Kwa mujibu wa huduma ya habari ya kimataifa ya shirika la habari la Hawzah, zaidi ya wiki tatu zimepita tangia kutangazwa usitishwaji wa mapigano kati ya makundi ya Muqawama huko Ghaza na utawala wa Kizayuni, na kila siku tunashuhudia uhalifu wa kinyama wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Baada ya kupita miaka miwili tangia mauaji ya halaiki yaliyofanywa na Wazayuni huko Ghaza, Ofisi Kuu ya Takwimu ya Palestina imetoa takwimu za kushtua kuhusu uhalifu uliofanywa na utawala huu unaoungwa mkono na Marekani huko Ghaza na Ukingo wa Magharibi.
Majengo 192,812 yameripotiwa kuharibiwa katika Ukanda wa Ghaza, Misikiti 828 imebomolewa kabisa, wafungwa 6,600 wamekamatwa kutoka Ghaza, mashahidi 68,531, mashahidi 1,061 katika Ukingo wa Magharibi, majeruhi 9,034 katika Ukingo wa Magharibi na wafungwa 12,100 wamekamatwa katika Ukingo wa Magharibi. Takwimu hizi zimetolewa huku watu wengine 10,000 wakiwa bado wamezikwa chini ya kifusi.
“Mohammad Mun’im,” daktari wa Kipalestina, ameandika katika ukurasa wake binafsi wa mitandao ya kijamii; sasa ni zaidi ya siku 20 zimepita tangia kuanza usitishaji wa mapigano katika Ukanda wa Gaza. Katika siku saba za mwanzo, hali ilikuwa tulivu kiasi, lakini baada ya hapo mashambulizi yanayofanywa na utawala wa Kizayuni yameongezeka tena. Mabomu yanarushwa mara kwa mara katika maeneo ya mashariki na operesheni kadhaa za mauaji pia zimefanyika katika maeneo ya kati ya Ukanda wa Ghaza. Katika kipindi hiki pekee, zaidi ya Wapalestina 100 wameuawa kishahidi huko Ghaza.
Licha ya hatari na uharibifu, watu wa Ghaza waliodumu katika msimamo wao walirejea katika ardhi zao tangia siku za mwanzo za usitishaji wa mapigano, na kwa kutumia vifaa vichache sana, walijenga makazi ya muda kwa kutumia miti na vitambaa. Hata hivyo, kutokana na uharibifu mkubwa wa miundombinu, idadi kubwa ya watu bado hawajaweza kurejea katika nyumba na ardhi zao, na wamelazimika kuishi katika maeneo ya wakimbizi kama vile "Mawasi Khan Yunis" na sehemu za kati za Ukanda wa Gahza.
Katika kipindi hiki, kwa wastani, malori 300 yenye vyakula vikavu kama vile nafaka huingia Ghaza kila siku. Lakini hakuna msaada wa maana uliofikia vituo vya afya, na dawa, vifaa vya matibabu, hata vyakula vya msingi kama kuku, nyama na bidhaa nyingine muhimu hupatikana kwa shida sokoni.
Moja ya matatizo makubwa ya watu ni ukosefu wa fedha taslimu. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, watu wa Ghaza, mbali na kupoteza wapendwa wao, wamepoteza kazi na vyanzo vya mapato, na uwezo wa kununua kwa familia nyingi umeshuka hadi sifuri.
Mzingiro bado unaendelea na wasiwasi wa watu kuhusu kuwasili kwa msimu wa baridi huongezeka kila siku. Wanajua kwamba mahema yao hayataweza kuwa hifadhi salama kwa watoto wao.
Njama ya kuwafukuza watu wa Ghaza kwenda katika nchi mbalimbali duniani
“Daniella Weiss,” mmoja wa viongozi wa walowezi wa Kizayuni, katika kauli zake za hivi karibuni alisema: “Waarabu hawatabaki katika Ukanda wa Ghaza. Nani atabaki? Wayahudi! Afrika ni kubwa. Kanada ni kubwa, dunia itawapokea watu wa Ghaza. Tutafanikisha hili vipi? Tutawahamasisha.” Pia alisema: “Kama mnataka kuliita hilo kuwa ni usafishaji wa kikabila, au mnataka kuiita kuwa ni ubaguzi wa rangi, basi chagueni tafsiri yenu wenyewe.”
Ukingo wa Magharibi na Quds inayokaliwa kwa mabavu
Katika Ukingo wa Magharibi na Quds inayokaliwa kwa mabavu, mashambulizi ya walowezi wa Kizayuni dhidi ya watu na maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo yanaongezeka kila siku. Walowezi hao, wakiwa na msaada kamili wa jeshi la uvamizi, wanavamia vijiji vya Wapalestina na kuwazuia watu kufanya kazi na biashara zao. Mashambulizi haya yamekuwa makali zaidi hasa katika msimu wa kuvuna zeituni.
Katika Quds Tukufu, kibla ya kwanza ya Waislamu, kila siku na katika sehemu kubwa ya siku, inakuwa shabaha ya mashambulizi ya Wazayuni. Mamia ya walowezi, wakiwa na usaidizi wa wanajeshi wa uvamizi, huingia katika Msikiti wa Al-Aqsa, wakifanya kufuru katika maeneo matakatifu ya Kiislamu, Mtume wa Uislamu na Qur’an Tukufu, na kutamka kauli za matusi dhidi ya Waislamu.
Wakati kuanza na usitishaji wa mapigano uko mikononi mwa adui wa Kizayuni
Katika siku mbili zilizopita, katika tukio la kiusalama mashariki mwa Rafah, askari mmoja wa Kizayuni aliuwawa. Muqawama ulitoa tamko likieleza kuwa haujafanya operesheni yoyote dhidi ya majeshi ya Kizayuni na umeendelea kuheshimu makubaliano ya usitishaji wa mapigano. Hata hivyo, Wazayuni wakadai kuwa muqawama umevunja usitishaji wa mapigano (wakati ambapo wao wenyewe wamekiuka makubaliano hayo mara kadhaa), usiku uliopita walishambulia Ghaza na kuwaua kishahidi Wapalestina 100, nusu yao wakiwa watoto. Baadaye walitangaza kuwa “majibu yetu kwa uvunjaji wa usitishaji wa mapigano yamekamilika” na wakarudi katika usitishaji wa mapigano.
Mustakabali wa Ghaza katika kivuli cha amani na vita
Watu wa Ghaza bado hawajaonja ladha tamu ya amani ya kudumu na usalama katika maeneo yao wanayoishi. Wanapitia siku ngumu wakiwa na njaa, kiu, ukosefu wa chakula na dawa, na makazi yasiyofaa, huku matumaini yao yakiwa kwa Mwenyezi Mungu na msaada wa makundi ya muqawama yanayoamini malengo ya Palestina kutoka sehemu mbalimbali za dunia, ikiwemo Palestina yenyewe.
Maoni yako