Kwa mujibu wa kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Sayyid Zawar Hussain Naqvi, katika taarifa yake rasmi, ameonesha masikitiko makubwa kuguatia shahada ya kamanda shujaa na jasiri wa jeshi la Yemen, Luteni Jenerali Muhammad Abdulkarim al-Ghamari, aliyeuawa katika uvamizi wa kinyama uliofanywa na utawala wa Kizayuni.
Katika taarifa hiyo imeelezwa kuwa: “Kujitolea huku kukubwa si fahari tu kwa taifa lenye msimamo thabiti la Yemen, bali ni heshima na utukufu kwa Umma mzima wa Kiislamu. Shahidi al-Ghamari alikuwa miongoni mwa sura mashuhuri, zenye busara na ushujaa wa kipekee ndani ya jeshi la Yemen, ambaye alitekeleza jukumu adhimu katika kuutetea Umma wa Kiislamu na kuwaunga mkono wananchi wanyonge wa Palestina. Shahada yake imethibitisha tena kwamba taifa na uongozi wa Yemen wamesimama mstari wa mbele katika kuilinda heshima na hadhi ya Umma wa Kiislamu.”
Sayyid Zawar Hussain Naqvi, akigusia mashambulizi ya hivi karibuni yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Yemen, aliongeza: “Tendo hili la kigaidi ni mfano halisi wa ugaidi wa kiserikali wa Israel, na ni uvunjwaji wa wazi wa sheria za kimataifa na misingi ya kibinadamu. Jamii ya kimataifa, hususan Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), vinapaswa mara moja kutekeleza wajibu wake wa kibinadamu na kimaadili kwa kuchukua hatua madhubuti za kukomesha jinai na uvamizi huu.”
Katika sehemu nyingine ya ujumbe wake, alisema: “Shahidi Luteni Jenerali Muhammad Abdulkarim al-Ghamari alitoa uhai wake kwa ajili ya uhuru, hadhi na heshima ya taifa la Yemen, na kwa kulitetea taifa linalodhulumiwa la Palestina. Damu yake safi ni ujumbe wa kuamsha dhamiri za Umma wa Kiislamu, na inatuamsha tuwe na umoja, mwamko na uimara dhidi ya dhulma na ubeberu wa kimataifa.”
Mwisho wa taarifa yake, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Ja‘fariyya Pakistan alipeleka salamu za rambirambi kwa kiongozi wa Mapinduzi ya Yemen, Sayyid Abdulmalik Badruddin al-Houthi, kwa viongozi wa kijeshi, kwa familia ya shahidi, na kwa taifa lenye subira na jasiri la Yemen, huku akimuomba kwa Mwenyezi Mungu kumkirimu shahidi huyo daraja tukufu la peponi, na kuijalia Yemen uvumilivu na ustahimilivu.
Maoni yako