Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Hawza kutoka Tehran, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Muhammad Jawad Haj Ali Akbari, katika hotuba za Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran, alianza kwa kuwataka waumini wanaoswali kuzingatia uchamungu, akasema: Katika mijadala yetu iliyopita, tulichunguza nafasi ya maisha yenye kujisitiri na kujilinda na maovu katika maisha ya mtu binafsi. Tulieleza kwamba kujichumga na kujilinda na maovu ni msingi, nguzo na asili ya kuinuka kwa utu wa mwanadamu katika safari ya ukamilifu wa kiimani.
Mwanadamu anapoweza kudhibiti na kuyadhibiti matamanio ya nafsi yake pamoja na mielekeo yake ya kinyama, hujiandalia mazingira ya kufikia tunu nyingine za kibinadamu na za Kiungu, pamoja na fadhila za kimaadili.
Akizungumzia juhudi za kishetani za kuwachafua wanadamu na kuangamiza fadhila za kimaadili, alifafanua: Sababu ya mipango ya kishetani iliyobuniwa tangu mwanzo wa uumbaji hadi leo kwa lengo la kuwachafua watu, kuwaangusha na kuteketeza fadhila zilizomo ndani yao, nayo inaweza kueleweka kupitia suala hili.
Mhimili wa pili wa mijadala kuhusu maisha yenye kujisitiri na kujilinda na maovu ni nafasi yake katika kujenga, kuimarisha na kuinua familia. Familia ndiyo chembe msingi ya jamii na kituo cha malezi ya watoto wa Adam. Uislamu wetu mtukufu umeipa taasisi hii umuhimu wa pekee katika kuilinda na kuiimarisha.
Katika upande mwengine wa hotuba yake, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Haj Ali Akbari akielezea mapambano kati ya Iran na Marekani alifafanua: Mapambano ya Marekani dhidi ya taifa la Iran hayakomei katika miaka ya 1343, 1357 na 1358 Hijria Shamsia. Jambo hili lilianza tangu mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 28 Mordad 1332, na kwa kipindi cha takribani miaka 70, Marekani imekuwa ikiendelea kupanga njama dhidi ya taifa la Iran.
Firauni alikuwa mfano wa kujiona bora kuliko wengine; alijiona kuwa yuko juu ya watu wote na alitarajia wengine wawe chini ya mamlaka yake. Leo hii, Marekani nayo inafanya vivyo hivyo, kwani inataka mataifa yote yanyenyekee mbele ya matakwa yake.
Kama ambavyo Firauni alikuwa alama ya ukatili, unyama, kuwadharau wengine na udanganyifu, ndivyo ambavyo leo sifa hizi zinavyoonekana katika mwenendo wa ubeberu wa dunia.
Firauni alikuwa akibadilisha nafasi za shahidi na muuaji, pamoja na wanyonge na wenye kujiona wakuu. Kupitia udanganyifu wake, alijitambulisha kuwa ndiye mwokozi wa watu, ilhali leo hii pia tunashuhudia mwenendo kama huo kutoka kwa Firauni wa zama hizi, yaani Marekani.
Alisisitiza: Tangu mwanzo, Wamarekani walikuwa na lengo la kuimeza Iran, lakini walikabiliwa na upinzani wa kitaifa wa wananchi wa Iran. Orodha ya uhalifu wa Marekani dhidi ya taifa la Iran, kuanzia mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 28 Mordad 1332 hadi leo, ni ndefu sana. Baadhi ya uhalifu huo ulitekelezwa moja kwa moja, na sehemu kubwa zaidi ilitekelezwa kwa njia zisizo za moja kwa moja, kupitia utawala wa Pahlavi, Saddam na vibaraka wao.
Baada ya kuchukua hatua zisizo za moja kwa moja kwa miaka mingi, Marekani ilianza hatua kwa hatua kuonesha sura yake halisi, hususan kuanzia tukio la kuuawa kishahidi kwa Jenerali Qasem Suleimani. Tangu wakati huo, ilianza kuingia moja kwa moja katika uwanja wa mapambano.
Uwepo wa moja kwa moja wa Marekani katika makabiliano dhidi ya taifa la Iran si ishara ya nguvu, bali unaonesha udhaifu na hali yake ya kukata tamaa, hii ni kwa sababu iliposhindwa kufikia matokeo iliyokuwa imeyapanga katika mipango yake, iliamua kutumia hatua ya mwisho na kuingia moja kwa moja katika uwanja wa mapambano.
Imamu wa muda wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran, akirejelea ahadi za Mwenyezi Mungu kuhusu kuwasaidia Waumini dhidi ya maadui zao, alisisitiza: Taifa la Iran limekuwa likikabiliwa na mwenendo wa kinyama wa ubeberu, lakini kwa tawfiki ya Mwenyezi Mungu litapata msaada na nusura Yake. Leo hii, tunaweza kuona dalili za kushindwa, kukata tamaa na kutokuwa na uwezo kwa ubeberu wa dunia unaoongozwa na Marekani na kushirikiana na utawala wa Kizayuni.
