Shirika la Habari la Hawza | Katika aya nyingi za Qur’ani Tukufu, tukio la kurejea kwa baadhi ya wafu duniani limezungumziwa.
Nabii ‘Uzayr (as)
Nabii ‘Uzayr (as), baada ya kuwa amefariki kwa muda wa miaka mia moja, alifufuliwa kutokana na matakwa ya Mwenyezi Mungu na akarudi duniani, kisha akaishi tena miaka mingi.
«أَوْ كَالَّذِي مَرَّ عَلَىٰ قَرْيَةٍ وَهِيَ خَاوِيَةٌ عَلَىٰ عُرُوشِهَا قَالَ أَنَّىٰ يُحْيِي هَٰذِهِ اللَّهُ بَعْدَ مَوْتِهَا فَأَمَاتَهُ اللَّهُ مِائَةَ عَامٍ ثُمَّ بَعَثَهُ قَالَ كَمْ لَبِثْتَ قَالَ لَبِثْتُ يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ قَالَ بَلْ لَبِثْتَ مِائَةَ عَامٍ فَانْظُرْ إِلَىٰ طَعَامِكَ وَشَرَابِكَ لَمْ يَتَسَنَّهْ وَانْظُرْ إِلَىٰ حِمَارِكَ وَلِنَجْعَلَكَ آيَةً لِلنَّاسِ وَانْظُرْ إِلَى الْعِظَامِ كَيْفَ نُنْشِزُهَا ثُمَّ نَكْسُوهَا لَحْمًا ۚ فَلَمَّا تَبَيَّنَ لَهُ قَالَ أَعْلَمُ أَنَّ اللَّهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ.»
Au kama yule aliyepita karibu na mji mmoja uliokuwa umeharibiwa, na kuta zake zikiwa zimeanguka juu ya paa zake, akasema: “Mwenyezi Mungu atayahuisha vipi huu baada ya kufa kwake?” Hapo Mwenyezi Mungu akamfisha kwa muda wa miaka mia moja, kisha akamfufua. Akamuuliza: “Umekaa kwa muda gani?” Akajibu: “Siku moja, au baadhi ya siku.” Akasema: “La! Bali umekaa miaka mia moja. Basi tazama chakula chako na kinywaji chako; havijaharibika. Na tazama punda wako (jinsi alivyoangamia). Na tumekufanya kuwa alama kwa watu. Na tazama mifupa, jinsi tunavyoiinua na kisha kuifunika kwa nyama.” Alipoelewa hayo, alisema: “Ninajua hakika kuwa Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.” (Surat al-Baqara, aya ya 259)
Wateule wa Kaum ya Bani Israil:
Watu sabini miongoni mwa wateule wa Kaum ya Nabii Musa (as) walikwenda pamoja naye hadi katika mlima wa Turi ili wawe mashahidi kwenye mazungumzo yaliyo jiri kati ya Nabii Musa (as) na Mwenyezi Mungu, na kushuhudia upokeaji wa mbao (za amri) kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Walipoona mazungumzo ya Nabii Musa as na Mwenyezi Mungu, walisema: “Ewe Musa! Hatutakuamini mpaka tumuone Mwenyezi Mungu kwa wazi.”
Nabii Musa as alikataza sharti hilo lisilo na msingi na lisilowezekana, lakini wao walisisitiza mno, na hatimaye wakapatwa na radi ya Mwenyezi Mungu na wote wakafa. Nabii Musa (as) alihuzunika sana kwa tukio hilo na akawa na hofu juu ya matokeo yake kati ya Bani Israil; kwa hivyo, akamuomba Mwenyezi Mungu awarejeshe tena duniani, ombi lake likakubaliwa na Mwenyezi Mungu akawarudisha katika maisha ya dunia.
«ثُمَّ بَعَثْنَاكُمْ مِنْ بَعْدِ مَوْتِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ.»
Kisha tukakufufueni baada ya kufa kwenu ili mpate kushukuru. (Surat al-Baqara, aya 56)
Kurejea Duniani kwa Wafu Katika Siku Zijazo
«وَیَوْمَ نَحْشُرُ مِنْ كُلِّ أُمَّةٍ فَوْجًا مِمَّنْ یُكَذِّبُ بِآیَاتِنَا فَهُمْ یُوزَعُونَ.»
Na Siku tutapo kusanya kutoka kila umma kundi katika wanao kadhibisha Ishara zetu, nao watagawanywa mafungu mafungu. (Surat al-Naml, aya 83)
Katika aya hii, imezungumzwa siku ambayo baadhi ya watu watafufuliwa. Hii inaashiria siku nyingine isiyo ya Kiyama, kwa sababu katika Siku ya Kiyama watu wote kutoka wa mwanzo hadi wa mwisho watafufuliwa, kama Qur’ani Tukufu inavyosema:
«وَیَوْمَ نُسَیِّرُ الْجِبَالَ وَتَرَى الْأَرْضَ بَارِزَةً وَحَشَرْنَاهُمْ فَلَمْ نُغَادِرْ مِنْهُمْ أَحَدًا.»
Na siku tutapo iondoa milima na ukaiona ardhi iwazi, na tukawafufua, wala hatutamwacha hata mmoja kati yao. (Surat al-Kahf, aya 47)
Marehemu Tabrasi katika tafsiri ya "Majmaʿ al-Bayan", chini ya aya ya 83 ya surat al-Naml, ameandika kuwa kwa mujibu wa riwaya nyingi kutoka kwa Ahlulbayt (a.s), aya hii inamhusu kundi la Mashia wa Imam Mahdi (as) na pia baadhi ya maadui wa Imam huyo ambao watarejea duniani katika kipindi cha kudhihiri kwake.
Aya nyingine katika Qur’ani pia inaashiria kurejea kwa wafu duniani katika siku zijazo:
«وَحَرَامٌ عَلَىٰ قَرْیَةٍ أَهْلَكْنَاهَا أَنَّهُمْ لَا یَرْجِعُونَ.»
Na haiwi kwa wana-mji tulio uangamiza, ya kwamba hawatarejea. (Surat al-Anbiya, aya 95)
Aya hii pia ni miongoni mwa dalili muhimu zaidi za "rajʿa" (kurejea kwa wafu duniani), kwa sababu katika Siku ya Kiyama watu wote—wakiwemo wale walioteketezwa kwa adhabu ya Mwenyezi Mungu—watarejea, kama Qur’ani inavyofundisha.
Imam al-Baqir na Imam as-Sadiq (a.s) wamesema katika tafsiri ya aya hii:
«فهذه الآیة من أعظم الدلالة فی الرجعة، لان أحدا من أهل الاسلام لا ینکر أن الناس کلهم یرجعون إلی القیامة، من هلک ومن لم یهلک، فقوله: «لا یرجعون» عنی فی الرجعة، فأما إلی القیامة یرجعون حتی یدخلوا النار.»
Aya hii ni miongoni mwa dalili kubwa zaidi juu ya kurudi kwa wafu duniani (rajʿa), kwa sababu hakuna Muislamu hata mmoja anayekataa kwamba watu wote watarudi katika Kiyama, wawe walioteketezwa au wasiokuwa. Basi kauli ya Mwenyezi Mungu: "hawatarejea" ina maana ya kutorejea duniani, lakini katika Kiyama wote watarudi hadi waingie Motoni. (Bihār al-Anwār, juzuu ya 53, uk. 52)
Utafiti huu unaendelea...
Imenukuliwa kutoka katika kitabu "Negin-e Āfarinish" huku ikifanyiwa marekebisho kiasi
Maoni yako