Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, hivi karibuni kufuatia operesheni iliyofanywa na maafisa wa hisba wa idara ya kuamrisha mema na kukataza maovu ya Taliban magharibi mwa Kabul, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Hussein Dad Sharifi, mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Kishia nchini Afghanistan, alikamatwa kuhusiana na kusimamia kufungwa kwa ndoa ya kisheria ya wanandoa vijana.
Kwa mujibu wa ripoti zilizopokelewa, alipelekwa katika kituo cha polisi cha wilaya ya 18 mjini Kabul na akapigwa, kudhalilishwa na kutukanwa na maafisa hao.
Kufuatia tukio hilo, Hujjatul-Islam Sayyid Isa Husseini Mazari, mkuu wa Kituo cha Tibyan Afghanistan, kupitia taarifa rasmi aliyotoa huku akisisitiza nafasi isiyoweza kufidiwa ya wanazuoni katika kulinda Uislamu na umoja wa taifa, alitangaza kuwa; kumpiga na kumdhalilisha Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sharifi si uvamizi dhidi ya mtu mmoja tu, bali ni kutoheshimu jamii ya wanazuoni na ni kuvunja haki ya wafuasi wa fiqhi ya Jaafari.
Mkuu wa Kituo cha Tibyan alisema: “Kurudiwa kwa aina hii ya vitendo, hasa baada ya nafasi ya fiqhi ya Jaafari kupuuzwa katika mwongozo mpya wa mahakama wa Imarati ya Kiislamu, kumesababisha wasiwasi mkubwa miongoni mwa raia Mashia na kumeandaa mazingira ya kutokea kwa vitendo vya kiholela na vyenye mvutano.”
Husseini Mazari alionya kuwa, kuendelea kwa vitendo vya kiholela na vya upendeleo kama hivi kunaweza kuleta mpasuko mkubwa baina ya jamii ya Kishia na mfumo wa utawala, na kuharibu imani ya wananchi.
Aliongeza kuwa: “Nguzo kuu ya vikosi na maafisa wa Imarati ya Kiislamu wenyewe wametokana na safu za wanazuoni na wanafunzi wa elimu za dini. Kwa hiyo, kumvunjia heshima mwanazuoni mmoja ni kulenga hadhi ya pamoja ya tabaka hili tukufu.” Pia alisisitiza kuwa; kupuuzwa kwa haki za kidini za Mashia na kuwekewa mipaka shughuli zao za kidini kunaweza kuleta athari kubwa za kiusalama na kijamii.
Hujjatul-Islam Husseini Mazari, huku akirejelea uelewa wake kuhusu sera kuu za Imarati ya Kiislamu, alitangaza kuwa; vitendo hivi vibaya vinasababishwa na mitazamo binafsi na uelewa potofu wa baadhi ya maafisa wa ngazi za chini, lakini kuendelea kwa mwenendo huu kunahitaji majibu ya dhati na yenye kujenga imani kutoka kwa nguzo kuu za serikali.
Alipendekeza hatua mbili za haraka na muhimu kwa ajili ya kurekebisha hali hiyo:
1. Kumuomba radhi rasmi Hujjatul-Islam Sharifi na kuirejesha heshima yake, alisema kuwa, kuomba radhi huku ni ishara ya kuwajibika kwa mfumo wa utawala na si kurudi nyuma.
2. Kuwatambua na kuwaadhibu waliohusika katika kumpiga, kumdhalilisha na kumkamata kiholela Hujjatul-Islam Sharifi, ili maafisa wengine wazuiwe kurudia vitendo visivyo vya kisheria.
Mwisho wa taarifa yake, Husseini Mazari alionya kuhusu hali ya maeneo yenye wakazi wa Kishia, hususan magharibi mwa Kabul, na kusisitiza kuwa; sera za uteuzi, ajira na usimamizi wa maafisa wa kiutendaji zinahitaji kufanyiwa mapitio ya msingi.
Aliongeza kusema: “Kuendelea kwa mwenendo wa upendeleo unaokwenda kinyume na usalama na mshikamano kunapoozesha nguvu ya umoja wa taifa, na kunaweza kusababisha kuzuka kwa chuki zilizojificha na pengo lisiloweza kurekebishwa baina ya jamii ya Kishia na utawala.”
Maoni yako