Katika kisa cha Nabii Ibrahim (as) na Nabii Ismail (as), pamoja na mapambano yao dhidi ya vishawishi vya Shetani, Shetani alijidhihirisha waziwazi pale aliposhindwa kuwahadaa Nabii Ibrahim (as) na Nabii Ismail (as). Watukufu hao wawili walikabiliana naye kwa kumrushia mawe. Hata leo, taifa la Iran linaendelea kumrushia Shetani mawe.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Haj Ali Akbari, akizungumzia maombi ya Marekani ya kufanya mazungumzo, kutuma barua na kuwatuma wapatanishi, alisisitiza: Leo hii, maadui wanaomba kufanya mazungumzo, wanaandika barua na kutuma wapatanishi, lakini taifa la Iran halitadanganika, hii ni kwa sababu uzoefu umeonesha kwamba Wamarekani wanapozungumzia mazungumzo na kutuma ujumbe, huenda kukawa na hatari na njama nzito zaidi kuliko wakati wanapotishia kuanzisha vita.
Katika mazingira haya, ni jambo la lazima kuwa macho dhidi ya hatua na mienendo ya adui. Majeshi yetu yako tayari kwa mapambano, huku wananchi nao wakiwa hawaondoki katika viwanja na maeneo ya mikusanyiko wakati wa usiku. Hii ni kwa sababu wamefikia utambuzi wa ukweli kwamba mojawapo ya nguzo kuu za nguvu ya taifa la Iran ni uwepo huu wa wananchi uliojaa nuru na unaoendelea bila kukoma.
Aliendelea kusema: Wananchi, kwa kusimama imara na kuendelea kuwepo kwao katika medani, Inshaallah, kwa tawfiki ya Mwenyezi Mungu, watauvunja uti wa mgongo wa ubeberu wa dunia katika hatua hii.
Leo hii, ndani ya nchi, kuna umoja na mshikamano chini ya bendera ya Uongozi Mkuu. Jambo hili linaonekana miongoni mwa wananchi na viongozi pia. Kwa upande mwingine, kambi ya adui imekumbwa na machafuko, kusambaratika na hali ya kukata tamaa.
Imamu wa muda wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran, akirejelea misimamo yake ya awali kuhusu masharti ya Iran kwa ajili ya makubaliano yoyote, alisema: Kauli ya taifa la Iran iko wazi. Sisi tumetaja masharti saba, na upande wa pili hauna budi kuyatekeleza, hakuna njia nyingine.
Alirejelea pia miitikio iliyojitokeza kufuatia kuibuliwa suala la kutafakari upya fundisho la nyuklia la nchi, akakumbusha: Katika Swala ya Ijumaa iliyopita, tuliibua suala hili kwa kuuliza: Kwa nini tusitafakari upya fundisho letu la nyuklia?
Madai haya si mwitikio wa haraka wala wa kihisia, bali ni matokeo ya ukomavu na mwamko wa kitaifa. Maadui wamekanyaga mipaka yote myekundu ya taifa la Iran, wamemuua kishahidi Imam wetu, na hawajazingatia ahadi wala mikataba yao.
Taifa la Iran, katika kipindi cha miaka iliyopita, limepata uzoefu mchungu kutokana na mwenendo wa upande wa pili. Kwa sasa, likiwa na ufahamu na utambuzi mpana, limeibua suala la kutafakari upya fundisho la nyuklia kama mojawapo ya maeneo ya kuimarisha uwezo wa kuzuia mashambulizi na kuhakikisha usalama wa taifa.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Haj Ali Akbari, akieleza kwamba madai haya yana mizizi yake katika haki ya taifa la Iran kuishi maisha yenye heshima na utukufu, alifafanua: Baadhi ya watu walikasirishwa na kuibuliwa suala hili, lakini hili ni hitaji la taifa la Iran, na halipaswi kuhusishwa na kundi fulani maalumu pekee.
Hata kabla ya hapo, katika baadhi ya tafiti za maoni ya wananchi, zaidi ya asilimia 70 ya watu walikuwa wakitaka kufanyiwa marekebisho katika fundisho la nyuklia. Hata hivyo, baada ya suala hili kuibuliwa, kulitokea wimbi la maombi na mwitikio chanya kutoka kwa makundi mbalimbali ya wananchi, yakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu, wanafunzi wa shule, maprofesa wa vyuo vikuu, wasomi na wataalamu, pamoja na wafanyabiashara na wanachama wa vyama mbalimbali vya kitaaluma.
Leo hii, tunakabiliwa na hitaji la kitaifa, tunatumaini kwamba wasomi na wataalamu wa masuala haya watafanya utafiti na uchunguzi kuhusu suala hili, na kuwasilisha mapendekezo na mipango yao.
Viongozi na maafisa wanaohusika wanapaswa pia kufanya uchunguzi wa ziada, ili mapendekezo hayo yawasilishwe mbele ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi.
Imamu wa muda wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran alisisitiza: Hatimaye, uamuzi wowote ambao Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi atauona unafaa, sisi tutaufuata, na sote tupo chini ya bendera yake. Hata hivyo, wakati huohuo ni lazima kuzingatia pia hitaji na matarajio haya ambayo yamejengeka katika kiwango cha jamii.
Maoni yako