Jumamosi 2 Mei 2026 - 11:22
Ushirikiano wa moyo na udugu ni rasilimali muhimu zaidi kwa umoja wa umma wa Kiislamu

Hawza/ Mmoja wa Mara'ji' wakuu wa Taqlid katika ujumbe wake ulio na anuani isemayo “Umoja wa Umma wa Kiislamu” ameeleza kwamba; mshikamano wa moyo na udugu ndio rasilimali muhimu zaidi kwa umoja wa umma wa Uislamu.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah al-‘Udhma Ja‘far Subhani, miongoni mwa Mara'ji' wakuu wa Taqlid wa Kishia, katika ujumbe wake ulio na anuani isemayo “Umoja wa Umma wa Kiislamu” ameandika: “Udugu wa Kiislamu” ni rasilimali kubwa ya kijamii na kitamaduni ambayo utekelezaji wake hupeleka jamii kuwa salama kiroho na kuheshimika. Kushikamana na msingi huu ni dhamana ya rehema ya Mwenyezi Mungu, afya ya kisaikolojia ya jamii, na kunaimarisha hisia ya uwajibikaji miongoni mwa Waislamu, na huweka msingi wa maendeleo na utukufu wa umma wa Kiislamu.

Kudumu kwa Uislamu na uthabiti wa jamii ya Kiislamu kunategemea utekelezaji wa “udugu” miongoni mwa Waislamu. Msingi huu wa Kiungu, unaotokana na Qur’ani na Sunna, si tu unaimarisha mahusiano ya kihisia na kijamii, bali pia kwa kuleta mshikamano wa moyo na huruma, huifanya jamii iwe imara mbele ya vitisho vya nje na kugeuza matumaini ya maadui kuelekea kukata tamaa.

Umoja na mshikamano wa kijamii ni miongoni mwa mahitaji ya wazi na ya lazima zaidi katika maisha ya mwanadamu; kwa sababu jamii iliyotawanyika na kugawanyika haina nguvu wala athari, lakini kwa kuungana kwa nguvu ndogo ndogo, huzaliwa nguvu kubwa yenye kuleta mabadiliko. Hata hivyo, uzoefu umeonesha kuwa; sababu za nje kama rangi, lugha, historia ya pamoja au ardhi, ingawa zina mchango katika kuunda aina fulani ya umoja, lakini kwa kuwa zinategemea mambo ya kimada na yasiyo ya hiari, haziwezi kuwa dhamana ya umoja wa kudumu. Aina hizi za umoja mara nyingi huwa za muda mfupi, na baada ya kufikiwa malengo ya pamoja, tofauti hujitokeza tena.

Uislamu, kinyume na mitazamo hii, unatoa suluhisho la kina zaidi na la kudumu, nalo ni “umoja juu ya mhimili wa imani na itikadi.” Kwa mujibu wa mtazamo huu, Waislamu katika mwangaza wa kumuamini Mwenyezi Mungu huunganishwa kama viungo vya mwili mmoja na kutekeleza kanuni ya “udugu wa Kiislamu.” Qur’ani Tukufu kwa uwazi inasema: «إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ» na inawaomba Waumini kuhifadhi uhusiano huu wa kindugu na kujitahidi kuurekebisha na kuukuza. Tamko hili linaonyesha aina ya ndani zaidi ya uhusiano wa kibinadamu unaojengwa juu ya kushitikiana katika imani na malengo.

Katika Sunna ya Mtume pia maana hii imefafanuliwa wazi; Mtume wa Uislamu (saww) amewafananisha Waumini na viungo vya mwili mmoja ambapo maumivu ya kiungo kimoja huwathiri wengine pia. Aidha, katika historia ya mwanzo wa Uislamu, mkataba wa udugu miongoni mwa Waislamu ulikuwa sababu kuu ya kuondoka kwa tofauti za kikabila, kitabaka na kitamaduni, na kuundwa kwa umma mmoja. Hii inaonesha kuwa; udugu wa Kiislamu si dhana ya kinadharia tu, bali ni suluhisho la kivitendo katika kuiunda jamii iliyoungana na yenye maendeleo.

Athari na matokeo ya msingi huu muhimu ni mapana sana. Muhimu zaidi ni “mshikamano wa moyo na huruma” unaosababisha mshikamano wa kijamii na harakati ya pamoja ya jamii kuelekea malengo ya Kiungu. Pia “usalama wa pande zote” ni miongoni mwa matokeo yake; kiasi kwamba, uhai mali na kuwaheshimu watu katika jamii ya Kiislamu hutiliwa mkazo. Aidha, roho ya “kujitoa mhanga na kuwajali wengine” huimarishwa miongoni mwa watu, na kila mtu hujiona kuwa na jukumu juu ya matatizo ya wengine. Jamii kama hii kwa kawaida itakuwa mstari wa mbele katika mema na fadhila.

Hata hivyo, maadui wa Uislamu daima wamekuwa wakijaribu kudhoofisha uhusiano huu imara na kwa kuanzisha tofauti za kiitikadi, kisiasa na kikabila, wamejaribu kuvunja umoja wa Waislamu. Kuendelea kwa migogoro katika baadhi ya jamii za Kiislamu ni dalili ya mafanikio ya kiasi katika njama hizi na kupuuzwa kwa kanuni ya udugu wa Kiislamu.

Kwa muhtasari, inaweza kusemwa kuwa: “Udugu wa Kiislamu” ni rasilimali kubwa ya kijamii na kitamaduni ambayo utekelezaji wake huipeleka jamii kukua, na kuwa usalama kiroho na kuheshimika. Kushikamana na msingi huu ni dhamana ya rehema ya Mwenyezi Mungu, afya ya kisaikolojia ya jamii, na kunaimarisha hisia ya uwajibikaji miongoni mwa Waislamu, na huweka msingi wa maendeleo na utukufu wa umma wa Kiislamu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha