Jumamosi 7 Novemba 2026 - 08:00
Msimamo wa wananchi wa Iran mbele ya mashinikizo ndio utakaowezesha kutimia ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kuwapa ushindi

Hawza/ Msimamizi wa Haram Tukufu ya Mtukufu Abdul Adhim (a.s), huku akisisitiza kuwa dhuluma na madola dhalimu havina uhai wa kudumu, amesema kuwa kusimama imara kwa wananchi wa Iran mbele ya vitisho na mashinikizo ndiko kutakakoandaa mazingira ya kutimia ahadi hiyo ya Mwenyezi Mungu na ushindi wa haki.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Qadhi Askar, katika mahojiano na mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza mjini Tehran, amesisitiza kuwa; mwenendo na kanuni za Mwenyezi Mungu zimejengwa juu ya kuangamizwa dhuluma na ushindi wa haki. Amesema historia ya Mitume na simulizi za tawala dhalimu zinaonesha kuwa madola yaliyojengwa juu ya dhuluma hayadumu, na ingawa kutimia ahadi za Mwenyezi Mungu kunaweza kuchukua muda kutokana na sababu mbalimbali, hatimaye msaada wa Mwenyezi Mungu utawafikia Waumini na wale wanaosimama imara katika njia ya haki.

Msimamizi wa Haram Tukufu ya Mtukufu Abdul Adhim (a.s) ameeleza kuwa; historia ndiyo ushahidi bora zaidi wa kutodumu dhuluma, akiongeza kuwa tukirejea historia ya maisha ya mwanadamu, kuanzia kisa cha Habil na Qabil, historia za Mitume hadi zama za Mtume wa Uislamu (s.a.w.w), tutaona wazi kwamba madhalimu wametoweka, lakini majina na kumbukumbu za watu waliopigania haki zimeendelea kubaki.

Amesema kuwa Firauni na madola dhalimu ya zama za Nabii Musa (a.s), pamoja na watu kama Abu Jahl na Abu Sufyan wa zama za ujahilia, wote walitoweka, lakini jina la Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) bado linaendelea kuishi duniani kote. Kadhalika, hakuna jina la Muawiya na Yazid lililobaki kama mfano au shakhsia ya kudumu inayostahili kuigwa, ilhali jina la Imam Hussein (a.s) linaheshimiwa duniani kote na miongoni mwa watu wanaopenda uhuru.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Qadhi Askar, huku akibainisha kuwa ili kushuhudia kuangamizwa madhalimu haipaswi kutarajiwa kwamba mara tu baada ya kutokea kwa kila dhuluma, adhabu ya Mwenyezi Mungu itashuka papo hapo, amefafanua kuwa dunia ni mahali pa mitihani, na miongoni mwa mitihani hiyo ni namna ambavyo wanadamu wanavyokabiliana na dhuluma na matatizo.

Amesema kuwa; wakati mwingine mambo huenda kwa namna ambayo Waumini hujikuta wakijiuliza: Je, msaada wa Mwenyezi Mungu utafika lini? Hali hii ndiyo inayoelezwa na Qur’ani Tukufu katika kauli yake: «مَتَیٰ نَصْرُ اللَّهِ» (Msaada wa Mwenyezi Mungu utakuja lini?), kisha kwa upande mwengine inatoa ahadi kwa kusema: «أَلَا إِنَّ نَصْرَ اللَّهِ قَرِیبٌ» (Hakika, msaada wa Mwenyezi Mungu uko karibu). Kwa hiyo, hapaswi mtu kukata tamaa akiwa katika njia ya haki.

Akizungumzia nafasi ya Kiongozi Shahidi na misisitizo yake kuhusu ushindi wa wananchi wa Iran, amesema kuwa; ingawa Kiongozi Shahidi kwa sasa hayupo tena pamoja nasi kimwili, mawazo, fikra na maelekezo yake bado vinaishi ndani ya jamii. Ameeleza kuwa mara nyingi Kiongozi huyo alikuwa akizungumzia kwa yakini ushindi wa wananchi wa Iran, akisisitiza kuwa taifa lililosimama imara katika njia ya Mwenyezi Mungu na kutoa mashahidi hatimaye litapata ushindi.

