Alhamisi 23 Oktoba 2025 - 13:05
Wafungwa wa Kipalestina ni nembo ya uthabiti dhidi ya watawala dhalimu

Hawza/ Antonio Guerrero, shujaa wa Jamhuri ya Cuba na mmoja wa wanachama wa kundi la “Mashujaa Watano wa Cuba”, katika ujumbe wake wa kibinadamu na wa kina kuwaelekea wafungwa wa Kipalestina, amewataja kuwa ni nembo ya uvumilivu na uimara mbele ya utawala dhalimu, akisisitiza kuwa uhuru uko karibu, na Cuba haitawaacha peke yao.

Kwa mujibu wa  Shirika la Habari la Hawza, Antonio Guerrero katika mahojiano maalumu na kituo cha televisheni cha al-Mayadeen, pembeni mwa tamasha la kimataifa la “Granma–Rebelde”, akiwa ameonesha hisia za mshikamano wake na wafungwa wa Kipalestina, alielezea uzoefu wake binafsi wa miaka tele ya kifungo katika magereza ya Marekani kama daraja linalounganisha mapambano ya Cuba na Palestina.

Akasema: “Ninajua maana ya kuwa mfungwa mikononi mwa adui ambaye mwenyewe ni mhalifu. Najua ni kwa jinsi gani ni vigumu wakati wanapojaribu kukuondolea matumaini, lakini bado unaishi kwa imani.”

Msimamo wa kupinga dhulma; kiini cha ubinadamu

Mpiganaji huyu wa Kikuba, ambaye katika miaka ya 1990 aliingia ndani ya makundi yanayoipinga Marekani ili kukabiliana na vitendo vya kigaidi dhidi ya nchi yake, na kisha akafungwa kwa miaka mingi katika magereza ya shirikisho la Marekani, alisema kuwa upinzani ndio kiini cha ubinadamu, na akasisitiza:

“Funzo nililolipata kutokana na mapambano ni kwamba; kanuni ya haki ni yenye nguvu zaidi kuliko jeshi lolote. Kama alivyosema José Martí, ‘kutoka ndani ya pango dogo mtu anaweza kuishinda himaya kubwa.’”

Guerrero akaongeza kusena: “Wafungwa wa Kipalestina hawapiganii uhuru wao tu, bali pia heshima ya kibinadamu na haki ya kujitawala kwa taifa ambalo kwa miongo kadhaa limeishi chini ya uvamizi. Kila sekunde ya uvumilivu wao ni ushahidi wa ushindi, kwani hata wakiwa kifungoni bado wako huru.”

Ujumbe wa matumaini na upendo kutoka Cuba kwa Palestina
Antonio Guerrero katika mwisho wa ujumbe wake alisema: “Fahamuni kuwa Cuba haitawaacha peke yenu. Kutoka katika nchi hii ndogo lakini yenye uhuru, tunawatumia upendo usio na kikomo, mshikamano usio na mipaka, na nguvu kubwa. Uhuru uko karibu, na siku hiyo ikifika, sote – kuanzia Havana hadi Ghaza – tutasherehekea, bila kujali gharama zake.”

Mwitikio wa kihistoria na kisiasa kutokana na ujumbe huu

Ujumbe huu, ambao umeangaziwa kwa upana katika vyombo vya habari vya Amerika ya Kusini, umekumbusha uhusiano wa kihistoria kati ya Mapinduzi ya Cuba na harakati ya ukombozi ya Palestina – uhusiano uliojengwa juu ya misingi ya kudai haki, kujitegemea, na kusimama dhidi ya ubeberu.

Ni uhusiano unaoonesha kuwa mshikamano kati ya mataifa na uzoefu wa pamoja wa mapambano hauzuiliwi na mipaka wala jiografia, na kwamba jitihada za kutetea haki na uhuru daima zitabaki kuwa chanzo cha msukumo kwa vizazi vijavyo.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha