Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, mikusanyiko ya tafiti za Mahdawiyya wenye anuani isemayi “Kuielekea Jamii Bora”, kwa lengo la kusambaza mafundisho na maarifa yanayohusiana na Imam wa Zama (a.s.), inawasilishwa kwenu ninyi wasomi waheshimiwa.
Athari za mikondo potofu katika utafiti wa Mahdawiyya
Licha ya uadui mwingi unaoyakabili mafundisho ya dini, kuzingatiwa itikadi ya Mahdawiyya kunazidi kuongezeka siku baada ya siku. Kuongezeka kwa hamu na hisia ya haja katika nyanja za kiakili na kihisia, pamoja na kuwa ni jambo lenye baraka kubwa, hata hivyo kumesababisha kwamba sambamba na mafundisho asilia na ya kina, mielekeo potofu nayo imejitokeza na kwa muda mfupi imevutia baadhi ya watu wasio na uelewa wa kutosha au wenye malengo mabaya.
Kwa bahati mbaya, mikondo hii potofu huzaa athari kadhaa, ambazo ni kama zifuatazo:
Kuyumba imani za kidini
Inaonekana kwamba athari muhimu zaidi za upotovu huu ni kusababisha kuyumba na kutetereka imani za kidini na kimadhehebu za watu; jambo ambalo lenyewe ni dhambi kubwa isiyosameheka, na ni mfano kamili wa kauli ya Qur’ani: “يَصُدُّونَ عَنْ سَبِیلِ اللَّه”¹.
Kuangamiza mtaji wa fikra
Bila shaka leo, madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.) yanahitaji zaidi kuliko wakati mwingine wowote, kunufaika na nguvu za fikra katika nyanja mbalimbali. Kupotea kwa nguvu hizi ndani ya mikondo potofu na kupotezwa kwa uwezo wao wa kiakili ni hasara kubwa.
Ili kukabiliana na mikondo potofu yatufaa tufanye nini?
1. Mwenendo wa kielimu
Kunufaika na maarifa sahihi
Elimu ni mwanzo wa kila mwenendo. Kutojua itikadi sahihi za Mahdawiyya ni sababu ya msingi ya kuibuka kwa mielekeo potofu; hivyo basi hatua ya kwanza ya kujinasua na mikondo hii ni kuongeza maarifa sahihi na ya kuaminika.
Uwanja muhimu zaidi wa kujifunza haya ni kushikamana na aya za Qur’ani na riwaya sahihi za Ma‘sūmīn (a.s.). Kwa hiyo katika upande wa kielimu na utambuzi, ni lazima wenye uchungu katika uwanja huu waingie kwa mpango, kwa busara na kitaalamu, na watekeleze wajibu wao ipasavyo.
Upandikizaji wa maarifa haya unaweza kufikiriwa katika vipengele viwili vya msingi: kwanza, “maarifa sahihi na asilia ya Mahdawiyya”, na pili “kutambua upotovu, sifa zake na athari zake.”
Kubuni mfumo wa uhandisi mpana wa Mahdawiyya
Bila shaka, kutokuwiana na kutokuratibiana miongoni mwa vipengele vya utamaduni wa dini huandaa mazingira ya kusambaa upotovu. Mtazamo wa juu juu katika tafiti za Mahdawiyya ni miongoni mwa sababu muhimu za kuibuka kwa mikondo potofu. Mtazamo mpana na wa jumla kuhusu maarifa ya Mahdawiyya, kupitia mfumo wa uhandisi wa jumla kutoka kwa wasimamizi wa kitamaduni wakiwemo wanazuoni wa dini na walimu wa utamaduni, kwa namna iliyoratibiwa, unaweza kuwa kizuizi kisichopenyeka dhidi ya kuibuka kwa mikondo hii na kuendelea kwa harakati zake.
2. Njia za kivitendo
Kufichua na kuibua hisia ya tahadhari
Bila shaka ukubwa wa athari mbaya za mikondo hii potofu hakutoi nafasi ya kuzembea wala ya kuvumilia; kwa kuwa upotovu huu ni mbaya kuliko dawa za kulevya: kwani zile huharibu uhai wa mwili, na hizi huharibu roho za watu. Na kamwe hakuna yeyote atakayeridhia kuvumilia wale wanaosababisha vijana kuchafuliwa na dawa za kulevya. Kwa hiyo ni wajibu wa wote, hasa tabaka la wasomi katika jamii, kutumia fursa zilizopo kufichua mielekeo hii na hasa kuwakinga vijana na mitego ya upotovu huu.
Kung’oa mizizi ya upotovu
Mahali ambapo ushauri mwema hauleti majibu, chaguo bora ni kukabiliana ana kwa ana na mielekeo potofu na kung’oa kabisa mizizi ya upotovu wao.
Utafiti huu unaendelea…
Imenukuliwa kutoka katika kitabu kiitwacho “Dars-nāmah-ye Mahdawiyya; kilichoandikwa na Khodāmorād Salīmiyān” huku ikifanyiwa mabadiliko kiasi.
¹ “الَّذِینَ یَصُدُّونَ عَنْ سَبِیلِ اللَّهِ وَیَبْغُونَهَا عِوَجًا وَهُمْ بِالْآخِرَةِ هُمْ کَافِرُونَ؛
Wale ambao walikuwa wakizuilia Njia ya Mwenyezi Mungu, na wakataka kuipotosha, nao wanaikanusha Akhera
(Surat Hūd / Aya ya 19)
Maoni yako