Msimamizi wa Haram ya Mtukufu Abdul Adhim (a.s), akizungumzia matukio na vitisho vya hivi karibuni dhidi ya Iran, amesema kuwa; katika miezi iliyopita, maafisa wa Marekani wamezungumza mara kadhaa kuhusu kuiangamiza Iran na ustaarabu wa Kiirani, huku wakitoa vitisho mbalimbali. Hata hivyo, wananchi wa Iran hawakuogopa, bali kwa kutegemea moyo wa uthabiti walioujenga kupitia maelekezo ya Kiongozi wao Shahidi, waliendelea kubaki imara katika medani. Ameongeza kuwa; uwepo wa kudumu wa wananchi katika viwanja vya mikusanyiko na msimamo thabiti wa vikosi vinavyolinda nchi, hususan katika maeneo ya mipakani, umeonesha kuwa wananchi wa Iran hawako tayari kurudi nyuma mbele ya vitisho.

Akisisitiza kuwa Muqawama pia una gharama zake, amesema: Inawezekana tukapata madhara katika njia ya kusimama imara na tukatoa mashahidi, lakini imani yetu ni kwamba iwapo tutabaki thabiti katika njia ya haki, hatimaye ushindi utakuwa wa Uislamu na Iran.

Katika kuendeleza mazungumzo yake, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Qadhi Askar ameyataja mabadiliko ya kisiasa nchini Marekani na katika utawala wa Kizayuni kuwa ni miongoni mwa ishara zinazopaswa kuchambuliwa katika muktadha wa ahadi ya Mwenyezi Mungu kuhusu hatima ya madhalimu. Amesema kuwa; mabadiliko ya hivi karibuni ya uchaguzi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na nchini Marekani yamekuwa na athari kwa serikali zinazounga mkono utawala wa Kizayuni.

Akizungumzia kushindwa kwa Netanyahu kupata idadi ya kura alizohitaji pamoja na misimamo ya wapinzani wake wa kisiasa, ameeleza matumaini yake kwamba; mwenendo wa mabadiliko hayo utasababisha kuondoka kwake madarakani na kufikishwa mahakamani kutokana na uhalifu wa kivita alioufanya.

Vilevile, akizungumzia matokeo ya uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani na kushindwa wafuasi wa Republican katika uchaguzi amesema kuwa; baadhi ya vyombo vya habari na wachambuzi wameyatafsiri matukio hayo kuwa ni tetemeko la kisiasa. Ameongeza kuwa hata Trump, katika matamshi yake, amehusisha kutoridhika sehemu ya wananchi wa Marekani na matokeo ya vita, kufungwa Mlango-Bahari wa Hormuz na athari zake katika hali ya upatikanaji wa nishati na kupanda mfumuko wa bei.

Msimamizi wa Haram ya Mtukufu Abdul Adhim (a.s), huku akieleza kuwa haoni tofauti kati ya wafuasi wa Republican na Democrat katika msingi wa sera za Marekani dhidi ya Iran, ameongeza kuwa; suala kuu ni kwamba Muqawama wa Iran umesababisha gharama kwa Marekani na washirika wake.

Akizungumzia mashambulizi na vitendo vya kikatili vilivyofanyika nchini Iran, pamoja na kuuawa kishahidi watoto, makamanda na Kiongozi Shahidi, amesisitiza kuwa; madhalimu hawapaswi kudhani kwamba kwa kutenda uhalifu, basi jalada la matendo yao litakuwa limefungwa. Amesema kuwa Mwenyezi Mungu yuko macho na anawangojea madhalimu, na kwamba ni lazima waonjeshwe matokeo ya dhuluma zao.

Ameeleza kuwa suala hili haliihusu Iran pekee, bali hatima ya Saddam ni mfano mwingine wa wazi wa jambo hilo. Amesema kuwa; madola yaliyokuwa yakimuunga mkono Saddam wakati fulani, hatimaye yaligeuka na kusimama dhidi yake, na serikali yake ikaanguka.

Msimamizi wa Haram ya Mtukufu Abdul Adhim (a.s), katika kuendeleza mazungumzo yake, amezungumzia nafasi ya kimkakati ya Mlango-Bahari wa Hormuz, akisema kuwa matukio ya hivi karibuni yameonesha kwa kiwango gani nafasi ya kijiografia na kimkakati ya Iran ina umuhimu  duniani.

Amefafanua kuwa kuwekwa vikwazo katika usafiri wa majini kupitia njia hiyo kunaweza kuathiri soko la nishati, bei za mafuta na bidhaa katika nchi mbalimbali, hususan barani Ulaya, na kusababisha shinikizo kubwa la kiuchumi.

Akizungumzia pia nafasi ya Muqawama wa Yemen na eneo la Bab al-Mandab, amesema kuwa; wananchi wa Yemen, licha ya kuwa na uwezo na vifaa vichache, wameendelea kusimama imara. Aidha, amebainisha kuwa eneo la kimkakati la Bab al-Mandab nalo lina umuhimu wa kipekee.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha