Jumanne 17 Februari 2026 - 12:30
Harakati za muqawama zimethibitisha uhalali wake kupitia vitendo vyake

Hawza/ “Jumuiya ya Vituo vya Utamaduni vya Imam Ruhollah Khomeini nchini Lebanon” kutokana na mnasaba wa maadhimisho ya miaka 47 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na katika mfumo wa “Wiki ya Makamanda Mashahidi”, imeandaa mkutano wa kitamaduni na kielimu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, “Jumuiya ya Vituo vya Utamaduni vya Imam Khomeini (r.a.) nchini Lebanon” iliandaa mkutano huo katika mji wa Qana kusini mwa Lebanon, ambapo Hujjatul-Islam Sheikh Akram Barakat, Naibu wa Masuala ya Utamaduni wa Hezbollah, alihutubia mbele ya kundi la wanazuoni wa dini, wanaharakati, watu mashuhuri na wakazi wa eneo hilo.

Programu ilianza kwa usomaji wa aya za Qur’ani Tukufu, kisha Sheikh Barakat alisema katika hotuba yake: Harakati za muqawama zimethibitisha uhalali wake kwa vitendo, na zimeweza kuleta matokeo ambayo wengine hata hawakuyatarajia; mwaka 2000 ziliweza kuikomboa ardhi, na mwaka 2006 pia zilipata mafanikio makubwa kutokana na subira na uimara wake.

Akirejelea kauli ya mmoja wa wasomi wa Jordan katika kipindi hicho, aliongeza kuwa: Ilisemekana kwamba mapambano yaliweza kufufua roho iliyovunjika ya watu na kushinda hisia ya kushindwa waliyoishi nayo. Mtazamo na utendaji huu ulipelekea roho ya muqawama kusambaa katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu, jambo lililokuwa tishio kubwa kwa maslahi ya Marekani na utawala wa Kizayuni.

Sheikh Barakat aliendelea kusema: Mbele ya ukweli huu, mkondo mwingine ulianzishwa ili kuharibu sura ya muqawama kwa njia ya kihistoria na ya kimkakati; kampeni za kuchochea fitina za kimadhehebu kati ya Shia na Sunni zilianzishwa, na tuhuma kama kufuata miradi ya Iran na nyinginezo zikazushwa. Mwaka 2023, wakati Ghaza ilipoinuka tena, watu wengi waliathiriwa na propaganda za kupotosha zilizodai kuwa dunia — hata Waislamu — wamewaacha Wapalestina; kiasi kwamba baadhi walisema Waarabu na Waislamu wameiacha Palestina. Ilhali kiini cha suala hilo ni haki na wajibu wa kumtetea mwenye kudhulumiwa, si mgogoro wa kimadhehebu.

Mjumbe huyo wa Hizbullah aliongeza: Baadhi wanaamini kuwa wale waliosimama pamoja na Palestina ni wabeba mradi unaoamini umoja wa Umma wa Kiislamu, mshikamano wa kijamii na fikra za Imam Ruhollah Khomeini (r.a.), pamoja na dhana ya kusubiri kwa kujenga na kuondoa vikwazo katika njia ya uadilifu. Walisimama juu ya itikadi inayochukulia kumtetea mwenye kudhulumiwa kuwa wajibu wa kidini na kimaadili. Ndani ya mtazamo huu kuna dhana ya uongozi na utawala unaojengwa juu ya misingi na maadili ya Kiislamu, si pragmatismu inayohalalisha kila njia ili kufikia lengo.

Aliendelea kusema: Katika mtazamo huu, siasa hazitenganishwi na maadili, na lengo haliwezi kufikiwa kwa kutumia njia zinazopingana na maadili. Ndiyo maana daima hurejelewa mwenendo wa Mtume Mtukufu (s.a.w.w) na Amirul-Muuminina Ali (a.s.), ili kukumbusha kuwa, kushikamana na misingi kulikuwa muhimu zaidi kuliko ushindi wa haraka wa kijeshi. Inasimuliwa kuwa waliepuka mbinu ambazo zingetoa ushindi wa haraka lakini zikawa kinyume cha maadili, kwa sababu katika mantiki yao, lengo halihalalishi njia.

Sheikh Barakat alisisitiza: Kwa mtazamo huo, matumizi ya silaha zinazosababisha mauaji ya kiholela na kuathiri watu wasio na hatia, hasa wanawake na watoto, hayakubaliki, kwa kuwa yanapingana na kanuni ya kuheshimu uhai wa watu wasio na ulinzi. Kiini cha fikra hii ni kwamba; uongozi wa kweli hata katika mazingira magumu zaidi hulinda dini na maadili na huepuka hila na usaliti, hata kama kwa nje kungekuwa na manufaa ya kijeshi.

Akiashiria mwenendo wa Magharibi alisema: Hotuba ya Magharibi kuhusu uhuru na maadili imeporomoka mbele ya utendaji wao halisi, na kuibuka kwa watu kama Donald Trump kumeonesha sura iliyofichika ya siasa za Magharibi ambayo sasa imekuwa wazi.

Sheikh Barakat alihitimisha kwa kusema: Mkabala huu si vita ya kijeshi au kisiasa tu, bali ni mapambano ya mitazamo na maadili; kati ya wale wanaounganisha siasa na maadili pamoja na misingi ya dini, na wale wanaokubali mantiki ya maslahi na pragmatismu hata kwa gharama ya kuharibu maadili.

Mwishoni alisema: Leo tunazungumzia waliodhulumiwa wa Ghaza, na tunapaswa kujiuliza: msimamo wetu ni upi? Je, tutabaki bila upande au tutatekeleza wajibu wetu wa Kiislamu? Je, kutokuegemea upande wowote kunaendana na dini na maadili? Kama tusingesimama, huenda tungepata hasara ndogo ya mali, lakini tungepata hasara kubwa zaidi — kupoteza heshima, utu na maana ya maisha. Kilichotokea ni kwamba, tulilinda heshima yetu na tunaendelea kutembea kifua mbele, kwa sababu tulimtetea mwenye kudhulumiwa na tukabaki upande wa haki; na msimamo huu haukuwa tu kuzuia hasara, bali ulikuwa utangulizi wa ushindi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha