Alhamisi 25 Desemba 2025 - 23:50
Ayatullah Milani kwa hakika alikuwa mhuishaji wa Hawza ya Mashhad

Hawza/ Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu alimuelezea marehemu Ayatullah Milani kuwa ni shakhsia kamili katika nyanja za kiroho, kimaadili, kielimu na kijamii na kisiasa, na akasisitiza kuwa: Ayatullah Milani kwa hakika alikuwa mfufuaji wa Hawza ya Mashhad, na Hawza hii inamdai marehemu huyo mkubwa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza kutoka Tehran, maandishi ya hotuba ya Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika mkutano na wajumbe wa kamati ya maandalizi ya kongamano la kumuadhimisha Ayatullah al-‘Udhmaa Sayyid Muhammad Hadi Milani ni kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu sana

Na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote, na rehema na amani zimshukie Muhammad na Aali zake watoharifu.

Karibuni sana mabwana waheshimiwa; nami kwa dhati kabisa nawashukuru mabwana waheshimiwa, hususan Mheshimiwa Marvi na wengine waliotekeleza [mpango wa] kumuadhimisha marehemu Ayatullah Milani (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake). Pamoja na kwamba kwa miaka ishirini alikuwa Mashhad akifanya kazi za kielimu, kijamii, kisiasa na aina zote za shughuli, baada ya kufariki kwake, alama zake Mashhad hazikuonekana sana. Mimi wakati mwingine nilipokutana na masuala ya Mashhad, nilikuwa nashuhudia hali hii. Kwani wakati fulani alikuwa mhimili wa Mashhad; yaani alihesabiwa kuwa ni kilele cha Hawza ya kelimu, lakini baada ya kufariki kwake, kumbukumbu na jina lake lilitajwa kidogo. Mtoto wake wa mwisho, marehemu Ayatullah Asayyid Muhammad Ali, naye pia hakuonekana sana, nasi tulikuwa tukimuona mara chache katika mikusanyiko na mfano wake; inaonekana yeye pia amefariki. Hivyo basi, mkusanyiko huu mliouandaa ni mzuri, ili ufanyike utafiti juu yake, kazi zifanyike, na athari zake zifufuliwe. Nimeandika nukta kadhaa ambazo nitazieleza kuhusiana naye.

Kwanza, shakhsia yake ilikuwa na nyanja mbalimbali, ambazo kwa kila upande na kila kipengele, mtu anaweza kusema maneno kadhaa: upande mmoja ni shakhsia yake binafsi, tabia na maadili yake; upande mwingine ni wa kielimu, unaoweza kujadiliwa hali yake ya kielimu; upande mwingine ni wa mwenendo wa kiroho—ingawa wakati wa uhai wake hatukuwa na umakini wala taarifa; baadaye ndipo nilipokuja kufahamu kwamba alikuwa katika njia ya mwenendo wa kiroho, masuala ya kiroho na mfano wake, mtu wa tafakuri, riyadha na kutafakari; mambo haya hayangeweza kufahamika wakati wa uhai wake; huu pia ni upande mmoja—na upande mwingine ni wa kijamii na kisiasa. Kwa pande zote hizi, inawezekana kuzungumza juu yake, nami nitagusia kila moja kwa maneno machache.

Katika upande wa kwanza, yaani shakhsia yake binafsi na mwenendo wake binafsi, kwa hakika alikuwa mtu wa kipekee. Kwanza kabisa, alikuwa akitembea, akizungumza na kuchukua hatua kwa heshima na utulivu mkubwa. Wakati huo huo, alikuwa mnyenyekevu sana. Ndani yake kulikuwa na unyenyekevu, heshima na utulivu, pamoja na amani ya ndani ambayo mtu aliweza kuishuhudia kwake; hata katika mazingira magumu, mtu alihisi kwamba alikuwa na utulivu huo.

Uaminifu na kuthamini urafiki wa marafiki; alikuwa akiwajali marafiki zake. Alikuwa mwenzake katika masomo ya awali na marehemu mzazi wetu huko Tabriz. Alizaliwa Najaf, na baba yake alikuwa mkwe wa marehemu Sheikh Muhammad Hasan Mamqani mashuhuri, mwandishi wa sherehe ya Makaseb na shakhsia kubwa na marji' wa wakati wake, ambaye inaonekana alifariki mwaka 1321 au 1322 Hijria. Hivyo alizaliwa Najaf, lakini baba yake alihamia Tabriz na kukaa huko kwa mwaka mmoja au miwili, kisha akarudi Najaf. Katika kipindi hicho kifupi, mtu huyu aliyekuwa akisoma madrasa alisoma pamoja na marehemu mzazi wetu na mmoja wa wanazuoni wa Tabriz, yaani marehemu Asayyid Ibrahim Darvazeh’i—ambaye mwanawe Asayyid Mahdi Darvazeh’i alikuwa Tehran; huenda baadhi yenu mnamfahamu. Hawa watatu walikuwa wenzake masomoni. Ayatullah Milani, kutokana na historia hiyo, alikuwa na uhusiano wa kipekee na marehemu mzazi wetu.

Mara nyingi alikuwa akiamka asubuhi mapema na kuja pale. Wakati fulani pia marehemu Asayyid Ibrahim Darvazeh’i alipokuja Mashhad, wote watatu walikutana nyumbani kwa marehemu mzazi wetu. Alikuwa mwaminifu; alithamini urafiki wa zamani.

Alikuwa mtu mwenye kikao kizuri sana; yaani mtu alipokaa naye, kikao chake kilikuwa chenye ladha na mvuto; alikuwa na hisia nyororo za kisanaa na mashairi. Katika baadhi ya maandishi na vitabu ambavyo kwa mtazamo wangu havikuwa na uhusiano wa moja kwa moja naye, niliona kwamba alikuwa ameandika mashairi; bila shaka alikuwa ameandika mashairi ya Kiarabu; alikuwa mtu wa mashairi, ladha ya kisanaa na mambo kama hayo; yaani alikuwa mkusanyiko wa sifa za shakhsia bora na ya kipekee. Aidha, ikumbukwe kwamba alikuwa mjukuu wa Sheikh Muhammad Hasan Mamaqa'ni na mkwe wa Mamaqa'ni mwenye kitabu cha Rijal; alikuwa mkwe wa marehemu Sheikh Abdullah Mamaqa'ni. Darasani pia wakati mwingine alikuwa akimtaja mjomba wake akisema: “marehemu mjomba,” akirejea maneno yake katika kitabu cha Rijal. Kwa ujumla, alikulia katika familia ya kielimu.

Marehemu Ayatullah Milani (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake), kwa upande wa kielimu, bila shaka katika wakati wake alikuwa sura mashuhuri ya kielimu; alikuwa mwanazuoni mkubwa sana. Sehemu kubwa ya manufaa yake ya kielimu aliipata kutoka kwa marehemu Ayatullah Na’ini na marehemu Sheikh Muhammad Husayn Isfahani, ambao aliwaita katika masomo yake: “Mirza mwalimu” na “Haj Sheikh mwalimu.” Hata hivyo, mwelekeo wake wa fikra za kifikh na kielimu ulikuwa karibu zaidi na marehemu Ayatullah Na’ini. Mimi kwa kuwa sikuhudhuria masomo yake ya Usul, sijui alikuwa akifundisha vipi katika Usul, lakini katika masomo ya Fiqhi, mwelekeo wake ulikuwa zaidi upande wa marehemu Ayatullah Na’ini, na alikuwa akijadili na kufundisha kwa mtindo unaofanana na wake.

Katika masomo, alikuwa mtulivu sana, mwenye heshima na mwasilishaji mzuri; yaani si kwa maana ya kuzungumza mfululizo bila kukoma, bali alikuwa mfasiri mzuri sana; mwanafunzi yeyote aliyesikiliza somo lake, kwa hakika alielewa. Alikuwa mwalimu mashuhuri na mkubwa. Kwa kweli, Hawza ya Mashhad aliifufua yeye. Hawza ya Mashhad, katika kipindi fulani cha marehemu Aqazadeh na marehemu Haj Aqa Husayn, ilikuwa katika kilele cha maendeleo; lakini baada ya kuuawa kwao, kwa miaka mingi Hawza iliingia katika hali ya kudorora; yaani katika Fiqhi na Usul hakukuwa na somo ambalo lingeweza kumfunga na kumweka mwanafunzi mwenye hamu Mashhad. Alipokuja yeye, aliifufua Hawza; yaani Hawza ya Mashhad kwa kweli inamdai marehemu Ayatullah Milani. Kwa hakika aliifufua Hawza na akaanza masomo yake pale; alianza masomo ya Fiqhi usiku, na katika Madrasa ya Msikiti wa Haj Mulla Hashim akaanza somo la Ijara. Mimi wakati huo sikuhudhuria masomo ya nje, kwa hiyo sikuyaona, lakini baadaye alianza masomo ya Swala, ambayo yaliendelea kwa kina kwa miaka mingi, labda miaka saba, nane au kumi. Baadaye pia alizungumzia Zaka, Khums na mfano wake, ambazo nadhani baadhi yake hata zilichapishwa.

Zaidi ya shakhsia yake ya kielimu, alikuwa na mtazamo makini juu ya Hawza—mtazamo wa dhati kabisa—na tangu alipokuja, alikuwa akiwatafuta wanafunzi bora. Mwanzoni mwa kuja kwake Mashhad, alifanya mgawanyo fulani kwa wanafunzi bora, jambo ambalo hata lilimletea matatizo fulani. Alikuwa akitafuta wanafunzi wenye vipaji na kuwajali; kwa sababu hiyo, alianzisha madrasa; inaonekana alianzisha madrasa mbili au tatu. Wakati alipokuwa akianzisha madrasa hizo, sisi hatukuwa tena na uhusiano wa karibu naye, kwa hiyo sina taarifa nyingi juu ya hali ya madrasa zake; lakini alikuwa makini juu ya Hawza na mambo yanayohusiana nayo. Huu pia ni upande wa kielimu wake.

Katika upande wa mwenendo wa kiroho, alikuwa na uhusiano na marehemu Asayyid Abdul Ghaffar Mazandarani, ambaye alikuwa katika safu ya marehemu Ayatullah Qadhi na wanazuoni wengine kama hao huko Iraq na Najaf.

Katika kitabu kilichochapishwa kutoka kwake—ambacho nilikiona miaka kadhaa iliyopita; inaonekana marehemu Asayyid Muhammad Ali ndiye aliyekusanya na kuchapisha barua zilizoandikwa kwake—kuna barua kadhaa kutoka kwa marehemu Asayyid Abdul Ghaffar kwenda kwake, zenye maelekezo, na inaonekana kwamba alikuwa ameuliza maswali na alikuwa na uhusiano wa kiroho naye. Sisi wakati huo tuliona kwamba alikuwa akihusiana na watu wa mwenendo wa kiroho na masuala ya kiroho; tulishuhudia hili mara nyingi. Kwa mfano, marehemu Haj Mulla Aqajan alipokuja Mashhad, alikuwa na uhusiano naye na alipanda mimbari; niliona mwenyewe kwamba nyumbani kwa Ayatullah Milani, marehemu Haj Mulla Aqajan alipanda mimbari. Au wengine, kama yule Bwana Naqibi mashuhuri kwa jina la “Nur” huko Mashhad, walikuwa na mawasiliano naye. Uhusiano wa aina hii ulikuwepo na mtu aliweza kuuona. Lakini kwamba alikuwa katika njia ya mwenendo wa kiroho akipata mafunzo kutoka kwa mwalimu au akifanya amali maalumu za kiroho na ibada maalumu, hili hatukulihisi kuhusu Ayatullah Milani; lakini lilikuwepo; baadaye ndipo mtu anapofahamu kwamba hali hiyo ilikuwapo. Marehemu Ayatullah Tabataba’i alikuwa na uhusiano mkubwa sana naye. Ayatullah Tabataba’i karibu kila mwaka majira ya joto alikuwa akija Mashhad na, nadhani, alikaa kwa wiki mbili au tatu, na katika kipindi hicho alikuwa makini kuhudhuria Swala yake. Marehemu Ayatullah Milani alikuwa akiswali Magharibi na Isha majira ya joto katika uwanja mpya, sasa unaitwa Uwanja wa Azadi, na marehemu Ayatullah Tabataba’i alikuwa akisisitiza kushiriki Swala hiyo na alikuwa na ukaribu na uhusiano wa dhati naye; jambo hili lenyewe lilikuwa dalili ya kuwa alikuwa na upande wa mwenendo wa kiroho. Pia kuna simulizi nyingi za miujiza yake zilizopokewa kupitia njia za kuaminika; mimi binafsi nimesikia matukio kadhaa kupitia njia zilizoaminika kabisa. Moja ni kupitia kwa marehemu Haj Aqa Murtadha Ha’iri, ambayo yameandikwa na hata kuchapishwa; na kutoka kwa wengine pia, matukio kama hayo yameshuhudiwa, jambo linaloonesha kwamba alikuwa mtu wa maana ya ndani, umakini, mtazamo wa wazi wa kiroho na mfano wake. Huu ndio upande wa mwenendo wake wa kiroho.

Ama katika upande wa masuala ya kisiasa na kijamii; mwanzoni mwa mapambano, alikuwa miongoni mwa nguzo za harakati. Katika mwaka 41 na 42 (Hijria Shamsia) mapambano ya wanazuoni yalipoanza, marehemu Ayatullah Milani kwa hakika alikuwa miongoni mwa nguzo za harakati. Kwanza kabisa, matamko yake yalikuwa imara sana. Sisi tulikuwa katika Madrasa ya Hujjatiyya; kulikuwa na ubao wa matangazo ambapo matamko yalibandikwa, nasi tulisimama na kuyasoma. Nakumbuka wakati mmoja tamko kutoka kwa Ayatullah Milani lilikuja, na maandishi yake yalikuwa yenye nguvu, heshima na uimara kiasi kwamba kila mtu aliguswa na uzuri na nguvu ya maneno hayo. Alikuwa wa aina hii; maandishi yake yote ya Kiajemi yalikuwa hivyo hivyo. Sasa sikumbuki kama nimeona maandishi yake ya Kiarabu, lakini maandishi yake ya Kiajemi yalikuwa yenye heshima, yenye nguvu na mazuri sana. Baadaye, wakati Imam alipofungwa gerezani na kulikuwa na uwezekano wa hukumu kali, wanazuoni wa daraja la juu kutoka miji yote walikuja Tehran; bila shaka, kilele cha mkusanyiko huo kilikuwa marehemu Ayatullah Milani—hakuna shaka. Ingawa Ayatullah Shariatmadari naye alikuwapo na alikuwa marji' wa taqlid, lakini heshima na hadhi ya Ayatullah Milani miongoni mwa wanazuoni ilikuwa dhahiri sana na ya juu. Na bila shaka, kilele cha mkusanyiko huo wa wanazuoni na aliyeathiri zaidi alikuwa marehemu Ayatullah Milani (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake).

Na mwanzoni mwa mwaka 42, pale tukio la tarehe kumi na tano ya Khordad lilipotokea, alikuwa katikati ya matukio. Imam (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) alinipa jukumu la kwenda Mashhad na kuzungumza na kila mwanazuoni mmoja mmoja. Kulikuwa na ujumbe wa aina mbili; mmoja maalumu kwa Ayatullah Milani na marehemu Haj Aqa Hasan Qumi, na mwingine wa jumla.

Ujumbe uliomhusu Ayatullah Milani, nilimfikishia; nilimwambia kwamba Imam Khomeini anapendekeza muwalazimishe wahubiri kuanzia siku ya saba ya Muharram wazungumze juu ya tukio la Fayziyyah juu ya mimbari; na kuanzia siku ya tisa, mzilazimishe jumuiya za kidini zizungumze. Huu ndio ujumbe niliomfikishia. Alisema: kuanzia siku ya tisa? Mimi nimeshaanza kabla ya hapo; aIlionekana wazi kwamba alikuwa ameingia kikamilifu katika masuala hayo, na fikra ile ile ambayo ilijitokeza na kutekelezwa Qum kupitia Imam (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake), ilikuwa pia ndani yake. Yaani uwepo wake katika mapambano ulikuwa wa aina hiyo na alikuwa na mpango kwa ajili ya suala hilo. Bila shaka, kwa kiasi fulani mpango wake ulikuwa tofauti na wa Imam, lakini alikuwa ameandaa mpango; alikuwa na mpango kwa ajili ya jambo hilo.

Katika nyanja za kisiasa na kijamii, alikuwa mtu mwenye kifua kipana; yaani alikuwa akiwasiliana na watu wa aina mbalimbali waliokuwa hai katika mapambano, siasa na mambo yanayofanana. Kwa mfano, alikuwa na uhusiano na marehemu Mhandisi Bazargan na Daktari Sahabi na wengine kama wao. Mara mbili au tatu nilipotaka kusafiri kutoka Mashhad kwenda Tehran, nilimtembelea kwa ajili ya kumuaga, alinieleza: Unapofika Tehran, je, utaenda gerezani kumtembelea Mhandisi Bazargan pia?—wakati huo alikuwa gerezani; mwaka 43 na 44—nikasema ndiyo, akaniambia: msalimie kwa niaba yangu. Yaani mara mbili au tatu alituma salamu zake kwa Mhandisi Bazargan kupitia mimi. Ilionekana wazi kwamba alikuwa na uhusiano na kundi hilo pia. Hata hivyo, alikuwa akijiepusha sana na kwamba mtu amhusishe na makundi ya kisiasa kama vile Jabhah Melli na mfano wake; aliniambia binafsi kwamba ikiwa mtu atanihusisha na Jabhah Melli, sitaridhika naye wala sitamsamehe. Hivyo ndivyo alivyokuwa, lakini alikuwa na mawasiliano mengi.

Katika baadhi ya miaka, kwa mtazamo wetu, alionekana kana kwamba amepunguza kasi katika masuala ya mapambano, hadi tulimkosoa; lakini sasa baada ya barua kuchapishwa, imeonekana kwamba katika kipindi hicho alikuwa na mawasiliano mengi kwa barua na Ayatullah Shariatmadari na wanazuoni wengine na alikuwa akifanya kazi; ila sisi hatukuwa na taarifa juu ya shughuli zake. Katika barua ambazo watu waliandika wakitangaza kuunga mkono maraji' waliokusanyika Tehran kwa ajili ya kuachiliwa Imam Khomeini, labda jina lake lilitajwa zaidi kuliko yote, na alikuwa ndiye aliyekuwa akipewa umuhimu mkubwa zaidi.

Aliandika barua moja kwa Imam ambayo kwa mtazamo wangu ni waraka wa kihistoria. Mwaka 43, Imam alipopelekwa uhamishoni Uturuki, Ayatullah Milani aliandaa mkutano nyumbani kwake na akawaalika wanazuoni wa Mashhad; sisi vijana wachache tuliokuwa tukihusika na mapambano pia tulialikwa; tulikuwepo. Wanazuoni wa Mashhad, akiwemo marehemu Haj Sheikh Mujtaba na wengine, wote walihudhuria. Mtoto wake alisimama na kusoma barua aliyokuwa amemwandikia Imam (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake). Ni barua ya kipekee sana; barua yenye nguvu na heshima kubwa katika kumuunga mkono Imam na kuonesha huzuni juu ya uhamisho wake. Nakumbuka baadhi ya maneno yake: Kunyamaza ni ndugu wa kuridhia, na asiekuwa nasi basi yupo dhidi yetu. Maneno haya yalikuwepo ndani yake. Pia alielezea maneno ya Amirul-Mu’minin wakati Abu Dharr alipohamishwa. Kwa mtazamo wangu, ni waraka wenye kuaminika sana. Yeye mwenyewe alikuwa amekaa pale, na mtoto wake alisimama na kusoma barua hiyo, na wote walisikiliza.

Kwa ufupi, kwa hakika alikuwa mtu kamili wa pande zote; kielimu, kimaadili, kiroho, kisiasa na kijamii; mtu mkubwa, kamili, mwenye sifa nyingi na mwenye haki isiyosahaulika juu ya Hawza ya Mashhad.

Tunatumaini, Insha’Allah, kwamba dhima hii mliyoiandaa itaweza kumtambulisha kwa watu kwa upana zaidi kuliko alivyojitambulishwa hadi sasa.

Wassalamu ‘alaykum wa rahmatullahi wa barakatuh

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha