Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Muhammad Saidii katika khutba za Swala ya Ijumaa za tarehe 25 Mehr 1404 (sawa na Oktoba 17, 2025) zilizofanyika katika Muswala wa Quds mjini Qom Iran, amesema:
“Iran yenye nguvu inaweza kupatikana tu kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na kuwa na uchumi thabiti na uliounganishwa. Uchumi ambao unategemea uwezo wa ndani, rasilimali watu wenye ufanisi, na uhusiano wa kimantiki na wa busara na uchumi wa kikanda na kimataifa.”
Akiendelea na hotuba yake amesema: “Katika dunia ya leo, nguvu ya mataifa inapimwa zaidi si kwa rasilimali asilia au uwezo wa kijeshi, bali kwa nguvu ya kiuchumi yenye uwezo wa kushindana na dunia. Uchumi wenye nguvu si tu ni nguzo ya usalama wa taifa, bali pia ni chanzo cha maendeleo ya elimu, kuinua kiwango cha maisha ya wananchi, kujitegemea kisiasa na kusonga mbele kimaendeleo. Nchi ambayo ni dhaifu kiuchumi, bila shaka itakuwa dhaifu pia katika nyanja nyingine.”
Khatibu wa Ijumaa wa Qom ameongeza kusema: “Kufanikisha uchumi wenye nguvu hakuwezekani bila ushiriki wa wananchi na usimamizi wa serikali. Uwepo hai wa sekta binafsi zinazozalisha, ujenzi wa miundombinu ya kisasa, mfumo wa kifedha ulio salama, na sera endelevu za kiuchumi – haya yote ndiyo misingi ya uundaji wa nguvu hiyo. Uchumi usioweza kutikiswa na vitisho ndiyo injini ya kuisukuma Iran yenye nguvu.”
Amesema pia kuhusu kukaririwa mazungumzo ya uongo na Trump kwamba: “Trump aliona kuvunja ahadi na kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia (Barjam) kuwa ni jambo la kujivunia kwake. Hata hivyo, kwa unafiki, ameeleza kuwa ananyoosha mkono wa urafiki na kuonesha hamu ya kufikia makubaliano ya amani.”
Imamu wa Ijumaa wa Qom ameendelea akisema: “Kauli hizi za kudhalilisha zinatolewa ilhali Iran ilikuwa katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani, na hapo ndipo alipomwachia mbwa wake mwenye kichaa – yaani utawala muovu wa Kizayuni – ili uishambulie Iran. Pia katika kamusi ya Marekani ya kibeberu na rais wao mwenye tabia za kifir’auni, maana ya neno ‘mazungumzo’ na ‘makubaliano ya amani’ ni tofauti kabisa na ile inayofahamika duniani.”
Akaongeza kuwa: “Kila mtu mwenye haki atakiri kwamba makusudio ya Marekani inaposema ‘makubaliano ya amani’ si kitu kingine isipokuwa udhalili, fedheha na kujisalimisha bila masharti mbele ya tamaa za kupindukia za Marekani. Matokeo ya jambo hili yanaonekana katika hafla ya Sharm al-Sheikh na katika uvunjaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano na utawala wa Kizayuni, utawala ambao mauaji ya kimbari yamekuwa dira yake kuu.”
Mwakilishi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkoa wa Qom ameongeza kusema:
“Taifa la Iran, linalokabiliana na utawala huu mchafu na Marekani, linawaambia: sisi, taifa la Iran, tutayavunja meno yenu nyinyi wazushi.”
Kuishi kwa uadilifu na kujichunga ni faradhi ya kijamii
Akiendelea na hotuba yake, Ayatullah Saidi amesema:
“Kuishi kwa uadilifu na kujichunga, katika mtazamo wa kwanza, ni jukumu la kimungu na wajibu wetu wote kwa ujumla. Na kwa mtazamo mwingine, ni haki ya kimsingi ya kila binadamu. Wajibu huu hauhusu kundi fulani au jinsia fulani tu, bali ni jukumu la kila mtu, taasisi za malezi na utamaduni, vyombo vya habari, familia na viongozi wote wanawajibika kulilinda jambo hili.”
Msimamizi wa Haram ya Bibi Fatima al-Ma’suma (a.s) amesema: “Mwanamume na mwanamke wanaoingia katika jamii kwa kuheshimu mipaka ya sheria tukufu ya dini, mipaka ya kimaadili, na kuvaa mavazi yanayostahiki, kwa hakika wanakuwa wametekeleza faradhi ya kijamii. Kuheshimu mavazi yenye staha si chaguo la kibinafsi tu, bali ni kutekeleza jukumu kubwa mbele ya jamii.”
Amefafanua kwa kunukuu maneno ya Mwenyezi Mungu katika Aya ya 27 ya Suratun-Nisaa:
{ وَٱللَّهُ یُرِیدُ أَن یَتُوبَ عَلَيكُم وَیُرِیدُ ٱلَّذِینَ یَتَّبِعُونَ ٱلشَّهَوَ تِ أَن تَمِیلُوا۟ مَیلًا عَظِیما }“Na Mwenyezi Mungu anataka kukurejezeni kwenye ut'iifu wake, na wanao taka kufuata matamanio wanataka mkengeuke makengeuko makubwa.”
[Surah An-Nisāʾ: 27]
Kisha akasema: “Aya hii inaonyesha kuwa irada ya Mwenyezi Mungu ni wanadamu kuishi maisha ya uadilifu na kujichunga.”
Imamu wa Ijumaa wa Qom akaendelea kusema: “Jumii ya waumini lazima isimame pamoja mbele ya kambi ya shetani, ambayo ni alama ya upotovu, uovu na ukosefu. Kujichunga si amri ya kisheria tu, bali ni ufunguo wa bahari ya baraka na mafanikio ya kimwili na ya kiroho kwa watu.”
Kuhusu shahidi Yahya Sinwar
Akiwakumbuka mashahidi wa Palestina, Ayatullah Saidi alisema: “Yahya Sinwar alikuwa kamanda shujaa wa harakati ya kishujaa ya Toufan al-Aqsa. Kwa nguvu, ujasiri na imani yake, aliwazuia wavamizi wa Kizayuni kutekeleza njama zao katika uvamizi wa Palestina. Kuwa kwake na tasbihi iliyotengenezwa kwa udongo wa Sayyid al-Shuhadaa (Imam Husayn a.s.) wakati wa kuuawa kwake ni ujumbe mkubwa kwa wote, kwamba njia pekee ya wokovu katika mambo yote ni kufuata njia ya Ahlul-Bayt (a.s.).”
Ayatullah Saidi katika khutba yake ya kwanza alisema:
Imam Bāqir (a.s) anasema:
«فَوَ اللّه ما شیعَتُنا إلا مَن اتَّقَی اللّه وَأطاعَهُ؛»
Naapa kwa Mwenyezi Mungu, si miongoni mwa wafuasi wetu ila ni yule anayemcha Mungu na kumtii Yeye.
Akasema: Waja wapendwa na wahishimiwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu ni wale watu wenye taqwa (wachamungu).
Imamu wa Sala ya Ijumaa wa Qum, katika tafsiri ya aya ya kwanza ya Suratul-Fath alisema:
«إِنَّا فَتَحْنَا لَکَ فَتْحًا مُبِینًا؛»
Hakika tumekupa ushindi ulio wazi.
Akasema: Maelezo kuhusu umuhimu wa sura hii yanahusiana na mazingira ya mahali na wakati wa kushuka kwa aya ya mwanzo ya Suratul-Fath. Sura hii ins ujumbe wa ushindi mkubwa, wa hakika na wa wazi dhidi ya maadui wa Uislamu.
Akaongeza kusema: Sura hii iliteremshwa baada ya tukio la Sulhu ya Hudaybiyyah, mwaka wa sita wa Hijra, pale Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa akielekea Makka akiwa pamoja na Ansari na Muhajirina kwa ajili ya kutekeleza ibada ya ‘Umrah. Makafiri wa Kiquraish waliwazuia katika eneo la Hudaybiyyah wasiingie Makka, hivyo Mtume (s.a.w.w.) na wenzake walilazimika kurudi Madina bila kutekeleza ‘Umrah. Hali hii ilitokea wakati Waislamu wakiwa tayari wamevaa ihram na hawakuwa na dalili yoyote ya vita. Kitendo hicho cha washirikina hakikuizuia tu ‘Umrah ya Waislamu bali pia kilivunja utamaduni wa kale wa usalama wa mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu.
Msimamizi wa Haram Tukufu ya Bibi Ma‘suma (a.s.) alisema: Tukio hili, ingawa kwa mtazamo wa juu lilionekana kama kushindwa kwa Waislamu, lakini lilikuwa ni utangulizi wa ushindi mkubwa zaidi uliokuja baadae. Mwenyezi Mungu alilitaja kama "Fathun Mubīn" (ushindi ulio wazi), kwa kuwa katika tukio hili washirikina kwa mara ya kwanza walikubali rasmi uwepo na nguvu ya Waislamu.
Akaendelea kusema: Tukio hili linafanana na yanayotokea huko Ghaza na Palestina siku hizi, ambapo madola makubwa ya dunia yameungana kukaa mezani na kikundi kimoja tu, nacho ni Harakati ya Hamas, jambo linaloonyesha wazi nguvu na ushawishi wa Hamas.
Khatibu wa Ijumaa wa Qum akabainisha: Baada ya kipindi kifupi tangia tukio la Hudaybiyyah, nguvu za Waislamu na jamii ya Kiislamu zilipanuka sana kiasi cha kuwa chachu ya ushindi wa Makka katika mwaka wa nane wa Hijra. Ndiyo maana Suratul-Fath, ambayo ni kumbukumbu ya tukio muhimu na la kihistoria, inabeba ujumbe wa ushindi na mafanikio makubwa.
Nguzo Saba za Kimaudhui za Suratul-Fath
Ayatullah Saidi alisema: Maudhui ya Suratul-Fath yanagawanyika katika sehemu saba:
1. Sehemu ya kwanza inazungumzia bishara ya ushindi na mafanikio ambayo ni utimilifu wa ndoto ya Mtume Mtukufu (s.a.w.w.), kwani Mtume alikuwa ameota katika ndoto yake kuwa anatekeleza ‘Umrah, jambo lililoashiria ushindi wa Makka kwenye siku za usoni.
2. Sehemu ya pili inahusu matukio ya Sulhu ya Hudaybiyyah pamoja na matokeo yake yote, umuhimu wa utulivu wa mioyo ya waumini na Bai‘atur-Ridhwān.
3. Sehemu ya tatu inazungumzia nafasi tukufu ya Mtume (s.a.w.w.) na lengo lake kuu la kuwaongoza wanadamu katika uongofu, wokovu na furaha ya milele.
4. Sehemu ya nne imeelezewa kuhusu sifa na hila za wanafiki na namna walivyokuwa wakifanya hujuma dhidi ya Mtume na Uislamu.
5. Sehemu ya tano inabainisha madai yasiyo na msingi na matarajio yasiyo na mipaka ya wanafiki.
6. Sehemu ya sita inahusu umuhimu wa Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.
7. Sehemu ya saba imeelezewa sifa za wafuasi wa kweli wa Mtume (s.a.w.w.), wale wanaomtii kwa unyenyekevu na uaminifu.
Mwakilishi wa Kiongozi wa Dini (Waliyyul-Faqih) katika mkoa wa Qum akaongezea kusema:
Kwa kuzingatia maudhui yake tajiri na yenye upeo mpana, Suratul-Fath inasababisha kuimarika kwa ari ya kiimani, kuongeza uimara wa nafsi na kustawisha imani imara ndani ya mwenye imani. Baadhi ya aya za sura hii zinatoa ahadi ya nusra ya Mwenyezi Mungu na zinaleta moyo wa uthabiti na muqawama miongoni mwa wapiganaji na jamii kwa ujumla.
Maoni yako