Jumatatu 6 Aprili 2026 - 14:07
Ayatullah A’rafi Alaani Mashambulizi ya Marekani na Utawala wa Kizayuni Dhidi ya Maeneo ya Ibada na Urithi wa Kihistoria

Hawza/ Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, ametoa tamko la kulaani mashambulizi ya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya maeneo ya kidini na kihistoria.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, maandishi ya tamko la Ayatullah A’rafi, Mkurugenzi wa Hawza, la kulaani mashambulizi ya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya maeneo ya kidini na kihistoria ni kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

Wala msikiuke mipaka, hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wanaokiuka mipaka.
(Suratul Baqarah, aya ya 190).

Kwa jumuiya ya kimataifa, wafuasi wa dini zinazomuamini Mungu mmoja, na hususan viongozi watukufu wa kidini.

Amani ya Mwenyezi Mungu, rehema Zake na baraka Zake ziwe juu yenu.

Kwa mara nyingine tena, mikono michafu ya ubeberu wa kimataifa, yaani utawala wa kihalifu wa Marekani na Israel, imejichafua kwa kutenda uhalifu mwingine dhidi ya maeneo matakatifu na urithi wa kiroho wa mwanadamu.

Mashambulizi haya si hatua ya kijeshi pekee, bali ni mapambano ya moja kwa moja kati ya “wafuasi wa Shetani” na “majeshi ya Mwenyezi Mungu”, pamoja na dharau ya wazi dhidi ya tunu zote za pamoja za kibinadamu na kidini.

Baada ya mashambulizi ya kinyama dhidi ya maeneo ya kidini, sehemu za kuzuru, misikiti na Husseiniyyah Kuu ya Zanjan, ambayo ni mahali pa kukutana watu wema na wapenzi wa Imam Hussein (as),

mnamo tarehe 12 Farvardin, sawa na tarehe 1 Aprili 2026, siku ya maadhimisho ya kuanzishwa Jamhuri ya Kiislamu na kuelekea tarehe 13 Farvardin, ambayo kwa mujibu wa kauli ya Kiongozi Mkuu (Mwenyezi Mungu aendeleze maisha yake) ni siku ya matumaini na uhai, yalifanyika mashambulizi ya kigaidi ya makombora bila kujali madhara yake. Mashambulizi hayo yalilenga Kanisa Kuu la Waorthodoksi la Mtakatifu Nicholas mjini Tehran, na kusababisha uharibifu mkubwa katika mkusanyiko wa majengo ya kihistoria, kidini na matakatifu ya Wakristo.

Kuvunjwa madirisha na milango, kuporomoka kwa sehemu ya paa la nyumba ya wazee, ambayo wakati huo bado ilikuwa na wazee wasio na hatia waliokuwa wakiishi humo, pamoja na kulihujumu na kulivunjia heshima kanisa wakati wa uvamizi usio halali, ni kilele cha ukatili na uadui dhidi ya dini zote za Mwenyezi Mungu.

Mimi, kwa nafasi yangu ya Ukurugenzi wa Hawza, taasisi ambayo daima imekuwa mtetezi wa waliodhulumiwa, muungaji mkono wa kuishi kwa amani baina ya wafuasi wa dini mbalimbali na mtetezi wa kuleta ukaribu baina ya madhehebu, ninaukemea vikali kabisa uhalifu huu na kutangaza yafuatayo:

Kwanza: Maeneo ya kidini, yakiwemo misikiti, Husseiniyyah, makanisa, masinagogi, maeneo yanayoelekezwa katika ibada na sehemu za kufanyia ibada za dini zinazomuamini Mungu mmoja, ni mipaka myekundu ambayo hairuhusiwi kuvukwa. Uvamizi au ukiukaji wowote dhidi ya maeneo hayo, iwe Palestina, Lebanon, Syria, Iran au sehemu nyingine yoyote duniani, ni mfano wa “kupigana vita dhidi ya Mwenyezi Mungu na dini Yake”, na ni uhalifu dhidi ya ubinadamu pamoja na urithi wa kidini na kiutamaduni.

Pili: Ninatoa wito kwa Umoja wa Mataifa, UNESCO, Vatican, Baraza la Makanisa Duniani na viongozi wote wa kidini duniani wasikae kimya mbele ya vitendo hivi vya wazi vya kuvunjia heshima maeneo matakatifu na mashambulizi dhidi ya misikiti, Haram Tukufu, Husseiniyyah, sehemu za ibada, makanisa na masinagogi.

Ikiwa leo msikiti na kanisa mjini Tehran vitashambuliwa na jambo hilo likapita bila jibu lolote, kesho tunapaswa kutarajia majanga ya aina hii kutokea katika nchi zipi? Na ni nani atakayelinda na kusimamia usalama wa maeneo matakatifu ya Mwenyezi Mungu duniani kote?

Tatu: Ninawaonya wafuasi wa dini zote za mbinguni kwamba; ubeberu wa kimataifa na utawala wa Kizayuni si maadui wa Waislamu pekee, bali pia ni maadui wa kila mtu anayemuamini Mwenyezi Mungu, Mitume Wake na Vitabu Vyake vya mbinguni.

Leo ni zamu ya Husseiniyyah Kuu ya Zanjan na Kanisa la Waorthodoksi mjini Tehran; kesho huenda ikawa zamu ya sehemu nyingine yoyote ya ibada, umoja wa dini zinazomuamini Mungu mmoja mbele ya jitu hili linalokula dini ni ulazima usioweza kupingwa.

Nne: Ninatoa wito kwa Hawza za Elimu za Kidini, vyuo vikuu vya ulimwengu wa Kiislamu na watu wote wapenda uhuru duniani, watoe matamko madhubuti, waandae mikusanyiko ya kupinga mashambulizi haya na kuchukua hatua za kidiplomasia, ili wasiruhusu uhalifu huu kufanywa kuwa jambo la kawaida linalokubalika.

Damu ya kila mtu asiye na hatia na uharibifu wa kila eneo lililojengwa kwa jina la Mwenyezi Mungu vitachochea dhamiri hai ya ubinadamu kusimama na kupaza sauti.

Mwisho, huku nikitangaza mshikamano wangu na watu wote wanaomuamini Mwenyezi Mungu, jumuiya ya Waorthodoksi wa Urusi na Wakristo wote wa Iran na duniani kote, ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu aiokoe jamii ya wanadamu haraka iwezekanavyo kutokana na shari ya madhalimu na watu wenye tabia za kishetani wa Marekani na Israel.

"Wameruhusiwa (kupigana) wale wanaopigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa, na hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwapa ushindi".

Ayatullah Alireza A’rafi
Mkurugenzi wa Hawza, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha