Jumatatu 9 Februari 2026 - 22:30
Zaidi ya bandari 20 za Mediterania zagoma kwa ajili ya kuonesha mshikamano na Palestina

Hawza/ Wafanyakazi katika gati za Bahari ya Mediterania walianzisha mgomo mkubwa, na kusimamisha shughuli katika zaidi ya bandari 20 kupinga mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina yanayofanywa na utawala wa Israel huko Ghaza, pamoja na ubinafsishaji na kugeuzwa miundombinu ya bandari kuwa ya kijeshi kwa ajili ya ushirikiano wa kijeshi na Israel.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tajama cha Shirika la Habari la Hawza, viongozi wa vyama vya wafanyakazi walielezea hatua hiyo kuwa ni matokeo ya mshikamano wa muda mrefu wa wafanyakazi wa bandari na Palestina, pamoja na mapambano yao kwa ajili ya mazingira ya kazi yenye heshima katika nchi zao.

Maandamano hayo makubwa yalianzia bandari katika nchi za Ugiriki, Uturuki na eneo la Basque, na kuwakusanya mamia ya wafanyakazi wa bandari chini ya ujumbe usemao: “Dhidi ya mauaji ya kimbari na kwa mshikamano na Palestina.”

Nchini Ugiriki, wafanyakazi wa bandari pia waliashiria hali ngumu za maisha, huku wakikosoa uwekezaji mkubwa wa Ulaya katika kujizatiti kijeshi upya pamoja na Israel, kama sababu za mgomo huo.

Damianos Voudigaris wa chama cha wafanyakazi cha Ugiriki alisema katika hotuba yake: “Hatutakubali kufanya kazi bila ujira. Maendeleo ya jamii yanapaswa kumaanisha kurudi nyumbani kwa furaha baada ya zamu ya kazi. Bandari ni mahali pa kazi, si vita. Bandari ni mahali pa kutoa jasho, si pa kutuma na kupakia silaha kwa ajili ya kumwaga damu.”

Nchi ya Italia pia ilishuhudia migomo iliyoratibiwa katika bandari zaidi ya kumi, iliyohusisha wafanyakazi wa bandari, wafanyakazi wa ofisi za bandari, pamoja na wanafunzi na wananchi. Washiriki katika mgomo huo mkubwa walisema: “Bandari ni mwanzo tu wa mgomo wetu! Leo bandari, kesho sekta nzima ya usafirishaji wa mizigo, na kisha wafanyakazi wote watajiunga.”

Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Wafanyakazi lilitoa tamko likithibitisha mshikamano mkubwa wa wanachama wa mgomo huo, na likatambua rasmi bango lenye ujumbe usemao: “Wafanyakazi wa bandari hawafanyi kazi kwa ajili ya vita.”

Mgomo huo mkubwa ulifanyika siku moja baada ya meli za kimataifa za “Sumud” kutangaza kuwa ujumbe mpya wa misaada ya kiraia kwenda Ghaza utaanza safari tarehe 29 Machi.

Chanzo: Cradle.com

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha