Jumamosi 27 Desemba 2025 - 14:05
Kujitoa muhanga kwa mashahidi kusini kulikuwa kwa ajili ya Lebanon yote, na baadhi ya viongozi wanazungumza lugha ya adui

Hawza/ Qubaisi alitangaza: Uchaguzi ujao wa Baraza la Wawakilishi ni jihadi sambamba na mashahidi na ni ulinzi wa Lebanon iliyo huru, yenye heshima na yenye kujitegemea.

Kwa mujibu wa ripoti ya idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, mji wa Al-Nabatiyya uliadhimisha hafla Krismasi karibu na sanamu ya Hassan Kamel Al-Sabah katika lango la kaskazini la mji huo, huku ikihudhuriwa na wabunge Hani Qubaisi na Nasser Jaber, pamoja na Khalil Hamdan mjumbe wa bodi ya uongozi ya Harakati ya “Amal”, Hassan Faqih rais wa Shirikisho la Jumla la Wafanyakazi, pamoja na watu mashuhuri na wananchi.

Baada ya kuimbwa wimbo wa taifa na salamu za ukaribisho zilizotolewa na mshairi Muhammad Mu‘allim, Moussa Shumaysani, rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Al-Nabatiyya, alitoa hotuba na kusema kuwa; kuzaliwa ni furaha inayofufua matumaini ya maisha yenye heshima yanayojengwa juu ya upendo na uvumilivu, na ni ujumbe wa kuishi pamoja unaowaunganisha Walebanon kama familia moja iliyoungana.

Kisha, Hani Qubaisi, mwakilishi wa Harakati ya Amal katika Bunge la Lebanon, alitoa hotuba na kusisitiza kuwa mji wa Al-Nabatiyya, unaoinuka kutoka chini ya magofu, umesimama kwa fahari na unasambaza upendo katika taifa zima, huku ukiendelea kushikamana na ujumbe wa Imam Sayyid Musa al-Sadr kwa kuwakusanya Walebanon pamoja na kushikilia umoja wa taifa.

Alisema kuwasha mti wa Krismasi kuwa ni tendo la imani na upendo juu ya mmoja wa Mitume wa Mwenyezi Mungu, na ni ujumbe wa upendo kutoka Al-Nabatiyya kwenda kwa Walebanon wote na eneo lote, akisisitiza kuwa anayebeba imani hii huambatana na maadili, misingi na tabia njema, na hukataa sera za migawanyiko na mifarakano.

Mwanachama huyo wa Harakati ya Amal, huku akisisitiza kuwa; kujitoa muhanga kwa mashahidi kusini kulikuwa kwa ajili ya Lebanon yote bila ubaguzi wowote, na kwamba ujumbe wao ni upendo na amani, alitoa wito wa kushikamana na umoja na kukataa juhudi zozote za kuzua fitina na kudhoofisha dola.

Katika mwendelezo wa hotuba yake Qubaisi alitangaza kuwa; uchaguzi ujao wa Baraza la Wawakilishi ni jihadi sambamba na mashahidi na ni ulinzi wa Lebanon iliyo huru, yenye heshima na yenye kujitegemea, alisisitiza kuwa tukio hili la uchaguzi ni kituo cha jihadi pamoja na mashahidi na ni ulinzi wa taifa ili nchi ibaki tukufu, yenye heshima, huru na kwa uamuzi wake. Alikataa aina yoyote ya kusalimu amri kwa sera au masharti yanayolazimishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel au nguvu za kigeni.

Hatumuogopi adui huyu wala vitisho vya nje

Qubaisi alisema katika hafla ya kumbukumbu katika kijiji cha Yahmar al-Shaqif – Al-Nabatiyya: Tunasikia na kuelewa kila kinachotokea katika eneo letu, na hatumuogopi adui huyu wala vitisho vya nje, lakini kinachotuumiza ni hali ya ndani ya Lebanon.

Aliendelea kusema kuwa jambo la kusikitisha nchini Lebanon ni kuendelea kwa mpasuko wa ndani; hali ambayo katika mataifa mengine, wafuasi na wapinzani huungana duniani kote kukabiliana na wavamizi wa taifa, ilhali Lebanon inashuhudia mgawanyiko kati ya wale wanaoamini katika mapambano ya muqawama na wale wanaoyapinga, jambo linaloidhoofisha nchi na kusambaratisha nguvu ambayo Imam Musa al-Sadr aliiona kuwa ni alama ya kupambana na adui Mzayuni.

Mwanachama wa Harakati ya Amal, akibainisha kuwa anayeyaamini mapambano ya muqawama, njia yake na ujumbe wa Imam al-Sadr, ni yule anayetafuta umoja, undugu na kuishi pamoja miongoni mwa Walebanon, wakati huohuo alionya kuhusu hatari ya kaulimbiu zinazotolewa na baadhi ya nguvu za ndani ambazo zinafanana na kaulimbiu za Israel, hususan wito wa mara kwa mara wa kuvuliwa silaha mapambano ya muqawama.

Alisema: “Tunashangaa jinsi adui Mzayuni na baadhi ya vyama vya Lebanon wanavyopaza kaulimbiu moja, na jinsi wanavyojaribu kupanda mbegu za migawanyiko na mifarakano katika taifa, huku baadhi ya viongozi wakizungumza lugha ya adui.”

Qubaisi alisisitiza kuwa serikali na taasisi zake kamwe haziwezi kuchukua msimamo unaofanana na wa adui, na haifai kwa serikali, bunge au urais kutoa kaulimbiu zinazohudumia mradi wa Kizayuni.

Mwanachama huyo wa Harakati ya Amal alibainisha kuwa serikali, kupitia uongozi wake, inafanya juhudi za kuiondoa Lebanon katika mgogoro kwa njia ya mahusiano ya ndani na ya kimataifa, na inafuatilia utekelezaji wa Azimio 1701 kupitia mazungumzo, kinyume na baadhi ya nguvu za ndani zinazopambana na taasisi za dola na kulenga serikali na bunge kwa kaulimbiu zinazohudumia Israel.

Alieleza kuwa kuilinda damu ya mashahidi na kulinda taasisi za dola kunapaswa kufanywa kupitia haki za kikatiba zijazo, zilizo juu yake uchaguzi wa bunge, na akaonya dhidi ya juhudi za baadhi ya nguvu kutawala bunge na serikali na kulazimisha chaguo zao za kisiasa juu ya nchi.

Mwisho, Qubaisi alisisitiza kuwa; makabiliano ya kweli leo yako katika uwanja wa siasa, kupitia kuthibitisha kwamba uchaguzi ujao wa bunge ni jihadi sambamba na mashahidi na ni ujumbe wa ulinzi wa taifa, na akatoa wito kwamba uchaguzi huo uwe ujumbe wa kitaifa na wa pamoja dhidi ya yeyote anayetafuta migawanyiko na kutawala taasisi za dola.

Aidha, alisisitiza kushikamana na muqawama na mashahidi na kutoacha kamwe ujumbe wao, licha ya ugumu na changamoto kubwa, chini ya juhudi zinazoendelea za kubadilisha sheria ya uchaguzi na kusimamisha utendaji wa bunge kwa ajili ya kufikia malengo finyu ya kisiasa.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha