Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Nabila Syed, mwanamke Muislamu mwenye umri wa miaka 27, mwenye asili ya India na Marekani, kutoka chama cha Democratic, amemshinda mpinzani wake wa chama cha Republican kwa kupata asilimia 57 ya kura, na hivyo kujinyakulia kiti cha Seneta katika jimbo la Illinois.
Mwanasiasa huyo kijana Muislamu aliingia kwa mara ya kwanza katika Bunge la kutunga sheria la jimbo hilo akiwa na umri wa miaka 23. Syed ameshinda katika jimbo dogo la uchaguzi namba 26 la Seneti ya Illinois, na katika uchaguzi wa katikati ya muhula uliofanyika siku ya Jumanne nchini Marekani, ameongeza ushindi mwingine kwa chama cha Democratic.
Hatua muhimu katika safari yake ya kisiasa ilijitokeza baada ya Donald Trump kushinda mara ya kwanza uchaguzi wa urais mwaka 2016. Wakati huo, Syed alisema kuwa kuongezeka kwa uhasama dhidi ya Waislamu na wahamiaji kulimpa msukumo wa kuingia katika shughuli za kijamii na ulingo wa siasa.
Syed alizaliwa na kukulia katika jimbo la Illinois, akiwa mtoto wa wazazi wahamiaji wenye asili ya India kutoka mji wa Hyderabad. Alisomea Sayansi ya Siasa na Usimamizi wa Biashara katika Chuo Kikuu cha California, Berkeley.
Hapo awali, Syed amewahi kueleza jinsi uzoefu wake wa kukumbana na ubaguzi na chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) ulivyoathiri uamuzi wake wa kuingia katika taaluma ya siasa.
Akiwa amekulia katika mazingira ya Marekani kama Muislamu, anakumbuka kwamba baadhi ya wanafunzi wenzake walikuwa wakimwita «gaidi»; wakati mwingine kwa mzaha na nyakati nyingine kwa uzito. Pia alisimulia tukio lililotokea Washington, D.C., ambapo mtu mmoja alijaribu kumtemea mate alipokuwa akishiriki katika programu ya mafunzo.
Syed amehusisha matukio ya aina hiyo na mazingira ya kisiasa yaliyotawala nchini Marekani baada ya ushindi wa Trump katika uchaguzi wa mwaka 2016. Alisema kuwa; alihisi Waislamu na makundi mengine ya wachache hawapatiwi nafasi na uzingatiaji unaostahili katika nchi ambayo yeye mwenyewe amekulia.
Chanzo: New Arab.
Maoni yako