Jumanne 17 Februari 2026 - 16:30
Kuchomwa Husseinia nchini India ni tahadhari kubwa katika mshikamano wa kidini

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Safi Haider Zaidi, Katibu Mkuu wa Tanzim al-Makatib Lucknow, katika taarifa rasmi amelaani kuchomwa moto kwa Husseiniya katika mji wa Farrukhabad, India, akilitaja tukio hilo kuwa pigo kwa umoja wa kitaifa na utamaduni wa kuishi pamoja kwa dini tofauti, na akataka hatua za haraka na madhubuti zichukuliwe dhidi ya wahusika.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, katika taarifa hiyo imeelezwa kuwa, India ni nchi kubwa yenye historia ndefu ambayo daima imejulikana kama alama ya kuishi kwa amani kati ya dini mbalimbali, kwa kuzingatia kanuni ya “ishi na uwaache wengine waishi” pamoja na uhuru wa kidini. Hivyo, kuchomwa moto kwa Husseiniya huko Farrukhabad ni tukio la kusikitisha na la kuhuzunisha sana ambalo limeathiri umoja na mshikamano wa kijamii.

Maswali kuhusu usalama katika jimbo la Uttar Pradesh

Aliendelea kusema kuwa; tukio hilo limeibua maswali mazito kuhusu madai ya kuwepo kwa usalama na utulivu wa umma katika jimbo la Uttar Pradesh, India, na limekuwa changamoto kubwa kwa vyombo vya utendaji na usalama. Aidha, alieleza kuwa kitendo hicho kimeumiza sana hisia za kidini za jamii ya Kishia na kusababisha wasiwasi na hofu miongoni mwao.

Nafasi ya maombolezo ya Imam Hussein nchini India

Hujjatul-Islam Sayyid Safi Haider Zaidi, pia alizungumzia nafasi ya maombolezo ya Imam Hussein (a.s.) nchini India, akisema kuwa; mbali na nchi zenye idadi kubwa ya Mashia, India ni miongoni mwa nchi chache ambapo ibada na maadhimisho ya maombolezo ya Imam Hussein hufanyika kwa uhuru na kwa hadhi kubwa, na kwamba idadi kubwa ya wafuasi wa dini nyingine pia hushiriki katika hafla hizo.

Alitaja pia mila ya “Husseini Brahmins” kuwa ni ishara wazi ya utamaduni wa pamoja na kuishi kwa amani kati ya dini katika jamii ya India.

Wito wa kuchukuliwa hatua za kisheria

Mwishoni, kiongozi huyo wa kidini aliwataka viongozi husika kuchukua hatua za haraka kwa kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hilo na kuwaadhibu kwa mujibu wa sheria. Alionyesha matumaini kuwa, serikali ya jimbo la Uttar Pradesh itachukua hatua za haraka kuhakikisha haki inatendeka na mshikamano wa kijamii unalindwa.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha