra Nath Maharaj, mmoja wa viongozi wa kidini wa Wahindu nchini Nepal, naye akizungumzia nafasi na hadhi ya juu ya Bibi Fatimah Zahra (as), alisema: “Waislamu hawana haja ya kutafuta kielelezo kingine, kwani shakhsia ya Bibi Fatimah Zahra (as) ni mfano kamili unaojumuisha sifa zote tukufu na fadhila zote za kimaadili.”

Kufanyika hafla hii kwa ushiriki wa wafuasi wa Kiislamu na dini ya Kihindu kulidhihirisha uwezo mkubwa uliomo katika mwenendo wa Bibi Fatimah Zahra (as) wa kuimarisha mazungumzo baina ya madhehebu na dini mbalimbali, kueneza fadhila za kimaadili na kupanua utamaduni wa amani na kuishi pamoja kwa amani ndani ya jamii ya Nepal.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha