Alhamisi 16 Aprili 2026 - 22:40
Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia Pakistan amwandikia barua Ayatullah A‘rafi

Hawza/ Hujjat al-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia Pakistan, katika barua yake alieleza kwamba; damu takatifu ya mashahidi ni dhamana ya kudumu, ustawi na kuenea kwa harakati ya Kiungu, na athari pamoja na baraka zake zitaendelea daima katika historia yote na zitaufanya uso wenye kung’aa wa haki na ukweli kuwa wazi zaidi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjat al-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia Pakistan, katika barua aliyomwandikia Ayatullah A‘rafi alieleza kwamba; damu takatifu ya mashahidi ni dhamana ya kudumu, ustawi na kuenea kwa harakati ya Kiungu, na athari pamoja na baraka zake zitaendelea daima katika historia yote na zitaufanya uso wenye kung’aa wa haki na ukweli kuwa wazi zaidi.

Matini ya barua ni kama ifuatavyo:

Kwa heshima kubwa mbele ya Ayatullah Hajj Sheikh Ali-Reza A‘rafi, Msimamizi mtukufu wa Hawza nchini Iran

السلام علیکم و رحمة الله وبرکاته

Kwa huzuni kubwa na masikitiko, alfajiri ya tarehe 28 Februari 2026, habari ya kuhuzunisha na yenye majonzi makubwa ya kuuawa kishahidi Kiongozi Mkuu iliizamisha mioyo katika huzuni nzito na ya kuumiza; kwa namna ambayo kwa muda mfupi hali ya mshangao na kutoamini ilitanda juu ya nafsi na nyoyo, na ndimi zikashindwa kuelezea hali hiyo. Hata hivyo, kwa kushikamana na daraja ya ridhaa na kujisalimisha mbele ya mapenzi ya hekima ya Mwenyezi Mungu, tulijitahidi kuziita nyoyo katika subira njema na utulivu.

Kufuatia msiba huu mkubwa, wimbi la kuomboleza na kutoa pole lilienea miongoni mwa Waumini na wapenzi kote Pakistan, ambalo bado linaendelea kwa hamasa na ikhlasi. Bila shaka, kitendo cha kinyama na cha kihalifu cha Marekani na Uzayuni ni uhalifu usiosameheka na doa la milele katika rekodi ya wahusika wake, ambalo halina aina yoyote ya uhalalisho.

Kufuatia janga hili, msururu wa mashambulizi ya kivamizi ya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulianza; lakini taifa la Kiirani lililojaa imani, lenye utambuzi na lenye heshima, kwa uthabiti wa kusifiwa na azma thabiti, limesimama dhidi ya vita hivi vilivyolazimishwa na kwa uwepo mkubwa na wenye hamasa katika uwanja, limeonesha uungaji mkono wake kamili kwa mfumo mtakatifu wa Kiislamu. Mikusanyiko mikubwa ya wananchi katika barabara na viwanja ni taswira wazi ya uaminifu na mwamko huu, ambao bado unaendelea na umeshinda njama ovu za ubeberu wa kimataifa na maadui wa mapinduzi.

Kwa upande mwingine, vikosi vya kijeshi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kwa roho iliyojaa kujitolea, vimetetea Uislamu na taifa katika nyanja zote na kama ukuta imara, vimesimama dhidi ya mashambulizi ya adui; ukweli ambao umefanya marafiki na maadui kukiri.

Waumini wa Pakistan, katika kulinda mfumo wa Kiislamu, daima waliinua mikono yao kwa kuomba dua na mbele ya Mwenyezi Mungu, na kuiombea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iweze kudumu.

Bila shaka, vita hivi vilivyolazimishwa tangia mwanzo wake hadi sasa vimesababisha hasara kubwa za maisha na mali kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; kwa namna ambayo baadhi ya makamanda wakuu na shakhsia za kiwango cha juu wameitoa roho zao katika njia ya kuinua mfumo huu wa Kiungu, na kujitolea kwa taifa adhimu la Iran pia kumeonekana wazi mbele ya Umma wa Kiislamu. Roho hii ya kujitolea na jihadi si tu kwamba haijapungua, bali inaongezeka siku baada ya siku na imekuwa rasilimali ya kudumu kwa ajili ya kuendeleza njia yenye nuru ya mapinduzi.

Pamoja na hasara za kibinadamu, miundombinu muhimu ya nchi pia imelengwa na mashambulizi ya adui, na hasara kubwa zimepatikana katika vituo visivyo vya kijeshi, hospitali, viwanja vya ndege, viwanda, maeneo ya michezo, barabara kuu, reli, madaraja, shule na taasisi nyingine muhimu.

Tangu mwanzo wa mashambulizi haya, sisi kupitia vyombo vya habari vya ndani vya Pakistan na pia majukwaa na vyombo vya kimataifa, kwa namna endelevu tumelaani uhalifu huu. Vilevile kote nchini, mikusanyiko na maandamano ya wananchi kwa ajili ya kulaani janga hili vimefanyika, na katika programu mbalimbali tumepaza sauti ulimwenguni kote. Aidha, mchakato wa kukusanya misaada ya kifedha kwa waathirika wa vita bado unaendelea, na misaada hii inawasilishwa kupitia njia rasmi kwa ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Islamabad.

Hali ya huzuni na maombolezo bado imetanda katika nyoyo, na kupona kwa jeraha hili kubwa kunahitaji muda; hata hivyo, tunaamini kwa yakini kwamba kuuwawa kishahidi kiongozi mwenye hekima, wafuasi wake waaminifu na Waumini wengine, kutasababisha kuimarika na kukomaa zaidi kwa misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu. Bila shaka, damu takatifu ya mashahidi ni dhamana ya kudumu, ustawi na kuenea kwa harakati hii ya Kiungu, na athari pamoja na baraka zake zitaendelea milele katika historia na zitaufanya uso wenye kung’aa wa haki na ukweli kuwa wazi zaidi.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu akujaalie mafanikio yanayoendelea kuongezeka kwenu.

والسلام علیکم ورحمة الله و برکاته

Sayyid Sajid Ali Naqvi
Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia Pakistan

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha