Jumapili 27 Septemba 2026 - 14:35
Mtu anayekanusha Wilayatul-Faqih hakunufaika kabisa na elimu ya fiqhi/ Wananchi wa Iran, kusimama kidete mbele ya madola makubwa ni dhihirisho la neema ya Mwenyezi Mungu

Hawza/ Ayatullah al-Udhma Jawadi Amuli, huku akizungumzia msimamo thabiti wa wananchi wa Iran mbele ya madola vamizi, amesema: “Madola mawili makubwa yalifanya mashambulizi, lakini yalidhalilishwa na kushindwa; jambo hili si la kubembeleza wala kufunikwa kwa maneno. Walivamia, lakini kwa kusimama kidete watoto, ndugu na wananchi wenyewe, walirudi nyuma na kushindwa.”

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah al-Udhma Jawadi Amuli, katika kikao cha kwanza cha darsa yake ya fiqhi ya kiwango cha juu (Dars Kharij) kwa mwaka mpya wa masomo, huku akirejelea kuanza tafiti ya hudud na diyat, alitoa maelezo ya jumla kuhusu “mfumo wa Kiislamu” na kusema: Katika utafiti wa mahakama na ushahidi ilielezwa kwamba, ikiwa kutatokea hitilafu kuhusu haki, basi suala hilo hupelekwa mahakamani ili kubainika haki iko upande wa nani. Mwenye haki akipata haki yake, hakuna tatizo linalobaki, lakini ikiwa mtu hatatoa haki au hukumu miongoni mwa hukumu za Mwenyezi Mungu haitatekelezwa, au haki za Mwenyezi Mungu na za watu zikapotezwa, hapo ndipo masuala ya hudud na kuaziriwa upande mmoja, kisasi upande mwingine na diyat upande wa tatu yanapojitokeza. Hivi ni vitabu vitatu na milango mitatu tofauti, na ingawa vina mambo ya pamoja, kielimu kila moja ni tofauti na jingine, kitu kinachoviunganisha vyote ni suala la nidhamu ya jamii.

Katika zama za ghaiba, ni nani anayesimamia utekelezaji wa hukumu za Mwenyezi Mungu?

Akiuliza swali kwamba katika mfumo wa Uimamu na Umma, utekelezaji wa hukumu na uanzishaji wa utaratibu wa kijamii uko mikononi mwa nani, alisema: Suala kuu katika mfumo wa Uimamu na Umma ni kwamba ni nani anayepaswa kutekeleza hukumu za Mwenyezi Mungu. Katika zama za uwepo wa Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) na baada yake Maimamu Maasumu (a.s.), wao ndio waliokuwa na jukumu la kutekeleza mambo haya, na katika hilo hakuna utafiti. Lakini ni lazima ibainike kwamba katika zama za ghaiba hali ikoje, ili ijulikane kuwa jamii ina mfumo, utaratibu na hesabu.

Akirejelea mtazamo unaosema kuwa utekelezaji wa baadhi ya mambo katika zama za ghaiba ni wajibu wa kijamii (wajib kifai) na uko mikononi mwa watu wenyewe, alisema: Suala kuu katika zama za ghaiba ni kwamba je, Mtume na Maimamu (a.s.) waliwateua watu maalumu kwa ajili ya kipindi hiki au la? Ikiwa watu wenyewe watachukua jukumu hili bila mwongozo uliowekwa, jambo hilo litasababisha ombwe na kuanzisha machafuko na ukosefu wa nidhamu.

Akili ina uwezo wa kujadiliana mbele ya Mwenyezi Mungu

Ayatullah al-Udhma Jawadi Amuli, huku akiendelea kusisitiza nafasi ya akili katika utafiti huu, alirejelea aya za mwisho za Suratul Nisaa na kuongeza:

﴿رُّسُلًا مُّبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى اللَّهِ حُجَّةٌ بَعْدَ الرُّسُلِ وَكَانَ اللَّهُ عَزِيزًا حَكِيمًا﴾

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: Tumewatuma Mitume ili watu wasiwe na hoja dhidi ya Mwenyezi Mungu baada ya kuja kwa Mitume.
 (Suratu Nisaa: 165)

Alibainisha kwamba aya hii ni miongoni mwa aya muhimu sana za Qur’ani Tukufu na kusema: Mwenyezi Mungu anasema kwamba lau asingetuma Mitume, watu wangeweza kutoa hoja mbele Yake na kusema: “Wewe uliyetuumba, kwa nini hukututumia waongozaji?”

Akirejelea neno “baada” lililotajwa katika aya hiyo, alisema: Neno hili linaonesha ukomo maalumu; yaani kabla ya Mitume, akili inaweza kuuliza kwa nini Mitume hawakutumika, lakini baada ya kutumwa kwao, akili haina hoja hiyo tena, kwa sababu hoja imekamilika.

Alisisitiza: Akili yenye uwezo wa kutoa hoja mbele ya Mwenyezi Mungu inapaswa kutambuliwa, kuheshimiwa na kufuatwa hukumu zake; kwa sababu akili hii yenye nguvu inafahamu kwamba jamii ya wanadamu, ili kuondoa migogoro na kuzuia dhulma, inahitaji nidhamu na mwongozo.

Katika zama za ghaiba, hoja ya kiakili kuhusu ulazima wa mwongozo bado ipo

Akitoa swali kwamba je, hoja hii ya kiakili inahusu tu zama za uwepo wa Mtume au Imam, alisema: Wakati Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) yupo au Imam Maasumu (a.s.) yupo, hoja ipo. Lakini ikiwa hakuna Mtume wala Imam Maasumu, na pia hakuna mtu aliyeteuliwa na wao kusimamia majukumu hayo, basi hoja hii ya kiakili itaendelea kuwepo.

Akirejelea hoja za Sahib al-Jawahir, alisema: Watu hawawezi mmoja mmoja kubeba majukumu haya yote, lakini ni haki yao kumuuliza Mwenyezi Mungu kwamba katika zama za ghaiba wamrejee nani; hii ni haki ya mja kwa Mola wake. Ikiwa katika zama za ghaiba dini haijabainisha wajibu wowote, akili inaweza kusema: “Ewe Mola! Umewaacha watu hawa mikononi mwa nani? Je, hakuna mfumo wala hesabu?”

Aliendelea kusema: Msingi wa hoja ni kwamba watu katika zama za uwepo wanamuhitaji Maasumu, na ikiwa kufikiwa Maasumu haitawezekana, katika zama za ghaiba wanamuhitaji mtu asiye Maasumu lakini anayesimamia mambo kwa idhini ya Maasumu, ikiwa watu wataachwa bila mwongozo, basi hoja ya ulazima wa kutumwa mwongozo na hoja ya Mwenyezi Mungu itapoteza maana yake.

Hoja ya Sahib al-Jawahir kuhusu Wilayat al-Faqih

Ayatullah al-Udhma Jawadi Amuli, akiendelea na utafiti wa Wilayat al-Faqih na uwakilishi wa mafaqihi katika zama za ghaiba, alirejelea tawqi tukufu ya Imam wa Zama (a.f.) kwa Sheikh Mufid na pia tafiti za marehemu Sahib al-Jawahir, na kuongeza: Sahib al-Jawahir katika juzuu ya 21 ya kitabu Jawahir al-Kalam, katika utafiti wa Wilayat al-Faqih, alizungumzia ulazima wa kuwepo nidhamu ya mambo ya Mashia katika zama za ghaiba.bAkirejelea maneno ya Sahib al-Jawahir, alisema:

«فَمِنَ الْغَرِيبِ وَسْوَسَةُ بَعْضِ النَّاسِ فِي ذَلِكَ، بَلْ كَأَنَّهُ مَا ذَاقَ مِنْ طَعْمِ الْفِقْهِ شَيْئًا»

Maana ya maneno ya Sahib al-Jawahir ni kwamba mtu anayekanusha Wilayat al-Faqih ni kana kwamba hakunufaika kabisa na fiqhi; kwa sababu suala la uongozi na mamlaka katika zama za ghaiba kwa ajili ya kupanga mambo ya jamii ya Mashia, linatokana na msingi wa tafiti za fiqhi na riwaya zinazohusiana na mtawala, kadhi, hoja na khalifa.

Alisema: Takriban miaka arobaini iliyopita, nilisoma maneno haya ya Sahib al-Jawahir katika mkutano mbele ya wanaokanusha mfumo wa Wilayat al-Faqih na nikasema kwamba maoni ya Sahib al-Jawahir ni kuwa anayekanusha Wilayat al-Faqih ni kana kwamba hakupata kabisa sehemu yoyote ya fiqhi; kwa sababu ikiwa watu peke yao wanatosha kuendesha mfumo wa jamii, basi hoja ya aya ya Suratu Nisaa kuhusu ulazima wa mwongozo na hoja ya Mwenyezi Mungu itakuwa na maana gani?

Mfumo wa Uimamu na Umma lazima ujengwe juu ya ijtihadi, uadilifu na nidhamu

Katika sehemu nyingine ya darsa yake, Ayatullah al-Udhma Jawadi Amuli alisisitiza jukumu la hawza na mafaqihi, akisema: Katika mfumo wa Uimamu na Umma, juhudi zetu zinapaswa kuwa kuelewa kwa usahihi maneno ya Ahlul-Bayt (a.s.) na kuyafikisha kwa usahihi. Wanaosimamia jamii wanapaswa kuwa mafaqihi, wafahamu mambo kwa ijtihadi, watende kwa ijtihadi na watende kwa uadilifu, hiyo ndiyo nidhamu.

Uelewa sahihi wa maarifa ya Ahlul-Bayt (a.s.) ni sharti la kutimia mfumo wa Uimamu na Umma

Akizungumza na wanazuoni na mafaqihi wa hawza, alisema: Jukumu kubwa liko juu ya mabega yenu, na nyinyi mmebeba bendera ya njia hii, kwa mwongozo wenu, wanaume na wanawake watukufu wa Iran wamejifunza kujitetea na kusimama imara, na wamejifunza kuwa na roho ya Zaynab (s.a.) na Hussein (a.s.) kutoka kwenye hawza na wanazuoni.

Kusimama watu mbele ya madola makubwa ni dhihirisho la neema ya Mwenyezi Mungu

Ayatullah al-Udhma Jawadi Amuli, akirejelea kusimama kidete wananchi wa Iran mbele ya madola vamizi, alisema: Madola mawili makubwa yalivamia na yakadhalilishwa; hili si jambo la kubembeleza kwa maneno, walivamia lakini kwa kusimama imara watoto, ndugu na wananchi wenyewe, walirudi nyuma na kushindwa.

Akielekeza fikra kwenye jambo hili, alisema: Je, hii si neema ya Mwenyezi Mungu? Je, muujiza ni jiwe kuzungumza tu? Ikiwa umma wenye mikono mitupu unasimama mbele ya kundi fulani na kupambana nao, je, huu si muujiza na amri ya Mwenyezi Mungu? Nguvu hii imetoka wapi? Nguvu hii inatoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ambaye huwapa wafuasi wa Ahlul-Bayt (a.s.).

Simulizi ya kuhuzunisha ya Ayatullah al-Udhma Jawadi Amuli kuhusu mama mmoja wa Minab

Katika muktadha huo, akirejelea uhalifu na kiburi cha Marekani na Israel, alielezea tukio la Minab na kusema: Mama mmoja katika shule ya Minab alimpeleka mtoto wake shuleni, lakini baadaye akabeba si jozi ya viatu, bali kiatu kimoja tu, akisema: “Sijui mtoto wangu yuko wapi; hakuna athari yoyote iliyobaki ya mwanangu!” Kila ninapokumbuka tukio hili, ni vigumu sana kwangu kulivumilia. Je, hakuna mtu anayepaswa kuwajibika mbele ya mfumo huu? Nani anawajibika?

Kisha alisisitiza kwamba; watu wana haki na pia wana wajibu, na kusema: Watu wote wana haki na wajibu, lakini wanahitaji mwongozo na kiongozi; “Kwanza Mtume, kisha Maimamu (a.s.), halafu manaibu wao.” Huo ndio mfumo.

Kusisitiza jukumu la mafaqihi katika zama za ghaiba na ulazima wa kuelewa kwa usahihi maarifa ya Ahlul-Bayt (a.s.)

Ayatullah al-Udhma Jawadi Amuli alisisitiza: Ni lazima kuzingatia kwamba akili ina uwezo mkubwa kiasi cha kusimama mbele ya Mwenyezi Mungu na kusema: “Uliwaumba watu, kwa nini hukuwatumia waongozaji?” Na Mwenyezi Mungu anasema: Tumewatuma Mitume ili watu wasiwe na hoja dhidi ya Mwenyezi Mungu baada ya kuja kwao.

Katika hitimisho la mazungumzo yake, akirejelea tena nafasi ya mfumo wa Uimamu na Umma, alisisitiza ulazima wa kuelewa kwa usahihi maneno ya Ahlul-Bayt (a.s.), kuyafikisha kwa usahihi, kuiendesha jamii kwa msingi wa ijtihadi na uadilifu, na kuzingatia jukumu la mafaqihi katika zama za ghaiba. Pia aliwaombea wanazuoni na hawza izza, utukufu, fahari na baraka nyingi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha