Jumatatu 9 Novemba 2026 - 22:54
Ayatullah al-Udhma Wahid Khorasani Aruhusiwa kutoka Hospitalini

Hawza/ Ofisi ya Ayatullah Wahid Khorasani imetangaza kuwa, kwa fadhila na rehema zisizo na kikomo za Mwenyezi Mungu Mtukufu, baraka za neema za Maimamu wa Ahlul-Bayt (as), pamoja na baraka za dua na maombi ya waumini, Ayatullah huyo amefanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kuruhusiwa kutoka hospitalini, na kurejea nyumbani kwake.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Ayatullah Wahid Khorasani kufuatia kuruhusiwa kwake kutoka hospitalini inasema kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

Ewe Mwenyezi Mungu! Mteremshie rehema zako Fatimah, baba yake, mume wake, watoto wake na siri iliyowekwa ndani yake, kwa idadi ya mambo yote yaliyozungukwa na elimu Yako.

Kufuatia kulazwa hospitalini Ayatullah al-Udhma Wahid Khorasani (Mwenyezi Mungu aendelee kumhifadhi), idadi kubwa ya waumini na wapenzi wake, walioko ndani na nje ya nchi, waliendelea kumuombea kwa Mwenyezi Mungu na kuandaa majlisi za kutawasali kwa Mola wao. Hasa katika siku hizi zinazohusishwa na Bibi Fatimah al-Siddiqah al-Kubra (as), waumini hao walielekeza nyoyo zao katika kumtaja na kutawasali kupitia utukufu wa Bibi huyo, wakimuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu amponye na amjalie Ayatullah huyo afya njema.

Kwa fadhila na rehema zisizo na kikomo za Mwenyezi Mungu Mtukufu, baraka za neema za Maimamu wa Ahlul-Bayt (as), pamoja na baraka za dua na maombi hayo, Ayatullah huyo amefanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kuruhusiwa kutoka hospitalini, na kurejea nyumbani kwake.

Tunatoa shukrani na kutambua kwa dhati upendo uliooneshwa na waumini wote, wapenzi na wafuasi wake katika masuala ya kidini, viongozi na watu mashuhuri wa kitaifa, pamoja na watu wote wenye heshima ambao walionesha kumjali kwa kumuombea, kumpigia simu, kumtumia ujumbe au kueleza nia yao ya kumtembelea, huku wakiulizia hali yake njema.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa baraka za uangalizi na mazingatio ya Mtukufu Imam Mahdi (aj), aharakishe kudhihiri kwake, awajaalie watu wote afya njema, siha na mwisho mwema wa maisha yao. Pia, tunamuomba awaponye wagonjwa wote uponyaji wa haraka na kamili.

Vilevile, tunatoa shukrani zetu za dhati kwa madaktari, wauguzi, watumishi wengine wa sekta ya afya na wafanyakazi wa hospitali kwa juhudi na huduma zao. Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mkarimu awalipe kwa malipo makubwa, awajaalie afya njema, heshima na mafanikio zaidi katika kazi na maisha yao.

Aidha, tunaendelea kuwaomba waumini wote wasimnyime Ayatullah huyo dua zao njema, na waendelee kumuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu amjaalie afya njema na siha endelevu.

18 Aban 1405 Hijria Shamsia, / 9 Novemba 2026.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha